loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kumekucha chanjo ya corona mikoani

Kumekucha chanjo ya corona mikoani

MAMLAKA za mikoa zinaendelea kupokea chanjo dhidi ya ugonjwa wa Covid-19 na kumalizia maandalizi ili kuanza kuitoa. Mkoani Dodoma, Mganga Mkuu Mkoa wa Dodoma, Best Magona alisema jana walipokea chanjo dozi 50,000 na vituo 28 viko tayari kwa kazi hiyo.

Alisema chanjo hizo zimegawiwa katika wilaya zote saba za Dodoma, Bahi, Chamwino, Kongwa, Mpwapwa, Chemba na Kondoa na kwamba, kila wilaya itakuwa na vituo vitatu isipokuwa Wilaya ya Dodoma itakayokuwa na vituo saba.

“Mpaka leo mchana (jana) watu 900 walikuwa wamejiandikisha; mwitikio ni mkubwa na mimi nitachanja, wananchi waende kwenye vituo vya afya kukiandikisha,” alisema Magona.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka alisema anatamani watu wabishi na wanaokubali kupotoshwa waende wodini kuona masaibu wanayokumbana nayo wagonjwa wa Covid-19.

“Natamani watu wachache twende nao wodini wajue hali inayoendelea, ukipata maambukizi hatuna kitanda cha kukuweka,” alisema Mtaka.

Aliongeza:”Mimi nilichanjwa mara ya kwanza Nairobi mwaka jana na tulikuwa viongozi mbalimbali na wengine walisafiri hadi Nairobi, Afrika Kusini na Dubai kwa ajili ya chanjo, lakini sasa chanjo imefika nchini…”

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Rashid Mfaume, alisema mkoa huo ulipokea chanjo 160,000 na kuna vituo 28. Dk Mfaume alisema muda wowote kuanzia jana wangekuwa wamesambaza chanjo hizo. Alisema hadi jana wananchi 10,000 walikuwa wamejiorodhesha kuomba kupata chanjo hiyo.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Dk Boniface Kasululu, alisema jana kuwa, mkoa huo umekamilisha maandalizi ya kupokea dozi 20,000 za chanjo itakayotolewa katika vituo 11.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ofisa Habari Mkuu katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Rukwa, Kasululu alisema hayo alipozungumza na waandishi wa habari wakati akikagua vituo vituo vya kutolea chanjo hiyo katika Manispaa ya Sumbawanga.

“Maandalizi ya mapokezi ya dozi 20,000 za Uviko-19 zilizotengwa kwa ajili ya watu wa Mkoa wa Rukwa yamekamilika na sasa tunasubiri uzinduzi rasmi wa kuchanja wote waliojisajili kwa hiari yao… Mkuu wa Mkoa, Joseph Mkirikiti atazindua kazi hiyo Jumatano wiki hii,” alisema.

Dk Kasululu alisema ili mwananchi apate chanjo atapaswa kujisali kwenye mfumo uliowekwa na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto kupitia tovuti yake au aende kwa moja kwenye kituo kitakachotumika kutoa chanjo hiyo.

Alitaja vituo vitakavyotumika kwa awamu ya kwanza katika Manispaa ya Sumbawanga kuwa ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa mjini Sumbawanga, Hospitali ya Dk Atiman na Kituo cha Afya Mazwi. Wilayani Nkasi chanjo itatolewa kwenye katika Hospitali ya Misheni Namanyele, Kituo cha Afya Nkomolo na katika Kituo cha Afya Kilando.

Katika Wilaya ya Kalambo, chanjo hiyo itatolewa katika vituo vya afya vya Matai na Mwimbi. Dk Kasululu alisema katika Halmashauri ya Wilaya ya Sumbawanga vituo vitakavyotumika ni vituo vya afya vya Laela, Mpui na Mtowisha na kwamba, chanjo itatolewa pia kwa wananchi wa wilaya za Nkasi na Kalambo. Mganga Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Nyembea Hamadi alisema jana walitarajia kupokea dozi 10,000 za chanjo ya Covid-19.

Hamadi alisema katika Halmashauri ya Mbozi chanjo itatolewa katika Hospitali ya Wilaya ya Vwawa na katika vituo vya afya vya Isansa na Iyula.

Alisema katika Halmashauri ya Ileje chanjo itatolewa katika Hospitali ya Wilaya ya Itumba, vituo cha afya vya Ibaba na Lubanda na katika Halmashauri ya Mji wa Tunduma ni katika Hospitali ya Mji wa Tunduma, Moraviani na Tunduma TCHC.

Halmashauri ya Wilaya ya Momba alivitaja vituo vya Kamsamba HC, Zahanati ya Chitete na Kituo cha Ndalambo na Halmashauri ya Songwe chanjo itatolewa katika Hospitali ya Wilaya ya Songwe, Mbuyuni na Kapalala.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Thomas Rutachuzibwa alisema jana kuwa, wamepokea dozi 90,000 za chanjo ya Covidi- 19 na kuna vituo 27. Alisema kila halmashauri itakuwa na vituo vitatu.

“Kwa halmashauri za hapa mjini Ilemela na Jiji la Mwanza tutakuwa na vituo vingi ili viweze kuhudumia idadi ya watu waliopo na timu za watalaamu watakaotoa chanjo hiyo ziko kwenye maandalizi,” alisema Dk Rutachuzibwa.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Gunini Kamba, alisema wamepokea dozi 30,000 za chanjo na itatolewa katika vituo 27. Dk Kamba alisema wananchi zaidi ya 470,000 mkoani humo wanatarajiwa kupatiwa chanjo hiyo.

  • Imeandikwa na Baraka Messa (Songwe), Lucy Lyatuu (Dar es Salaam), John Gagarini (Kibaha), Nashon Keneddy (Mwanza), Sifa Lubasi (Dodoma) na Mwandishi Wetu, (Rukwa).
foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi