loader
Dstv Habarileo  Mobile
Hifadhi ya mikoko, ikolojia tegemeo kwa ustawi wa dunia

Hifadhi ya mikoko, ikolojia tegemeo kwa ustawi wa dunia

HIFADHI za mikoko ni ikolojia muhimu katika ustawi wa dunia, takwimu zinaonesha kuwa dunia ina takribani mikoko inayochukua asilimia moja tu ya misitu yote katika Kanda za Tropic.
Asilimia moja hiyo inatoa mchango mkubwa sana katika ustawi wa jamii za Pwani na lakini katika ustahimilivu wa mazingira kwa ujumla.
Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo anasema kwa bahati mbaya sana mikoko inatoweka duniani kwa kasi kubwa.
Kidunia takwimu zinaonesha kuwa asilimia moja inatoweka kila mwaka.
Profesa Silayo anasema mikoko inapatikana katika nchi 108 duniani na nchi yenye mikoko mingi duniani ni Indonesia kwa upande wa Afrika ni Nigeria.
Tanzania inachukua nafasi ya tisa ikiwa na mikoko yenye jumla ya hekta laki moja na nusu inayopatikana kwenye maeneo mbalimbali inayochukua mwambao wa Pwani kuanzia Wilaya ya Nkinga mkoani Tanga mpaka Mtwara.
Profesa Silayo anasema sehemu kubwa yenye mikoko ni kwenye maeneo yanayoingiliana maji baridi na chumvi. Tanzania kuna aina tisa za mikoko.
Anasema kutokana na umuhimu wa mikoko jitihada mbalimbali zimekuwa zikifanyika kuhakikisha mazao ya misitu yanahifadhiwa ikiwepo sheria inayohifadhi mikoko kutokana na uharibifu,
Pia serikali imekuwa ikiongeza vifaa vya kufanyia kazi ikiwemo boti ya kufanya doria katika maji mafupi na kina cha bahari, vifaa vingine vya doria ni pikipiki, magari lakini pia wanashirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kama Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Jeshi la Polisi.
Kila Julai 26 ni maadhimisho ya siku ya mikoko duniani hivyo anatoa wito kwa jamii kuitunza mikoko badala ya kukaushia samaki ama kwa ajili ya biashara bali wafanye shughuli nyingine za kiuchumi ikiwemo kilimo cha samaki ambacho kwa kushirikiana na wizara ya mifugo wanaisaidia jamii.

Anaiasa jamii kutochafua bahari kwa takataka ngumu au takataka sumu za maji kwani kwa kufanya hivyo husababisha mizizi ya mikoko kufa.
“Mfano unaposikia meli imemwaga mafuta baharini au kisima cha mafuta kimeharibika na kuvuja baharini yote hayo husababisha viumbe kutoweka,” anasema na kueleza kuwa, TFS wanapambana kuzuia uharibifu wa bahari ili mikoko isipotee.
Anasema hifadhi hiyo ya mikoko ni kubwa kuliko zote katika Ukanda wa Afrika Mashariki, ambapo ina hekta 53,255 nusu ya mikoko yote Tanzania ambapo mikoko yote nchini ina hekta 115,000.
Mhifadhi Misitu Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani kutoka TFS, Mathew Ntilicha anaelezea faida mbalimbali za mikoko zinazoonekana na zisizoonekana ambazo ni za kimazingira, kiikolojia, kiuchumi na kijamii.
Anasema kiuchumi nguzo za mikoko hutumika kwa ajili ya nguzo na mbao kwa ajili ya ujenzi wa nyumba, mashua na samani mbalimbali. Vile vile kuni, dawa za kutibu magonjwa mbalimbali mfano ya ngiri ambayo hutibiwa kwa kutumia mikoko jamii ya mkomafi.
Vile vile majani yake hutumika kwa ajili ya chakula cha mifugo, maganda yake kutengenezea rangi za ngozi, pia kwenye maeneo yenye mikoko hutumika kwa ufugaji wa kaa kwa kutumia masanduku na ndoo.
Si hivyo tu faida nyingine mikoko hutumika kutengenezea mkaa wa biashara kwa uangalizi maalumu wa kitaalamu.
Lakini pia mikoko ina faida kiikolojia kwa kuwa ni mazalia ya samaki wa aina mbalimbali wakiwemo kamba, kaa na wengineo, delta ya Rufiji iliyoko Mkoa wa Pwani inatoa asilimia 80 ya samaki aina ya Kamba kwa Tanzania.
Pia hulinda samaki wadogo dhidi ya maadui na hutoa kivuli kwa viumbe waishio maeneo hayo, vile vile ni makazi ya viumbe mbalimbali kama ngedere, kima, ndege, nyoka, viboko, mamba na nguruwe.
Faida za kimazingira za mikoko huzuia mmomonyoko wa kingo za mito na bahari dhidi ya upepo mkali na mawimbi baharini, huchuja udongo usiende baharini hivyo kulinda matumbawe na majani baharini.
“Mikoko huchuja sumu zilizoko kwenye maji na mito zisiingie baharini, hunyonya hewa ukaa na kusaidia kupunguza joto duniani, mikoko ni maeneo mazuri kwa ufugaji nyuki pia kwa ajili ya utalii, utafiti na mafunzo, utalii wa aina hii umeendelezwa sana kwenye nchi za mashariki ya mbali kama Japan na Malasia,” anasema.
Ntilicha anasema Misitu ya Hifadhi ya Mikoko Delta ya Rufiji ina mfumo ikolojia wenye miti inayoota kando kando ya bahari au kwenye maingilio ya mito mikubwa baharini.
Anasema hustawi kwenye maji ya chumvi, pia imeonekana kustawi zaidi katika mchanganyiko wa maji baridi na maji chumvi.
“Hifadhi hii ya mikoko ni kubwa kuliko zote katika Ukanda wa Afrika Mashariki ambapo ina hekta 53,255 ikiwa ni nusu ya mikoko yote Tanzania. Mikoko yote Tanzania ina hekta 115,000,” anasema.
Anaeleza kuwa eneo hilo hupokea asilimia 20 ya maji yote Tanzania yanayoingia delta na rutuba nyingi, udongo, mchanga na kemikali mbalimbali.
Kwa asili yake mikoko ina uwezo wa kufyonza kemikali zote na kuruhusu kuingizwa kwa maji safi baharini, endapo maji yenye sumu, udongo na mchanga ungeingia baharini ungeua viumbe wengi na kuharibu matumbawe na majani bahari ambayo ni mazalia na malisho ya samaki hivyo kuathiri ikolojia ya delta, bahari na kuathiri uchumi wa taifa.
Anaeleza kuwa makutano ya maji chumvi na maji baridi ya Mto Rufiji na mazingira ya mikoko huhifadhi chakula cha kutosha kwa viumbe mbalimbali wa bahari wakiwemo Kamba.
“Delta ya Rufiji hutoa asilimia 80 ya Kamba wote wanaozalishwa Tanzania na kuifanya delta kuwa sehemu muhimu kwa uchumi wa taifa na wa mtu mmoja mmoja.
“Delta ya Rufiji huifadhi miti ya mikoko ya aina nane kati ya tisa zinazopatikana Tanzania. Ina wanyama kama mamba, viboko, samaki wa aina mbalimbali na ndege wanaohama,” anasema.
Uwepo wa mazingira ya delta yenye wanyama na mimea hutoa fursa ya utalii wa kiikolojia. Kimataifa, mazingira ya bahari na misitu ya mikoko inatambulika kuhifadhi hewa ya ukaa nyingi kuliko ikolojia nyingine yoyote, hivyo kuchangia kwa kiasi kikubwa kupunguza athari za mabadiliko ya tabia nchi.
“Kutokana na sifa zote hizi Jumuiya ya Kimataifa imelitambua eneo hili la delta kuwa chepechepe lenye hadhi ya kimataifa,”anasema.
Kutokana na ongezeko kubwa la watu katika eneo hilo kumesababisha kuwepo kwa shughuli mbalmbali za kijamii ambazo zimekuwa si rafiki katika uhifadhi.
Shughuli kubwa inayofanyika katika eneo hilo ni kilimo cha mpunga kwani utafiti uliofanyika mwaka 2011 na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam eneo la kilimo hicho ndani ya delta ya 1995 ilikuwa ni hekta 3,015, mwaka 2000 hekta 3700 na mwaka 2011 eneo liliongezeka hadi kufikia hekta 8700.
“Kufikia sasa kuna uwezekano wa hekta zaidi ya 15,000 zitakuwa zimeharibiwa kutokana na kilimo cha mpunga,” anasema.
Anaeleza athari za kilimo hicho kuwa ni uharibifu wa mfumo mzima wa ikolojia ya bahari ya Pwani ikiwa ni pamoja na kupungua kwa miti ya mikoko, samaki na viumbe wengine baharini kutokana na ukataji mkubwa wa miti.
Pia mmomonyoko wa ardhi na kuporomoka kwa kingo za mito huchangia kuziba kwa mto, kupungua kwa kina chamaji mitoni na baharini na kuua viumbe wa baharini kama matumbawe na majani baharini.
Hivi karibuni katika ziara yake kwenye delta hiyo, Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mary Masanja alisema serikali inaandaa miongozo ya namna ya kuvuna mikoko iliyoko kwenye maeneo ya delta ambayo inakaribia kukamilika mwishoni mwa mwezi huu na kuwataka wananchi waendelee kuwa na subira.
Masanja alisema serikali imeandaa miongozo hiyo kwa kuwa eneo hilo la delta ni zuri lina mazalia mbalimbali ya samaki wakiwemo aina ya kamba ikiwa ni pamoja na kuepusha ukataji ovyo wa miti.
“Kipindi ambacho tutakuwa tumeruhusu uvunaji ina maana wananchi watapata faida kubwa ikiwemo uvunaji wa mazao ya misitu hususan kuvuna miti lakini wavuvi watanufaika na uvunaji wa samaki aina ya kamba,
“Eneo hili lina nusu ya mikoko yote inayohifadhiwa Tanzania wananchi waendelee kuhifadhi,  ni hifadhi endelevu watu wa maliasili tuna kauli mbiu inayosema ‘Tumerithishwa, Tuwarithishe. Sisi tumerithishwa na mababu zetu tumeendelea kuhifadhi maeneo haya ili na vizazi vijavyo viendelee kurithi,” alisema.
Naye Mkuu wa Wilaya ya Kibiti mkoani Pwani, Ahmed Abbas alisema ili kuhifadhi eneo hilo wamekuwa wakitoa elimu kwa wananchi ikiwemo kilimo bora kisichoathiri eneo hilo la delta.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/69fed2f7aab11e90f6066da8f5abf1ec.jpg

OFISI ya Taifa ya Ukaguzi (NAOT) ni Taasisi ...

foto
Mwandishi: Lucy Ngowi

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi