loader
Dstv Habarileo  Mobile
Yanga yasaka taji Kagame

Yanga yasaka taji Kagame

YANGA leo itaikabili Nyasa Big Bullets, katika michuano ya Kombe la Kagame ambayo inaanza kutimua vumbi Uwanja wa Benjamin Mkapa Dar es Salaam.

Katika mchezo huo wa ufunguzi ambao utaanza saa 10:00 jioni wenyeji Yanga wenye rekodi ya kutwaa taji hilo mara tano wanapewa nafasi kubwa ya kufanya vizuri licha ya kuwakosa baadhi ya nyota wake tegemeo wa kikosi cha kwanza.

Kukosekana kwa nyota hao kunatoa nafasi kwa wachezaji wengine wa kikosi hicho Wazir Junior, Paul Godfrey, Yassin Mustafa, Tonombe Mukoko, Ramadhani Kabwili, Zawadi Mauya na Balama Mapinduzi aliyekuwa majeruhi kuonesha ubora wao.

Wengine ni mabeki wa kati Dickson Job, Adeyum Salehe, Abdallah Shaibu ‘Ninja na wachezaji wawili wapya waliosajiliwa kwa ajili msimu ujao ambao ni Dickson Ambundo kutoka Dodoma Jiji, beki David Bryson wa KMC na kipa mpya Erick Johara aliyesajiliwa kutoka timu ya Aigle Noir ya Burundi Kocha wa Yanga, Razak Siwa atakuwa na kazi ya kuipa taji la sita na kuunganisha wachezaji kucheza kitimu kutokana na mchanganyiko wa wachezaji kutoka timu ya wakubwa, kikosi cha vijana chini ya umri wa miaka 20 na baadhi wapya.

Mchezo huo wa Kundi A unatarajiwa kuwa mgumu na wenye ushindani kwa sababu Yanga iliyomaliza nafasi ya pili kwenye Ligi Kuu na Kombe la FA, itataka kuonesha wao ni timu bora lakini wapinzani wao Nyasa walishika nafasi ya pili kwenye ligi ya Malawi wakizidiwa kwa pointi moja na vinara Silver Strikers.

Yanga wanatakiwa kucheza kwa umakini wa hali ya juu ili kuhakikisha wanaanza vyema michuano hiyo vinginevyo wanaweza kujikuta wakitoka vichwa chini. Kabla ya mchezo wa Yanga na Nyasa Bullets, mapema The Express SC ya Uganda itapambana na miamba ya Sudan, Atlabara FC mchezo ambao unatarajiwa kuanza saa 7:00 mchana kwenye uwanja huo wa Mkapa.

Mechi nyingine za Kundi B lenye timu za Le Messeger de Ngozi ya Burundi na KMKM zitachezwa kesho na mchezo wa funga kazi ni kati ya mabingwa watetezi KCCA ya Uganda dhidi ya Azam FC.

Jumla ya timu nane kutoka mataifa ya Burundi, Sudan, Uganda, Zanzibar na wenyeji Tanzania zinashiriki michuano hiyo ya 43 kwa ngazi za klabu ambayo inaandaliwa na Baraza la Vyama vya Soka kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati (Cecafa).

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/8bab137a9f10c49e3040589d1e3c3565.jpg

BAADA ya Yanga kuondolewa kwenye michuano ya Ligi ...

foto
Mwandishi: Mohamed Akida

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi