loader
Dstv Habarileo  Mobile
Karia amzawadia Samia kombe

Karia amzawadia Samia kombe

RAIS wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Wallace Karia amemzawadia Rais Samia Suluhu Hassan, ubingwa wa Kombe la Cecafa kwa timu ya vijana wenye umri chini ya miaka 23 iliyoifunga Burundi kwa penalti 6-5 katika mchezo uliochezwa Ethiopia juzi.

Huo ni ubingwa wa kwanza kwa timu hiyo na wa kwanza kwa timu za soka za taifa za wanaume kutwaa tangu Rais Samia awe madarakani. Akizungumza baada ya timu hiyo kukabidhiwa ubingwa, Rais Karia aliwapongeza wachezaji pamoja na benchi la ufundi kwa kazi kubwa waliyofanya hadi kutwaa taji hilo ambalo limeongeza heshima katika soka la vijana kwa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Niwapongeze wachezaji pamoja na benchi la ufundi lakini niseme ubingwa huu namzawadia Rais wetu Samia, najua leo (juzi) anapokea ndege lakini na kombe hili liwe sehemu ya furaha kwake katika jitihada zake za kusapoti michezo nchini,” alisema Karia.

Karia alisema ubingwa huo una maana kubwa kwake kama kiongozi lakini kubwa zaidi ni kuongeza bidii na kuwekeza kwenye soka la vijana ili Tanzania iweze kufanya vizuri kwenye michuano ya kimataifa siku zijazo.

Alisema baada ya kumalizika kwa michuano hiyo wataweka misingi mizuri ambayo itawalinda wachezaji hao na kuwajengea utaratibu mzuri ili wawe wachezaji tegemezi kwenye kikosi cha timu ya wakubwa ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.

Karia alisema anatambua soka la vijana linapewa kipaumbele hivi sasa hivyo naye kwa kushirikiana na wenzake watajitaidi kuanzisha mashindano mengi ya vijana ili kutengeneza vipaji vingi kwa faida ya baadaye.

Aidha alisema kuanzisha kwa mashindano ya U23 ni wazo lake alilitoa na kuungwa mkono na wajumbe wenzake hivyo anaona fahari Tanzania kutwaa ubingwa ikiwa ni mara ya pili kwa mashindano hayo kufanyika kwani awali Uganda ndio walichukua.

Naye nahodha wa timu hiyo Israel Patrick alisema wanashukuru kutwaa ubingwa kwani walikuwa hawana maandalizi lakini wamefanya vizuri.

“Tunashukuru kutwaa ubingwa huu, timu yetu haikuwa na maandalizi yoyote lakini tumefanya vizuri,” alisema Israel. Timu hiyo inatarajiwa kuwasili leo saa 12:30 asubuhi na ndege ya Shirika la Ethiopia.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/f631fe3745e05769d3e9a46877145358.jpeg

BAADA ya Yanga kuondolewa kwenye michuano ya Ligi ...

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi