loader
Ma-DED mlioteuliwa msimwangushe Rais

Ma-DED mlioteuliwa msimwangushe Rais

JANA Rais Samia Suluhu Hassan alifanya uteuzi wa Wakurugenzi Watendaji wa Halmashauri za Jiji, Manispaa, Miji na Wilaya kwa kuteuwa wapya, kuhamisha vituo baadhi yao na kujaza nafasi 10 zilizokuwa wazi.

Kwa mujibu wa Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu, Rais ameteua wakurugenzi 184, kati yao 72 ni wapya, waliohamishwa ni 67 na waliobaki kwenye nafasi zao za awali ni 42.

Uteuzi huo wa Ma-DED na nyingine alizozifanya Rais Samia huko nyuma katika nafasi mbalimbali kama wakuu wa wilaya, wakuu wa mikoa na wakuu wa baadhi ya taasisi za umma, ni hatua ambazo amekuwa akizichukua katika kuimarisha serikali yake kuwahudumia wananchi tangu alipoapishwa kuwa Rais Machi 19, mwaka huu.

Rais Samia mara kwa mara amekuwa akisisitiza katika hafla za kuwaapisha viongozi aliwateuwa kuwa, teuzi hizo si zawadi au kufanyia mbwembwe bali ni kwa ajili kumsaidia kutatua changamoto za wananchi, pamoja na kuendeleza miradi ya maendeleo na kukuza uchumi wa nchi.

Hivyo, rai yetu kwa walioteuliwa kushika nyadhifa hizo ni kuhakikisha wanakwenda kuwatumikia wananchi kwa moyo wa dhati, kujituma, ubunifu na uadilifu ili kutomwangusha Rais Samia katika dhamira yake safi ya kuwatumikia wananchi ili wawe na maisha bora.

Wateule hao watambue Rais Samia ameonesha imani kubwa kwao, hivyo wanapaswa kumuonesha kuwa hajakosea katika kuwateua kwa kuchapa kazi usiku na mchana kuwahudumia wananchi ipasavyo.

Wakiwa katika maeneo yao ya kazi wanatakiwa kusimamia vizuri sera za kiuchumi ili kuboresha maisha ya watu, pamoja na kuweka mazingira mazuri ya kuvutia wawekezaji.

Pia wanatakiwa kuwa na usimamizi mzuri wa rasilimali za nchi, ukusanyaji mapato mengi na udhibiti wa matumizi yake, kudhibiti rushwa na ufisadi, kusimamia ustawi wa jamii bila ya matabaka, ujenzi wa miradi ya maendeleo, uwezeshaji wananchi na kuhimiza uchapaji kazi.

Usimamizi mzuri wa mapato ya serikali, uendelelezaji wa miundombinu na uwekezaji katika maeneo yao utatoa fursa zaidi kwa raia kuwa na fursa nyingi za kujipatia vipato zaidi hivyo kuboresha maisha yao.

Waende wakawahimize wananchi kuongeza juhudi ya kuchapa kazi kwa bidii na maarifa, pamoja na kubuni shughuli mbalimbali za kiuchumi na maendeleo bila kusubiri fursa chache za kuajiriwa ili maendeleo yaweze kugusa maisha ya mtu mmoja mmoja kwani kila mmoja atakuwa na shughuli ya kujiingizia kipato hivyo kuboresha uchumi wake na wa taifa.

Tunawasihi wateule hao wasiende kubweteka katika maeneo yao ya kazi kwa kudhani nafasi walizopewa ni kwa ajili ya ‘kula bata’, bali wajikite katika kushughulikia maendeleo na kuondoa shida za wananchi ili Watanzania wafurahie nchi yao chini ya Jemadari Rais Samia.

foto
Mwandishi: MHARIRI

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi