loader
Dstv Habarileo  Mobile
Tanzania mwenyeji Maonesho ya Utalii EAC

Tanzania mwenyeji Maonesho ya Utalii EAC

TANZANIA imechaguliwa kuwa mwenyeji wa maonesho ya kwanza ya kila mwaka ya utalii Afrika Mashariki (EARTE), yatakayofanyika Oktoba, mwaka huu kwa lengo la kuboresha na kutangaza utalii wa ukanda huo kama eneo moja la utalii.

Uamuzi huo umefanywa na Baraza la Mawaziri wa Afrika Mashariki katika sekta ya utalii na usimamizi wa wanyamapori katika kikao chao kilichopitisha mpango maalumu wa kukuza utalii wa EAC kwa lengo la kufufua sekta hiyo iliyoathirika na mlipuko wa janga la ugonjwa wa Covid-19.

Maonesho hayo yatakayofanyika kwa mara ya kwanza, ni moja ya mipango waliyokubaliana mawaziri hao kufufua sekta hiyo. Mawaziri hao waliokutana chini ya uenyekiti wa Katibu wa Baraza la Mawaziri la Utalii na Wanyamapori wa Kenya, Najib Balala, walikubaliana kuna haja ya kuwa na mipango ya pamoja katika kufufua sekta hiyo ili kusaidia utekelezaji mipango ya kila nchi ya kufufua sekta hiyo.

Waliidhinisha na kupitisha rasimu ya miongozo ya kikanda kuanza tena huduma za utalii katika ukanda huo wenye vivutio vingi. Walisema miongozo hiyo ya kikanda itasaidia kuhakikisha huduma kwa watalii zinarejea na kujenga imani na ujasiri kwa watalii wa kimataifa wanaotembelea ukanda huo na kuifanya EAC kuwa eneo bora na nafuu la utalii Afrika.

Katika kikao hicho, Baraza la Mawaziri la Kisekta lilikubaliana kuanzisha maonesho ya kila mwaka ya ukanda wa EAC kwa lengo la kuutangaza kama eneo moja la utalii kwa kuanza mwaka huu nchini Tanzania.

Katibu Mkuu wa EAC, Dk. Peter Mathuki alisema sekta ya utalii ni muhimu katika ushirikiano wa jumuiya hiyo kutokana na mchango wake katika uchumi na pato la ndani la nchi wanachama kwa takribani asilimia 10, huku mapato ya kuuza nje ya nchi ni asilimia 17 na kutoa ajira takribani asilimia saba.

Alisema kwa mujibu wa takwimu za EAC, ukanda huo ulipoteza takribani asilimia 70 ya watalii wa kimataifa mwaka jana na kushusha mapato yanayotokana na utalii pamoja na ajira na kwamba mwaka huu ishara bado ni mbaya kutokana na kuwapo kwa mlipuko wa wimbi la tatu la virusi vya corona.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi