loader
Dstv Habarileo  Mobile
Rais Samia, Dk Mwinyi, Ndugai wamlilia Kwandikwa

Rais Samia, Dk Mwinyi, Ndugai wamlilia Kwandikwa

RAIS Samia Suluhu Hassan amesema aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa (JKT), Elias Kwandikwa, alikuwa mzalendo na mahiri katika uongozi.

Kwandikwa alifariki dunia juzi usiku katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, mkoani Dar es Salaam. Kiongozi huyo alizaliwa Julai Mosi, 1966. Alikuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa tangu Desemba mwaka jana alipoteuliwa na Rais John Magufuli kushika wadhifa huo mpaka mauti yalipomkuta juzi.

Kutokana na kifo chake, Rais Samia alisema kupitia ukurasa wake wa Twitter kuwa anakumbuka umahiri wa Kwandikwa katika uongozi na uzalendo wake. “Nasikitika kuwajulisha kuwa aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Elias Kwandikwa, amefariki dunia. Nitakumbuka umahiri wake katika uongozi na uzalendo.

Natoa pole kwa familia, Jeshi, Bunge na wananchi wa Jimbo la Ushetu,” alisema Rais Samia. Kupitia taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari jana, Samia alimtaka Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Jenerali Venance Mabeyo kufikisha salamu zake za pole kwa familia ya Marehemu, ndugu, jamaa, marafiki na wote walioguswa na msiba huo.

Alisema taifa limempoteza mtu muhimu ambaye mchango wake katika utumishi wa umma hautasahaulika na alikuwa shupavu katika kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia sheria na taratibu. Rais wa Zanzibar, Dk hussein Mwinyi jana alimtumia salamu za rambirambi Rais Samia kutokana na kifo hicho.

Taarifa iliyotolewa jana na Mkurugenzi wa Mawasiliano Ikulu, Zanzibar Abdul Van Mohamed, ilisema Rais Dk Mwinyi alipokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Kwandikwa aliyekuwa akipatiwa matibabu Muhimbili kwa takribani siku 14.

Mohamed alisema enzi za uhai wake, Kwandikwa alikuwa mtu wa kujitolea kwa dhati kuitumikia Tanzania kwa bidii na kwamba, kabla ya Kwandikwa hajaitumikia wizara hiyo, Dk Mwinyi alihudumu katika wizara hiyo. “Marehemu Mhe. Elias John Kwandikwa, aliteuliwa na marehemu Rais John Magufuli kuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Jumamosi Desemba 5 mwaka 2020 nafasi ambayo awali aliihudumu Rais wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi,” alisema.

Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai kupitia taarifa yake kwa umma jana, alisema alipokea kwa mshtuko na masikitiko taarifa za kifo cha Kwandikwa. “Natoa pole kwa serikali, wabunge, familia na wananchi wa Jimbo la Ushetu. Mwenyezi Mungu awape moyo wa ustahimilivu na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu,”alisema Ndugai. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa jana alisitisha ziara ya siku sita mkoani Mbeya ili akashiriki kwenye msiba wa Kwandikwa. Majaliwa alifika Mbeya Agosti Mosi mwaka huu na tayari alifanya ziara katika halmashauri za Busokelo, Kyela na Rungwe.

Kutokana na kifo cha Kwandikwa, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kimepoteza mtu muhimu aliyekuwa na mchango mkubwa kwa CCM na utumishi wa umma. Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM Taifa, Shaka Hamdu Shaka, alibainisha hayo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari jana. Kupitia taarifa hiyo Mwenyekiti wa CCM Taifa Rais Samia alisema CCM kimepoteza mwanachama na mtu muhimu ambaye mchango wake katika utumishi wa umma hautasahaulika.

Kwa mujibu wa Shaka, Kwandikwa alikuwa Mjumbe wa Kamati ya Siasa katika Wilaya za Kibaha Mjini mwaka 2012-2015 na Kahama mwaka 2015 mpaka umauti unamkuta. Pia alikuwa Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Shinyanga mwaka 2015 na Mbunge wa Jimbo la Ushetu kuanzia mwaka 2015-2021, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kuanzia mwaka 2017-2020 na Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa hadi umauti unamfika.

Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Donald Wright, kupitia ukurasa wake wa Twitter, alituma salamu zake rambirambi zake kwa familia, marafiki na taifa kwa jumla kutokana na kifo cha Waziri Kwandikwa. Balozi Wright alisema Taifa limepoteza kiongozi na mtumishi wa umma mzalendo kwa taifa lake. Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk Philemon Sengati alisema Kwandikwa alijitoa kusaidia jamii na taifa katika kusukuma maendeleo. Dk Sengati aliyasema hayo jana alipokwenda nyumbani kwa marehemu katika Kijiji cha Butibu katika Kata ya Kinamapula Halmashauri ya Ushetu.

“Tumeona tuje waliko wazazi wake na ndio alipozaliwa kuungana na familia na kujua utaratibu utakuaje yupo mdogo wake na marehemu Emily Kwandikwa tumemkuta hapa nyumbani ambaye atatoa ushirikiano kwenye serikali ya mkoa,” alisema. Akaongeza: “Marehemu alikuwa na ushawishi wa kuleta mradi ya maendeleo kama vile umeme, maji na barabara na alikuwa waziri pekee ndani ya mkoa aliyeleta mchango wake na tuliusikiliza; kweli ameacha pengo kubwa mchango wake bado tukiuhitaji.”

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Mkoa wa Shinyanga Mabala Mlolwa, alisema Kwandikwa alikuwa mtu wa watu. Mlolwa alisema yeye ni mmoja wa wanafamilia ya Kwandikwa sababu alikuwa rafiki yake wa karibu na kumuweka kama ndugu wa karibu kwa kutoa ushauri hata ndani ya Chama Cha Mapinduzi.

Imeandikwa na Matern Kayerana Ikunda Erick (Dar), Kareny Masasy (Ushetu), Joachim Nyambo (Mbeya)

foto
Mwandishi: Na Matern Kayera

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi