loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wakurugenzi wapya watakiwa kuripoti Dodoma kesho

Wakurugenzi wapya watakiwa kuripoti Dodoma kesho

WAKURUGENZI wapya 69 walioteuliwa kwa mara ya kwanza na Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni kuongoza halmashauri na manispaa, wametakiwa kuripoti Dodoma kesho kwa ajili ya kupewa maelekezo ya kazi.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana Dodoma na Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano Serikalini wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Nteghenjwa Hosseah, wakurugenzi hao wanatakiwa kufika katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma-Mkapa House saa 3:00 asubuhi.

Hosseah alisema Waziri wa Tamisemi, Ummy Mwalimu alitoa tangazo hilo la kuwataka wateuliwa hao kuripoti wakiwa na cheti cha kuzaliwa, Kitambulisho cha Taifa, wasifu binafsi (CV), vyeti ya kitaaluma na picha mbili. Aidha, taarifa hiyo ilisema wakurugenzi ambao wamehamishwa vituo na wanaoendelea kuwepo kwenye vituo vyao vya awali waendelee na utaratibu wa kwenda kuripoti kwenye vituo vyao vya kazi kwa ajili ya makabidhiano kuanzia jana.

Taarifa hiyo ilisema wakurugenzi ambao uteuzi wao umesitishwa wanapaswa kuripoti kwa makatibu tawala wa mikoa yao mara moja. Juzi Tamisemi ilitoa siku tano kuanzia jana kwa wakurugenzi wapya wa majiji, manispaa, miji na halmashauri za wilaya wafike kwenye vituo vya kazi kuanza kutekeleza majukumu yao.

Ummy aliwataka wakurugenzi hao waende kuripoti kwa makatibu tawala wa mikoa kwenye mikoa husika. Rais Samia Suluhu Hassan aliteua wakurugenzi 184 na kwa mujibu wa Ummy, 70 kati yao wamehamishwa kutoka vituo vyao vya kazi na 45 wamebaki walipokuwa.

“Aidha, katika idadi hiyo wakurugenzi 69 ni wapya wakiwemo 15 walioteuliwa kujaza nafasi 54 zilizoachwa wazi baada ya waliokuwa wakurugenzi katika nafasi hizo kutenguliwa,” alisema Ummy.

Alisema miongoni mwa wakurugenzi wapya, 33 sawa na asilimia 48 ni wanawake na hivyo kufanya idadi ya jumla ya wanawake wakurugenzi kufikia 55 sawa na asilimia 29 ya wakurugenzi wote nchini.

foto
Mwandishi: NA MWANDISHI WETU

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi