loader
Dstv Habarileo  Mobile
NIMR: Chanjo ya corona salama 99.99%

NIMR: Chanjo ya corona salama 99.99%

TAASISI ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR), imesema ipo kwenye mchakato wa kutengeneza chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid- 19.

Aidha, NIMR ilisema jana kuwa chanjo zitakazotolewa nchini dhidi ya ugonjwa huo ni salama kwa asilimia 99.99 na zimethibitishwa na na jopo la wanasayansi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO).

Mkurugenzi Mkuu wa NIMR, Dk Yunus Mgaya alisema hayo jana wakati akijibu swali kama Tanzania ina mpango wa kutengeneza chanjo yake dhidi ya corona.

Dk Mgaya alikuwa akizungumza kwenye Kipindi cha Clouds 360 kilichorushwa na Kituo cha Televisheni cha Clouds kinachomilikiwa na Kampuni ya Clouds Media Group.

“Ndio Tanzania tunao mpango wa kuja na chanjo yetu ya corona. Rais Samia Suluhu Hassan alishasema na Katibu Mkuu akazungumzia hilo pia na sisi NIMR tukapewa jukumu,” alisema Dk Mgaya.

Alisema kutokana na maagizo hayo, tayari NIMR iko kwenye mchakato utakaoifikisha kwenye utafiti wa chanjo yake.

“Nasema Inshallah Mungu akipenda, tunaweza tukawa na chanjo yetu Tanzania ya ugonjwa huu na magonjwa mengine,” alisema Dk Mgaya.

Alisema Covid 19 ilivyoingia na kusambaa dunia nzima wanasayansi waliona hakuna namna ya kuudhibiti ugonjwa huo kwa kuwa hauna dawa hivyo mkazo uliwekwa kwenye chanjo.

Dk Mgaya alisema na hadi jana kulikuwa na chanjo zaidi ya 200 duniani zilizokuwa kwenye majaribio, lakini zilizopitishwa na WHO zitumike chini ya mpango wa dharura ziko sita.

Alitaja chanjo hizo kuwa ni nne kutoka Marekani ambazo ni BioNTech, Pfizer, Johnson & Johnson na Moderna NIAID, Novavax ya Uingereza, AstraZeneca ya Sweden na China ziko mbili; Sinovac-CoronaVac na Sinopharm.

Aidha, alisema chanjo ya Urusi ya Sputnik V ambayo pamoja na kwamba imeshaanza kutumika kwenye nchi nyingi duniani, bado inafanyiwa tathmini na WHO huku Cuba ikitengeneza chanjo inayoitwa Abdala.

Alisema chanjo hupitishwa zitumike baada utafiti na mamlaka mbalimbali kujiridhisha ziko salama kwa matumizi.

“Mfano chanjo inatengenezwa Marekani ni lazima ipitiwe na udhibiti wa mamlaka za Marekani pia lazima WHO iidhinishe. WHO ina kamati zake za kitaalamu zinazokagua mpaka kujiridhisha kitaalamu na kubwa zaidi huangalia usalama na ufanisi,” alisema mtendaji huyo wa NIMR.

Alisema chanjo sita zilizopitishwa na WHO zimefaa, haziwezi kumdhuru mtu kwamba akinywa atakufa au kuugua na kwamba kiwango cha athari ni kidogo mno kinachofikia asilimia 0.00004.

Dk Mgaya alisema manufaa ya chanjo za corona ni pamoja na kupunguza vifo, kuzuia watu kulazwa hospitalini, kupunguza makali ya ugonjwa na maambukizi.

Alisema kwa sasa dunia ina jumla ya watu bilioni 7.4, lakini waliochanjwa ni bilioni 1.5 sawa na asilimia 20 hadi 25 jambo linaloashiria kwamba bado kuna kazi kubwa ya kudhibiti ugonjwa wa Covid-19.

Alisema chanjo zinazotolewa zimehakikiwa na kupitiwa na watalaamu na kuthibitishwa kwa ushahidi wa kitaalamu.

“Nikisema Panadol inapunguza au inaponya maumivu si majaribio au kubahatisha imethibitishwa. Kwenye chanjo pia, ukweli unabaki wa kisayansi kabisa kwamba ziko salama kwa asilimia kubwa,” alisema.

Alisema chanjo Pfizer imeshatumika kwenye nchi 91, Moderna 54, Johnson ambayo imeingizwa Tanzania nchi 53, Sinopharm 56, AstraZeneca nchi 117, Sinovac 33 na Sputnik V nchi 69.

“Chanjo zote au dawa zote zina athari kidogo ila kinachoangaliwa ni faida inayopatikana ikilinganishwa na athari hasi. Athari ya Johnson kwa baadhi ya watu hupata damu kuganda, idadi ilikuwa kwenye milioni moja watu wanne tu sawa na asilimia 0.00004,” alisema Dk Mgaya.

Aliongeza, “Ukiambiwa asilimia ya watu wanaodhurika na Panadol asilimia inaweza kuwa kubwa kuliko hiyo chanjo. Nchi zinazotumia Johnson ni Marekani, Canada, Norway iliyoikataa na sasa imerejea kutumia pamoja na Denmark.”

Kuhusu hoja kwamba chanjo hizo si salama kwa kuwa zimetengenezwa kwa muda mfupi, alisema utaratibu wa kawaida wa kutumia teknolojia ya zamani kutengeneza chanjo ilikuwa inatumia mpaka miaka 20, lakini kwa teknolojia ya sasa ndani chanjo zinatengenezwa ndani ya mwaka.

“Kirusi kilipogundulika China, watu waliingia maabara na kusoma vinasaba vyake vyote kwa teknolojia ya sasa hiyo ni kazi ya saa mbili tu tofauti na zamani. Na hata teknolojia iliyotumika kutengenezea Pfizer au Johnson zimeshatumika kutengenezea chanjo nyingine ambazo nazo zimetumika vya kutosha na machapisho yapo ya kujiridhisha,” alifafanua.

Alisema katika kufanyia majaribio chanjo ya Pfizer na Johnson zimetumia zaidi ya watu 43,000 na kuthibitisha usalama wake.

Akielezea kuhusu ulazima wa kujaza fomu kabla ya chanjo, Dk Mgaya alisema alisema jambo hilo ni la kawaida katika taaluma ya tiba.

“Leo hii ukienda kufanyiwa operesheni ndugu zako wanajazishwa fomu kama ile. Hata tunapoenda kufanya utafiti kwenye jamii tunakuwa na fomu. Hii ni kitu cha kawaida katika taaluma ya tiba,” alibainisha.

 

foto
Mwandishi: Halima Mlacha

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi