loader
Dstv Habarileo  Mobile
Hongera Rais Samia kwa maelekezo ya tozo

Hongera Rais Samia kwa maelekezo ya tozo

MOJA ya sifa kubwa ya kiongozi ni kuwa msikivu na kujali maoni ya watu anaowaongoza.

Hatua ya Rais Samia Suluhu Hassan kutoa maelekezo kwa Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na ya Mawasiliano ya Teknolojia ya Habari kuhusu tozo za miamala ya simu, inastahili pongezi.

Kwa mujibu wa Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba, Rais Samia ameguswa na jambo hilo, amesikia maoni ya Watanzania.

Amesema wanaenda kuyafanyia kazi malalamiko hayo ya wananchi kwa maelekezo ya Rais Samia.

Uamuzi wa Rais kuingilia kati suala hilo unastahili pongezi kwa sababu umeonesha na kudhihirisha jinsi yeye binafsi na serikali yake wanavyojali maisha ya Watanzania wanaowaongoza.

Kilio cha kutaka tozo za miamala ya simu ziangaliwe kwa hakika kilisikika kutoka kwa wananchi wengi, na hiyo ilidhihirisha kuwa kuna jambo linapaswa kuangaliwa upya katika nia nzuri ya serikali kukusanya kodi.

Kama alivyoeleza Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu, ni vyema wananchi wakawa watulivu kwenye jambo hilo kwa kuwa tayari Rais Samia amelitolea maelekezo na hivyo watalaamu wanalifanyia kazi.

Lakini wakati tunampongeza Rais Samia kwa maelekezo yake ambayo yamepokelewa kwa furaha na Watanzania wengi na kupongeza hatua yake hiyo, tungependa kusisitiza umuhimu wa kulipa kodi kwa maendeleo.

Ni ukweli usiofichika kwamba, Serikali ya Awamu ya Sita inatekeleza miradi mingi ya maendeleo ambayo inahitaji fedha nyingi ili kuweza kuikamilisha.

Fedha hizo hazipatikani kwingine bali ni kutokana na kodi za Watanzania wenyewe kutokana na huduma mbalimbali wanazozipata.

Kwa mfano, serikali imepanga kujenga madaraja, barabara, kupeleka umeme katika vijiji vyote vilivyobaki nchini, vivuko, ujenzi wa Reli ya Kisasa, Bwawa la Julius Nyerere, zahanati, hospitali za wilaya, mikoa na rufaa, kulipa mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu na kupeleka maji safi na salama kote nchini.

Kwa hiyo, miradi hii inahitaji fedha nyingi na ili kuikamilisha, ni lazima Watanzania walipe kodi ili wanapokwenda hospitalini wasilalamike kukosa dawa, wasilalamike kuwa hakuna maji safi na salama, kwamba barabara ni mbovu, kwamba wanafunzi hawana madarasa na wanakaa chini, kwamba mikopo ya elimu ya juu haitoshi, na mengine mengi.

Kwa msingi huo, ni lazima kila Mtanzania ajione na ajisikie kuwa anao wajibu wa kulipa kodi ili kuchangia katika maendeleo ya taifa kwa sababu hakuna mjomba kutoka nje atakayekuwa na uchungu wa kutoa fedha zake ili kuwasaidia Watanzania, bali Watanzania wenyewe kujenga nchi yao.

Hivyo wakati serikali ikifanyia kazi maoni ya wananchi kuhusu kodi ya tozo za miamala ya simu, jamii ya Watanzania ikumbuke kuwa inao wajibu wa kulipa kodi ili kupata huduma bora za kijamii na kukuza uchumi wa nchi, kwani mjenga nchi ni mwananchi mwenyewe.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/dfc64cfca4bf5400536b033a02dd4a6d.jpg

Miradi ya Maendeleo katika halmashauri za Serengeti, ...

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi