loader
Dstv Habarileo  Mobile
NEC : Jimbo la Konde liko wazi

NEC : Jimbo la Konde liko wazi

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imetangaza Jimbo la Konde visiwani Zanzibar, liko wazi baada ya mbunge wake mteule kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Sheha Mpemba Faki, kujiuzulu kwa sababu za kifamilia.

Taarifa ya Mkurugenzi wa Uchaguzi NEC, Dk. Wilson Mahera, imekuja  baada ya Faki kujuzulu nafasi hiyo.

Mahera amesema  NEC imeamua kutangaza jimbo hilo kuwa wazi, baada ya kupokea taarifa kutoka kwa Katibu Mkuu wa CCM, Daniel Chongolo, juu ya uamuzi wa mwanachama wake kujiuzulu ubunge.

“NEC imepokea barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa CCM yenye Kumb. Na. CCM/T.40/8vol.1/72, Agosti  2, 2021, ikitoa taarifa kuwa Mbunge mteule wa Konde, Faki aliandika barua kwa chama hicho kukitaarifu kuwa hayupo tayari kuwawakilisha wananchi wa Konde katika Bunge , kutokana na changamoto za kifamilia,” imesema taarifa ya Dk. Mahera.

 “Kutokana na hatua hiyo, tume inatoa taarifa kwa umma kuwa Jimbo la Konde lipo wazi na taratibu za kujaza nafasi hiyo zitatangazwa hivi karibuni. Tume imefanya hivyo kwa kuwa ilikuwa bado haijamjulisha Spika wa Bunge, kuhusu kukamilika kwa uchaguzi huo na kuchaguliwa kwa Faki,” imesema taarifa ya Dk. Mahera.

Faki alijiuzulu nafasi hiyo siku 15 baada ya kutangazwa mshindi wa uchaguzi mdogo wa Jimbo la Konde, uliofanyika tarehe 18 Julai 2021, baada ya aliyekuwa mbunge wa jimbo hilo, Khatib Said Haji kupitia ACT-Wazalendo, kufariki dunia.

Katika uchaguzi huo, Faki alimbwaga aliyekuwa mgombea wa ACT-Wazalendo, Mohammed Said Issa.

Haji aliyeliongoza jimbo hilo kwa zaidi ya miaka 10 akiwa Chama cha Wananchi (CUF) na ACT-Wazalendo, alifariki dunia  Mei 20, 2021, katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, alikokuwa anapatiwa matibabu.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi