loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kabudi ahimiza matumizi Kiswahili cha kiserikali

Kabudi ahimiza matumizi Kiswahili cha kiserikali

WAZIRI wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi ameeleza kukerwa na kitendo cha baadhi ya watumishi wa umma kutumia lugha za mitaani ofisini.

Profesa Kabudi alisema hayo wakati wa ziara yake ya kikazi mkoani Singida ambako alikutana na viongozi waandamizi wa Mahakama na wadau wa utoaji haki.

“Nimekasirika, nimefadhaika, nimeghadhabika kuona ndani ya serikali baadhi ya watumishi wameanza kupoteza umahiri wa kuandika Kiswahili cha kiserikali na badala yake kinachotumika zaidi ni kile cha mtaani. Napenda ifahamike serikali ina Kiswahili chake,” alisema.

Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, miaka ya nyuma mtumishi alikuwa hawezi kupanda daraja bila kufaulu mtihani wa Kiswahili uliotungwa na Chuo cha Utumishi wa Umma Magogoni.

“Ni lazima tuanze kujifunza na kuandika nyaraka na miongozo kwa kutumia Kiswahili cha serikali,” alisema.

Akizungumzia uendeshaji wa mashauri kwa kutumia lugha ya Kiswahili, Profesa Kabudi alisema kwa sasa wapo kwenye hatua ya kutengeneza kamusi ya Kiswahili cha kisheria itakayotafsiri sheria mbalimbali.

“Lugha hii ni fahari kwa taifa na lengo hasa la kutengeneza kamusi na kitabu cha Kiswahili cha kisheria ni kuongeza ‘access to justice’ (upatikanaji wa haki) na tunatarajia mpaka ifikapo Juni, 2022 kanuni za sheria mbalimbali zitakuwa zimetafsiriwa,” alisema.

Profesa Kabudi aliwaagiza watendaji wa Mahakama mkoani humo waharakishe mchakato wa kuandaa eneo la ujenzi wa Mahakama ya wilaya ya Manyoni.

“Ujenzi wa mahakama hii ambayo itashughulikia kesi za ujangili, kulinda utajiri wa asili na mali za asili haukwepeki na upo kwenye mpango wa mwaka huu wa fedha, nataka kufikia Ijumaa muwe mmeainisha eneo la ujenzi wake na mmeshughulikia vibali vyote na nitafika kukagua,” alisema.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu, Singida

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi