loader
Wagogo na utamaduni wa kujivunia

Wagogo na utamaduni wa kujivunia

LEO katika mwendelezo wa makala za utamaduni, mila na desturi za makabila mbalimbali ya Tanzania, tunaangazia jamii ya Wagogo wanaopatikana katika Mkoa wa Dodoma.

Kwa mujibu wa tovuti ya Halmashauri ya Jiji la Dodoma, mji ambao sasa unaitwa Dodoma ulikuwa ukifahamika kama Chalangu (Calangu).

Mji huu haukuwa na wenyeji bali ulikuwa na wahamiaji toka maeneo mengine ambao ni Wamanghala, Wabambali, Wayenzele na Wanghulimba.

Wahamiaji hawa walikuwa wakitofautiana kwa tabia zao, Wamanghala na Wabambali waliishi msituni na walikuwa wawindaji wakila nyama na asali. Wayenzele na Wanghulimba walikuwa wakulima na wafugaji.

Watu hawa walikuwa waoga kiasili hivyo watu wengine walipoanza kuingia kutoka maeneo ya Kaskazini (Wambugwe), Magharibi (Wanyamwezi) na Kusini (Wahehe) watu hawa waliondoka na kwenda kuishi sehemu nyingine.

Sababu ya wahamiaji hawa kuitwa Wagogo inatokana na wafanyabiashara wa Kinyamwezi walipokuwa wakipita na bidhaa zao kuelekea Pwani, walipofika kati ya Itigi na Manyoni walikuta mti mkubwa umeanguka na kuzuia njia (gogo), hivyo kwa muda mrefu walilazimika kulala upande mmoja kabla ya kuvukia upande wa pili wa mti.

Hii iliwafanya kila walipoulizwa wanalala wapi kabla ya kuendelea na safari walisema wanalala kwenye limgogo. Kwa hiyo wahamiaji hawa wakafahamika kama gogo (Wagogo) kutokana na gogo hilo.

Mnamo mwaka 1912 Mjerumani Dk Spreling (Spelenje) alifika hapo na kuanzisha ngome yake, ngome hiyo kwa sasa ni Ofisi ya Waziri Mkuu.

Ofisi aliyokuwa akifanyia kazi za utawala na utoaji uamuzi kwa wahalifu (kufungwa, kuchapwa viboko na kunyongwa) kwa sasa ni Ofisi ya CCM Wilaya ya Dodoma Mjini.

Bustani aliyopenda kutembelea na kupumzika ilikuwa eneo la Kikuyu ambayo kwa sasa ni Chuo Kikuu cha St. John’s, eneo hili kwa wakati huo lilikuwa tepetepe na mapitio ya wanyama watokao mbuga za Kaskazini (Arusha) kuelekea mbuga za Kusini (Mikumi).

Mapitio ya wanyama hao ndiyo yaliyosababisha kubadilika kwa jina la eneo hili baada ya tembo kudidimia katika eneo hilo tepetepe ambalo sasa ni Chuo Kikuu cha St. John’s.

Tendo hili la kudidimia kwa lugha ya Kigogo linajulikana kama Idodomia, hivyo baada ya kitendo hiki jina likabadilika kutoka Chalangu na kuwa Idodomia (Dodoma).

Lugha ya Wagogo ni Cigogo (Kigogo), na dini ya wengi wao ni Ukristo hasa wa madhehebu ya Anglikana, halafu wa Kanisa Katoliki.

Lafudhi ya lugha

Kabila la Wagogo lina lahaja ndani yake ambazo hutofautiana kutoka moja hadi nyingine kwa jinsi ambavyo hutamka maneno, yaani huongeza na kupunguza baadhi ya matamshi kwenye neno, na pia katika msamiati.

Kwa ujumla kuna lahaja zipatazo nne (4), ambapo lahaja za Cinyambwa (Kinyambwa) na Cinyaugogo (Kinyaugogo) ndizo hujulikana zaidi.

1. Wanyambwa: hili ni kundi linaloonekana wazi kwenye kabila hili ambao huongea lafudhi ya Kinyambwa. Wanyambwa hutokea vijiji vya Magharibi kwa Mji wa Dodoma na sehemu ya Wilaya ya Manyoni mkoani Singida.

2. Wanyaugogo: hawa huongea lafudhi iitwayo Chinyaugogo. Wanyaugogo ambao ndio wanaowakilisha kundi kubwa sana hutokea vijiji vya Mashariki na Kusini kwa Mji wa Dodoma na pia Wilaya ya Mpwapwa.

Kwa sababu Mtemi Mazengo alikuwa Mnyaugogo kutoka Mvumi, mahali ambapo palijengwa kijiji kinachoitwa Mvumi Makulu (kwa maana kwamba ndipo ilipokuwepo Ikulu ya Mtemi), inaaminika kuwa lafudhi hii ndicho Kigogo cha asili isiyoathiriwa na lugha za nje.

3. Wetumba: hawa ni Wagogo walioathiriwa Kigogo chao na lugha ya Kikaguru. Hupatikana katika Wilaya za Kongwa na Mpwapwa.

4. Wetiliko: hawa ni Wagogo wenye asili au mchanganyiko na Wahehe pamoja na Wabena, na hupatikana maeneo ya Kibakwe wilayani Mpwapwa.

Utawala wa jadi

Kabla ya ukoloni kuja nchini Wagogo walikuwa wakiongozwa na mtu aliyeitwa Mtemi. Watemi kadhaa waliongoza kabila hilo kabla ya mfumo wa uongozi kuvurugwa na ukoloni. Mtemi wa mwisho aliitwa Mazengo ambaye alitokea katika eneo la Mvumi.

Kabila hili linatumia silaha za jadi kwa kujilinda kama vile upinde, mshale, mkuki na hengo.

Hata hivyo kabila hili lina utamaduni wa kujivunia nchini, Afrika na duniani kote, moja ya michezo ya asili katika kabila hili ni ngoma ambazo ni michezo ya kitamaduni zaidi katika makabila mengi Tanzania.

Ngoma hizi ni sehemu ya utamaduni wa Wagogo lakini pia katika nchi hii ni sehemu ya kujivunia kwa kuwa inasaidia kukuza na kueneza utamaduni wa Mwafrika kupitia maonesho mbalimbali ya utamaduni nchini na kimataifa kama vile maonesho katika Makumbusho ya Taifa.

Muziki wa asili wa Wagogo umepata sifa ya kimataifa. Na aliyesaidia sana kuufanya muziki wao ujulikane ni marehemu Dk Hukwe Zawose.

Zawose alikuwa msanii mahiri na maarufu duniani ijapokuwa hakufahamika sana nchini kwake Tanzania. Hata hivyo aliitangaza sana Tanzania duniani.

Zawose alivutia sana kwa kupiga zeze kubwa sana lenye hadi nyuzi 14 katika kikundi chake cha Chibite, ukijumlisha na sauti zinazohanikiza za marimba huku zikiitikiwa na milio ya ngoma zilizopigwa kwa ustadi, vyote hivyo vikikolezwa kwa sauti yake ambayo mara nyingi aliimba kwa lugha ya Kigogo.

Nyumba za asili

Wagogo wamekuwa wakijenga nyumba ambazo kwa Kigogo huitwa “itembe”. Tangu zamani kuta za tembe zilijengwa kwa fito (kwa Kigogo hutamkwa sito) zilizosukwa kwa kupishana kuzuia mwanga na maji. Vipande vya kuta vilivyosukwa kwa fito vinaitwa “izizi”.

Tembe huezekwa kwa udongo ambao hushikiliwa na miti midogomidogo iitwayo “walo”. Walo huwa inashikiliwa na miti mikubwa kidogo iitwayo “mahapa” na mahapa hushikiliwa na miti mikubwa iitwayo “michichi”.

Michichi ambayo ndiyo hubeba uzito wote hushikiliwa na nguzo kubwa za miti imara na migumu. Nguzo hizo hutiwa “masumbilili”.

Kwa miaka ya karibuni kuta za tembe hujengwa pia kwa matofali yanayotengenezwa kwa udongo.

Shughuli za kiuchumi

Historia na maendeleo ya Wagogo viliathiriwa sana na ukame na biashara ya utumwa, kiasi kwamba hata leo ni kati ya makabila fukara zaidi nchini Tanzania.

Hata hivyo, Wagogo ni miongoni mwa makabila ya wakulima na wafugaji kwa asili na hufuga mifugo kama ng’ombe, mbuzi (mhene) na kondoo (ngholo) pamoja na punda (ndogowe) kwa ajili ya ubebaji mizigo na wakati mwingine kulimia wakitumika kukokota majembe ya kukokotwa, kama watumikavyo ng’ombe pia.

Sambamba na shughuli hiyo, kilimo ndiyo shughuli kubwa na ya wengi, ijapokuwa mkoa wa Dodoma kwa miaka mingi umekuwa ukiathiriwa na kiwango kidogo cha mvua zinazonyesha kutokana na jiografia ya eneo la katikati ya Tanzania katika mikoa miwili ya Dodoma na Singida.

Kilimo na ufugaji huwasaidia katika chakula. Mazao ambayo hulimwa zaidi na wagogo ni mazao ya chakula kama vile mtama, mahindi, karanga, njugu mawe, lakini pia mazao ya biashara ni kama vile zabibu, ufuta na alizeti ambazo husaidia katika kuingiza kipato. 

Chakula kikuu

Wagogo hula ugali wa uwele na mtama kama chakula chao kikuu, lakini pia hula ugali wa mahindi ingawa huchukulia ugali wa mahindi kama chakula laini na chepesi kisicho na nguvu.

Miaka ya zamani mlo wa kawaida wa Mgogo mwenye uwezo (yaani mwenye ng’ombe) ulihusisha ugali, maziwa, mafuta ya ng'ombe (samuli) na mboga kama mlenda (ilende), majani ya kunde (safwe), cidingulilu, nyakifwega, muhilile, sanghala, munzimwa, cipali, ihaji, sagulasagula, ikuwi, fwene, nghalabwajila (hasa wakati masika inapoanza) n.k.

Kwa sasa Wagogo wamekuwa wakila chakula cha kawaida kama makabila mengine nchini Tanzania.

Makala haya yametokana na vyanzo mbalimbali vya habari.

0685 666964 au bhiluka@gmail.com

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/06150f1f3585f394891c491edc1bf923.jpg

SERIKALI kupitia Shirika ...

foto
Mwandishi: Bishop Hiluka

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi