loader
Dstv Habarileo  Mobile
Sakata la umeme Moro lasimamisha watatu

Sakata la umeme Moro lasimamisha watatu

WAZIRI wa Nishati, Dk Medard Kalemani ameagiza kusimamishwa kazi watumishi watatu wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoani Morogoro ili kupisha uchunguzi wa tukio la moto katika Kituo cha Kupokea na Kupooza Umeme cha Msamvu.

Dk Kalemani pia amemuagiza a Katibu Mkuu wizara hiyo, Leonard Masanja aunde kamati ya ngazi ya wizara kuchunguza tukio hilo na impe matokeo ndani ya siku tano. Aliagiza uchunguzi huo pia umuhusishe mfanyakazi wa kampuni ya Yapi Merkezi inayojenga Reli ya Kisasa (SGR).

Dk Kalemani alitoa maagizo hayo jana alipotembelea eneo la Tungi, Manispaa ya Morogoro ilipo kebo ya umeme. Alisema chanzo cha kuungua moto jengo la mitambo katika kituo cha kupooza na kusambaza umeme cha Msamvu ni kukatwa kwa bomba lenye kebo iliyochimbiwa chini ya ardhi ambayo inaunganika na kituo hicho.

Alisema uzembe wa kukatwa kwa kebo hiyo ni kutokana na kutokuwapo kwa alama kwenye maeneo yote yenye kebo. Dk Kalemani alisema msimamizi wa Tanesco katika mradi wa SGR alitakiwa kuhakikisha maeneo yote anayosimamia yanakuwa na alama na mipaka inaonekana.

“Kamati hii naipa siku tano iwasilishe taarifa kwangu na endapo itathibitika kuna uzembe hatua za kisheria zitachukuliwa na kama haitadhibitika warejeshwe kazini,” alisema. Dk Kalemani alisema moto katika kituo hicho ulisababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni mbili.

foto
Mwandishi: Na John Nditi, Morogoro

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi