loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kihamia ataja vikwazo vya masoko ya mazao

Kihamia ataja vikwazo vya masoko ya mazao

TANZANIA ina uwezo mkubwa wa kutosheleza masoko ya mazao duniani kutokana na uwepo wa ardhi ya kutosha pamoja na hali nzuri ya hewa japokuwa hilo linakwama kutokana na kilimo cha mazoea pamoja na kutotumia utaalamu wa kilimo bora.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Arusha, Dk Athumani Kihamia alisema hayo katika maadhimisho ya Siku ya Maonesho ya Kilimo Biashara yaliyofanyika katika Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), Kituo cha Selian Arusha.

Kihamia alisema pamoja na fursa iliyopo, bado kuna yapo mambo mengi yanayochangia kutotosheleza masoko hayo duniani ukiwamo uzalishaji mdogo katika eneo na uwepo wa magonjwa na wadudu waharibifu.

Mambo mengine yanayochangia kutotosheleza mahitaji ya soko kwa mujibu wa Kihamia, ni pamoja na athari za mabadiliko ya tabianchi na gharama kubwa ya pembejeo ikilinganishwa na kipato cha wakulima.

Lingine Dk Kihamia alisema ni kutokuwa na vikundi vya wakulima vinavyokopesheka, taarifa za utafiti kutokufikia maeneo mengi ya nchi pamoja na changamoto ya uwepo wa miundombinu hafifu ya hifadhi ya mazao.

Alisema ili kuongeza uzalishaji na tija katika kilimo, taasisi za umma na binafsi zihakikishe wakulima wanatumia mbegu bora ambazo hazishambuliwi na magonjwa, zenye mavuno mengi pamoja na matumizi ya viuatilifu.

Alihimiza wakulima kuzingatia maelekezo ya wataalamu ili kuwa na mazao mengi na bora yatayokubalika katika masoko ya ndani na nje ya nchi.

Awali, Mkurugenzi Mkuu wa Tari, Dk Geofrey Mkamilo alisema taasisi hiyo imeweka mkazo mkubwa katika teknolojia zilizopo ili zisambazwe kwa wakulima na wadau mbalimbali na kuchangia katika ukuaji wa uchumi.

Alisema kwa kuwa takriban asilimia 65 ya malighafi ya viwanda inatokana na kilimo, ni jukumu la kila mmoja kutumia kanuni za kilimo bora ili kuzalisha malighafi za zinazohitajika katika viwanda nchini. Mkurugenzi wa Kituo cha Selian, Dk Joseph Ndunguru, alisema maonesho hayo yanahamasisha wadau kupokea teknolojia bora kutokana na elimu na maarifa waliyopata na hivyo, kuongeza uzalishaji na tija.

“Kwa mfano wakulima wanaotumia mbegu bora za mahindi, wameweza kuongeza uzalishaji kutoka tani moja kwa hekta hadi tani nane na maharage kutoka kutoka tani moja hadi tani tatu kwa hekta,” alisema.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/ff01e951c229a70bf864cf9bc59d0ede.jpg

SHIRIKISHO la Wafanyabiashara na wenye viwanda nchini ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi, Arusha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi