loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mamia wajitokeza vituo vya chanjo ya corona

Mamia wajitokeza vituo vya chanjo ya corona

AJUZA mwenye umri wa miaka 90, Zahrakhanu Ladak ni miongoni wa mamia ya wananchiwaliojitokeza Dodoma kupata chanjo ya kujikinga na virusi vya corona vinavyosababisha ugonjwa hatari wa covid -19.

Mkuu wa mkoa huo, Anthony Mtaka jana alizindua utoaji chanjo hiyo mkoani humo na kukemea upotoshaji na kuhimiza wananchi wachanje ili kujilinda. “Uhai wangu ni mali yangu, mimi ninawajibika kuulinda na kuutunza.

Rais Samia Suluhu Hassan ametoa mwanga, anabeba dhamana ya familia na taifa kila moja anatakiwa kuthamini uhai wake,” alisema Mtaka wakati akizindua chanjo hiyo na kuongeza: “Kuna akili za kijinga sana eti viongozi wanachanja maji, hayo ni maneno ya upotoshaji sana, sasa wale matomaso wanaosema ni maji waache kupotosha wananchi, kuna mizaha mingi kwenye masuala ya misingi ila chanjo ni muhimu waache kupotosha wananchi.”

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Best Magoma alisema walipokea dozi 50,000 za chanjo ya corona na vimetengwa vituo 28 vya kutoa chanjo hiyo mkaoni humo.

Mbunge wa Dodoma Mjini, Antony Mavunde alisema kirusi cha corona kimekuwa kikibadilika mara kwa mara na serikali inalinda na kuwakinga wananchi ndiyo maana ikaleta chanjo hiyo.

“Tujifunze kuheshimu sayansi na utaalamu, naamini linalofanyika ni kwa nia njema, wenye hiyari wajitokeze kwa ajili ya kupata chanjo hiyo,” alisema Mavunde.

Mbunge wa Viti Maalumu, Fatma Tawfique alisema Rais Samia aliona umuhimu wa wananchi kupata chanjo ili kupambana na janga la covid-19.

Mkuu wa Wilaya ya Dodoma Mjini, Jabir Shekimweri alisema tangu saa 2:00 asubuhi wananchi walifika kwa wingi vituoni kusubiri kupata chanjo.

Alisema wilaya ya Dodoma Mjini imepokea chanjo 15,000 na kuwataka wananchi wajitokeze kuchanja kwani chanjo hizo ni bure.

Dar es Salaam Wakazi wa Dar es Salaam jana walijitokeza kwa wingi katika vituo vya afya kupata chanjo ya corona.

Chanjo iliyotolewa jana ililenga makundi matatu wakiwemo wahudumu wa afya, watu wenye magonjwa sugu na watu wazima kuanzia miaka 50 na kuendelea.

Wananchi wengi nje ya makundi hayo pia walijitokeza wakitaka kupata chanjo hiyo.

Miongoni mwa watu waliojitokeza ambao hawakukidhi vigezo ni Halima Majaliwa, mkazi wa Mburahati aliyeenda katika Kituo cha Afya cha Magomeni.

“Nimejiandikisha kwa mtandao nina siku nne sasa na leo nimefika hapa kupata chanjo lakini nimezuiwa naambiwa sijafikisha miaka 50, naiomba serikali iangalie hili ni watu wengi zaidi wanahitaji chanjo hivyo tupate wote,” alisema Majaliwa.

Mwananchi mwingine, Kulwa Mlewa alisema ni muhimu chanjo kuongezwa ili watu waweze kuipata kwa urahisi.

“Nimefika kituoni asubuhi lakini chanjo nimekosa kwasababu ya umri wangu, naomba serikali iangalie hili watu wote wapate kwani ugonjwa huu haubagua,” alisema.

Mkazi wa Manzese aliyepata chanjo katika Kituo cha Afya Palestina, Abedi Waziri alisema hakujisikia mabadiliko yoyote mwilini baada ya kupata chanjo hiyo.

“Serikali ikisema watu wasipinge, tuiamini kwani haiwezi kutuletea vitu visivyofaa, hivyo nawashauri watu wenye mtazamo hasi wajitokeze kupata chanjo ili kusaidia afya zao,” alisema.

Msimamizi wa chanjo katika Kituo cha Afya Palestina, Dk Nchang’wa Nhumba alisema wameweka mfumo mzuri kuhakikisha watu wote waliokusudiwa wanatapa chanjo hiyo.

Mkazi wa Dar es Salaam, Maulid Ahmed ambaye alipata chanjo siku tatu zilizopita alisema anaendelea vizuri.

“Siku ya kwanza nilikuwa kawaida sikupata maumivu ila siku ya pili saa 4:00 nilijisikia homa, kichefuchefu lakini sasa naendelea vizuri,” alisema.

Daktari Bingwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Daudi Shabani alisema amefurahi kupata chanjo hiyo.

Mhudumu wa Afya katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa ya Muhimbili (MOI), Mariam Materu alisema hakuona mabadiliko yoyote hasi baada ya kupata chanjo hiyo.

Katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Mfamasia Mkuu, Zawadi Secha alisema watu walijitokeza kwa wingi kupata chanjo na wamejipanga kuhakikisha huduma inatolewa kwa usahihi.

Arusha Mkuu wa Mkoa Arusha, John Mongela jana alizindua chanjo hiyo jijini humo na kuelekeza kuwa waipate wenye umri zaidi ya miaka 18 na kupaumbele kiwe kwa watu wazima.

“Chanjo sio nyingi ila zitatosha, naomba watu wasiwe na taharuki sababu wanaostahili kuipata wataipata na serikali inaendelea kufanya juhudi kuzileta nyingine ili kila mtu apate,” alisema Mongella.

Baada ya kupata chanjo hiyo jijini humo jana, Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Geofrey Pinda alihimiza wananchi wasipuuze kwa kuwa kuna siku wanaweza kuitafuta wa wasiipate.

Alisema serikali imejiridhisha kuwa chanjo hiyo ni salama na hivyo wananchi waende kuipata.

“Sioni sababu ya kutoiamini kama tuliamini majani ya aina mbalimbali siku za nyuma kujifukiza usiku na mchana kwanini tusiamini na chanjo hii ya kisayansi tulioifanyia tathimini katika ubora wake,” alisema.

Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Arusha, Mosses Mzuna alisema majaji ni waamuzi wa kesi, hivyo ili kuziamua vizuri ni lazima kila mmoja awe na afya bora.

Shehe wa Mkoa wa Arusha, Shaaban Juma alisema ni wajibu wa viongozi wa dini kushirikiana na serikali kuelimisha waumini juu ya watu wanaopotosha juu ya chanjo hiyo.

Mwanza Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Robert Gabriel jana aliongoza wananchi kupata chanjo ya corona katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Sekou Toure.

Gabriel alisema kumekuwapo na maneno mengi ya kukatisha tamaa wananchi kupata chanjo hiyo, lakini ni muhimu jamii ipokee kauli ya serikali kuwa chanjo hiyo ni salama.

“Afya yako ni muhimu kuzidi mambo yote, wewe ndo unalo jukumu la kujikinga, umekuwa ukipokea chanjo za aina mbalimbali tangu kipindi cha utoto wako hivyo endelea kujikinga,” alisema.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk Thomas Rutachunzibwa alisema wamepokea dozi 90,000 za chanjo hiyo na zinasambazwa katika vituo 27 vilivyopangwa kutoa chanjo hiyo mkoani humo.

Mtwara Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Brigedia Jenerali Marco Gaguti jana alizindua utoaji chanjo hiyo na akasema mkoa huo umepata dozi 20,000.

Alisema mahitaji ni makubwa kwani mkoa huo unakadiriwa kuwa na watu zaidi ya 250,000 wanaohitaji chanjo hiyo.

“Nawaomba wananchi wa mkoa wa Mtwara kushirikiana na wadau wetu wa afya ili zoezi hili liweze kwenda kama lilivyokusudiwa, jambo la pili ni kuendelea kuzingatia taratibu zote za afya za kujikinga,” alisema.

Gaguti alizindua chanjo hiyo katika Kituo cha Afya cha Likombe Manispaa ya Mtwara Mikindani na kwa mujibu wa Kaimu Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Kodi Mohamed kazi hiyo itafanywa kwa siku saba.

Kigoma Mkuu wa Mkoa Kigoma, Thobias Andengenye jana aliongoza wananchi wa mkoa huo kupata chanjo hiyo ya kujikinga na maambukizi ya virusi vya corona na akakemea upotoshaji.

Andengenye alizindua chanjo hiyo katika Hospitali ya Mkoa Kigoma (Maweni) na kusema serikali haiwezi kuwa na lengo baya kwa wananchi wake kwani ina taarifa za kutosha kuhusu manufaa ya kinga hiyo.

“Naamini hakuna chanjo ambayo haina maudhi madogo madogo zikiwamo chanjo zaidi ya 14 ambazo Watanzania wengi wamepata tangu wakiwa watoto,” alisema.

Awali, Mganga Mkuu wa Mkoa Kigoma, Dk Simon Chacha alisema walipokea dozi 8,000 za chanjo hiyo na zitatolewa kwenye vituo 24 mkoani humo.

Alisema watu 1,780 wanatarajiwa kupata chanjo hiyo katika awamu ya kwanza.

Morogoro Mkuu wa Mkoa wa Morogoro, Martine Shigella alizindua utoaji wa chanjo hiyo mkoani humo jana na kuwataka wananchi waendelee kuchukua tahadhari.

Mganga Mkuu wa Mkoa Morogoro, Dk Kusirye Ukio alisema chanjo katika mkoa huo itatolewa katika vituo 26.

Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Morogoro, Dk Masumbuko Igembya alisema katika awamu ya kwanza mkoa huo ulipokea chanjo dozi 50,000.

Iringa Mganga Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Dk Mohammed Mang’una jana ilisema Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendiga leo atazindua utoaji chanjo ya corona mjini Iringa.

Aliwaambia waandishi wa habari kuwa watu 30,000 mkoani humo wanatarajiwa kupata chanjo hiyo katika awamu ya kwanza mkoani humo.

Alisema mkoa huo utakuwa na vituo 15 vya kutolea chanjo hiyo kwa mgawanyo wa vituo vitatu kwa kila halmashauri.

“Kwa hapa Iringa Mjini ambako uzinduzi utafanyika, vituo vilivyoteuliwa ni Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa, Hospitali ya Manispaa ya Iringa ya Frelimo na Kituo cha Afya Ngome,” alisema.

Shinyanga Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Dk Yudas Ndungile jana alisema wamepokea dozi 25,000 za chanjo ya corona na wataanza kuitoa leo kwenye vituo 18 mkaoni humo.

Aliliambia HabariLEO kuwa, uzinduzi wa kutoa chanjo hiyo utafanyika kwenye ofisi ya mkuu wa mkoa. Geita Mratibu wa Chanjo Mkoa wa Geita, Wille Luhangija alisema jana kuwa, wanatarajia kupokea dozi 14, 000 za chanjo ya corona na kutakuwa na vituo 18 kwenye halmashauri za Chato, Geita Mji, Geita Wilaya, Mbogwe, Nyang’hwale na Bukombe.

Alisema kazi ya kutoa chanjo hiyo itaanza leo mkoani humo kwa kuanza na makundi ya kipaumbele wakiwemo watumishi wa idara ya afya, wenye magonjwa sugu na watu wazima wenye umri kuanzia miaka 50 “Uzinduzi wa utoaji wa chanjo, utafanyikia kwenye Kituo cha Afya cha Geita Mjini na kila dozi ni kwa mtu mmoja, kwa maana hiyo tunategemea kuchanja watu 14,000 kwa dozi hizi za awamu ya kwanza,” alisema.

Imeandikwa na Veronica Mheta (Arusha), Sifa Lubasi (Dodoma), Aveline Kitomary (Dar es Salaam), Sijawa Omary (Mtwara), Fadhili Abdallah (Kigoma), Suleiman Shagata (Mwanza), Kareny Masasy (Shinyanga), Yohana Shida (Geita), Frank Leonard (Iringa) na John Nditi (Morogoro).

foto
Mwandishi: Waandishi Wetu

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi