loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mtaka atoa wito kwa benki kuwawezesha wakandarasi

Mtaka atoa wito kwa benki kuwawezesha wakandarasi

MKUU wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka ametoa wito kwa Benki ya Exim Tanzania kuangalia namna ya kuwawezesha wakandarasi wa ndani ya nchi ili waweze kutekeleza miradi mikubwa ndani na nje ya nchi.

Mtaka alitoa wito huo mwishoni mwa wiki katika hafla ya chakula cha jioni iliyoandaliwa na Benki ya Exim kwa ajili ya wateja wake wa jijini Dodoma huku akiitolea mfano wa Benki ya Exim China ambayo imekuwa ikiwawezesha wakandarasi kutoka taifa hilo lenye nguvu za kiuchumi barani Asia.

“Nimefurahishwa na ufunguzi wa tawi jipya la Benki ya Exim hapa jijini Dodoma, hivyo basi pamoja na kuongeza mtandao na huduma kwa wateja wenu, nashauri ni vema zaidi pia muangalie namna ya kuwasaidia wakandarasi wetu wa ndani ili waweze kutekeleza miradi mikubwa ndani na nje ya nchi ikiwemo kwenye mataifa ambayo tayari Exim ina matawi kama Comoro, Djibouti, Uganda na Ethiopia,’’ Mkuu wa Mkoa lisema.

Aliongeza kuwa  kampuni kubwa zinazotekeleza miradi yake hapa nchini zimekuwa zikiwezeshwa na benki kutoka mataifa yao huku akisisitiza: “ipo haja kwa benki hapa nchini kuiga mfano huo.”

Mbali na hilo, Mtaka alitoa ushauri kwa benki hiyo kuangalia namna ya kusaidia kupunguza tatizo la ajira kwa vijana wanaohitimu vyuo hapa nchini kwa kufadhili miradi inayotokana na mawazo yao kwa kuanzisha mfuko maalum unaofanana na ule wa uwajibikaji kwa jamii (CSR).

“Badala ya kuwa na mpango wa uwajibikaji kwa jamii peke yake (CSR) benki ya Exim mnaweza kuwa na mpango wa uwekezaji kwa jamii (CSI), ambao pamoja na mambo mengine, ulenge kusaidia wahitimu wa elimu ya juu wakiwa mmoja mmoja au vikundi kwa kuwapatia mikopo ili waweze kutekeleza mawazo yao,’’ alisema.

Akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkurugenzi wa Bodi ya Benki hiyo, Irene Mlola alisema taasisi hiyo ya kifedha imepokea mawazo ya RC Mtaka na kuahidi kuyafanyia kazi huku akisisitiza uwepo wa tawi la benki hiyo Dodoma ni mwanzo wa kuwasaidia wakazi wa jiji hilo kukuza uchumi wao kwa kuwasogezea huduma za kifedha karibu.

Alisema benki hiyo pia imekuwa mstari wa mbele kuhakikisha inashiriki kikamilifu kujenga uchumi wa nchi kwa kushirikiana na serikali na sekta binafsi ili kufanikisha uchumi wa viwanda.

Awali, akizungumza kwenye hafla hiyo, Mkuu wa Huduma za Wateja Wadogo na wa Kati wa Benki ya Exim, Andrew Lyimo pamoja na kuwashukuru wakazi wa jiji la Dodoma kwa kuipokea vema benki hiyo, aliahidi kuwa benki hiyo imejipanga kutoa huduma za kibenki zinazoendana na mahitaji yao sambamba na ubunifu unaotokana na uwekezaji kwenye huduma za kidigitali.

“Pamoja na uwekezaji kwenye huduma kidigitali, wakazi wa Dodoma wajipange kufurahia huduma zetu zinazoendana na mahitaji yao ikiwemo mikopo ya binafsi, kibiashara au hata ya umiliki wa nyumba  zenye riba nafuu kabisa. Tunawakaribisha sana Benki ya Exim,’’ alisema.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/19fb126c7c0de704b0fd5b6d248ae567.jpeg

SHIRIKISHO la Wafanyabiashara na wenye viwanda nchini ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi