loader
Dstv Habarileo  Mobile
Naibu Waziri abaini mapato hafifu ya miradi

Naibu Waziri abaini mapato hafifu ya miradi

NAIBU Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Kundo Mathew amefanya ziara katika Halmashauri ya Wilaya ya Kongwa mkoani Dodoma kukagua maendeleo ya miradi ya mawasiliano na kueleza kutoridhishwa na mapato hafi fu yanayopatikana.

Katika ziara hiyo, Kundo alitembelea ofisi za Shirika la Posta Kongwa, mnara wa mawasiliano wa Shirika la Mawasiliano Tanzania (TTCL) uliopo kijiji cha Chang’ombe katika kata ya Iduo na minara ya Vodacom na Halotel katika kijiji cha Njoge.

Akiwa katika ofisi za Shirika la Posta, Kundo alibaini upungufu kadhaa ikiwemo pamoja na mapato hafifu.

Ofisa Mauzo Msaidizi wa TTCL tawi la Kongwa, Isaya Mpangala alisema miongoni mwa sababu zinazofanya kuwepo kwa wateja wachache ni kutokana na changamoto mbalimbali za kitaalamu. Alisema miongoni mwa mambo yaliyobainika katika ukaguzi huo ni pamoja na minara hiyo kuendeshwa kwa teknolojia ya zamani ya 2G) badala ya 3G na 4G ambayo si rafiki kwa mawasiliano ya mtandao wa intaneti.

Ofisa Mtendaji wa Kijiji cha Chang’ombe, kata ya Iduo, Leila Swai aliishukuru TTCL kwa kuweka mnara kijijini hapo na kutekeleza mkataba wa kulipa posho za walinzi kwa wakati.

Hata hivyo, baadhi ya wananchi walisema mikataba ya wawekezaji wa minara katika kijiji cha Njoge ni kandamizi.

Walilalamikia tozo ndogo na mikataba ya kudumu kwa miaka mingi pasipo kufanyiwa marekebisho.

Kutokana na malalamiko hayo, Kundo aliziagiza kampuni zote zilizowekeza na zitakazohitaji kuwekeza katika minara ya mawasiliano kufika katika ofisi ya mkurugenzi mtendaji wa halmashauri husika ili kukamilisha taratibu za kisheria kabla ya kufanya uwekezaji.

Alizitaka pia kampuni zote zinazolipa tozo kwa watu wasiotambuliwa na viongozi na wananchi wa maeneo husika kusitisha malipo hayo hadi taratibu zitakapofuatwa ili yaelekezwe kwa watu au mamlaka halali.

foto
Mwandishi: Sifa Lubasi, Kongwa

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi