loader
Siku ya Kuzuia Kuzama itukumbushe tahadhari safari za majini

Siku ya Kuzuia Kuzama itukumbushe tahadhari safari za majini

KWA mara ya kwanza leo dunia inaadhimisha Siku ya Kuzuia Kuzama Duniani ikiwa na kaulimbiu isemayo: ‘Kuzama Kunazuilika, Chukua Tahadhari.’

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirika la Afya Duniani (WHO), kwa kutambua uhusiano uliopo kati ya kuzama majini na maendeleo na kwamba zaidi ya asilimia 90 ya vifo vinatokea kwenye nchi zinazoendelea, Aprili mwaka huu, Umoja wa Mataifa ulijadili na kuridhia Julai 25 kila mwaka iwe siku rasmi ya kukumbusha nchi zote duniani kuchukua hatua stahiki kuzuia vifo vitokanavyo na kuzama majini.

Wakati dunia ikiadhimisha siku hii kwa mara ya kwanza, Tanzania nayo ni miongoni mwa nchi ambazo zimewahi kukumbwa na matukio makubwa ya watu kufariki dunia kutokana na kuzama majini kwa vyombo vyao vya usafiri.

Miongoni mwa matukio hayo yaliyosababisha vifo vya watu wengi nchini ni pamoja na kuzama kwa Meli ya Mv Bukoba katika Ziwa Victoria mwaka 1996. Takriban watu 800 walipoteza maisha.

Matukio mengine ya hivi karibuni ni kuzama kwa Kivuko cha Mv Nyerere katika Ziwa Victoria mwaka 2018. Takribani watu 200 walipoteza maisha. Mwaka 2011 meli ya MV Spice Islander iilizama katika Bahari ya Hindi, Zanzibar na miili iliyopatikana na kuzikwa ilikuwa 243.

Kivuko cha MV Kilombero nacho kilizama mwaka 2003 na kuua watu kadhaa. Kwa msingi huo, tunapofanya maadhimisho haya, ipo haja kubwa tukumbuke vyanzo vya ajali za majini zinazosababisha watu kuzama na kufariki dunia na kuchukua hatua makini kuepukana nazo.

Hizi ni pamoja na uzembe katika kukagua na kufanyia ukarabati vyombo hivyo, tamaa ya kuzidisha mizigo na abiria na kukosekana mavazi maalumu ya kujiokolea tena kwa idadi ya kutosha.

Sisi tunapongeza kuanza kwa maadhimisho haya ili kukumbusha jamii umuhimu wa kuchukua tahadhari katika kutumia vyombo vya majini na mambo mengine hivyo, kuepusha matukio ya kuzama.

Haya yatasaidia umma kupata taarifa na elimu kuhusu vifo vitokanavyo na kuzama kwenye maji ili kushirikiana na kuokoa maisha ya maelfu ya wavuvi, mabaharia na wasafiri wa majini.

Sisi tunaamini kuwa, vifo vya kuzama majini vinaweza kuepukika endapo wadau mbalimbali watachukua hatua za makusudi na za tahadhari ikiwamo kujenga uwezo wa kuogelea kwa makundi mbalimbaliwakiwamo watoto na wavuvi.

Hii ni kwa kuwa miongoni mwa sababu za vifo vya kuzama majini zinazoanishwa na wadau mbalimbali ni pamoja na watu kutojua kuogelea, kutozingatia taratibu za usafiri majini ikiwemo kuzidisha uzito, hali mbaya ya hewa, kutokuwepo viashiria vya maeneo hatarishi na ukosefu wa elimu kwa umma.

Ndio maana tunasema ni vyema maamlaka husika zikatilia mkazo vyombo vyote vya usafiri majini kuwa na vifaa vya kutosha vya kuokolea maisha zikiwamo jaketi za kuokolea maisha, boti za kuokolea maisha na maboya.

Tunasema: “Siku ya Kuzuia Kuzama itukumbushe tahadhari safari za majini sambamba na elimu sahihi nanmna ya kujiokoa kila kabla ya safari kama inavyofanyika katika ndege.”

foto
Mwandishi: Mhariri

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi