loader
Dstv Habarileo  Mobile
Bunge- Wabunge wanalipa kodi

Bunge- Wabunge wanalipa kodi

OFISI ya Bunge imesema taarifa zinazodai kuwa wabunge hawalipi kodi kwenye mishahara si kweli hivyo zipuuzwe.

Taarifa ya Kitengo cha Mawasiliano na Uhusiano wa Kimataifa cha ofisi hiyo ilieleza jana kuwa, wabunge kama ilivyo kwa watumishi wengine wa umma na viongozi wa kisiasa, wanakatwa kodi zote stahiki kwa mujibu wa sheria ikiwamo Kodi ya Mapato (PAYE) inayokatwa kwenye mishahara.

“Tunaomba umma upuuze taarifa hizo na tunatoa wito kwa vyombo vya habari hususani mitandao ya kijamii kuzingatia weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa habari pamoja na kuwasiliana na mamlaka husika ili kupata ukweli kabla ya kutoa taarifa kama hizi,” ilisema taarifa hiyo kwa umma.

Awali, Mbunge wa Mvumi katika Wilaya Chamwino mkoani Dodoma, Livingstone Lusinde alimpinga Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali mstaafu (CAG), Ludovick Utouh aliyesema wabunge hawakatwi kodi na kueleza kwamba wabunge wanakatwa kodi kama Watanzania wengine. Lusinde jana aliwaeleza waandishi wa habari jijini Dodoma kuwa, alichokisema CAG mstaafu Utouh si kweli kwani wabunge wanalipa kodi kwa mujibu wa sheria.

“Hivi kweli Utoh kama CAG mstaafu hajui kwamba wabunge wanakatwa kodi, hilo ni jambo la aibu katika nchi yetu,” alisema. Katika kuthibitisha kwamba wabunge wanakatwa kodi, Lusinde alitoa karatasi ya mshahara wake kutoka ofisi ya Bunge na kuwaonesha waandishi wa habari mshahara wake unakatwa kodi.

Karatasi hiyo ya malipo ya mshahara ilionesha, katika mshahara wake wa Sh milioni 4.6 amekatwa kodi Sh milioni 1.2 na kueleza kuwa sio kweli kwamba wabunge hawakatwi kodi.

foto
Mwandishi: Na Magnus Mahenge, Dodoma

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi