loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mnada majani ya chai kufanyika bandarini Dar

Mnada majani ya chai kufanyika bandarini Dar

WIZARA ya Kilimo imesema Desemba mwaka huu mnada wa majani ya chai utafanyika katika Bandari ya Dar es Salaam.

Naibu Waziri wa wizara hiyo, Husein Bashe alisema hayo juzi Rungwe, mkoani Mbeya.

Alisema awali mnada huo ulikuwa ukifanyika Mombasa nchini Kenya. Bashe alisema hayo wakati Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alipotembelea shamba la chai la la Kyimbila nje kidogo ya mji wa Tukuyu linalomilikiwa na Shirika la Wakulima Tea (Watco) wilayani humo.

“Mnada wa majani ya chai katika Bandari ya Dar es salam utaondoa madalali na propaganda zilizokuwa zinafanywa na mataifa ya kigeni kubeza chai yetu na hii itaongeza bei katika soko, tija kwa mkulima na mwonekano chanya katika mataifa ya kigeni,” alisema.

Majaliwa alitembelea shamba hilo alipowasili wilayani Rungwe akitoka wilaya ya Kyela ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kikazi mkoani Mbeya.

Aliwasihi wakulima waendelee kujiunga katika vyama vya ushirika na kuitaka Watco iwape bure miche ya zao hilo ili waongeze uzalishaji.

Awali, Majaliwa alizindua awamu ya tatu ya mafunzo ya stadi za kazi kwa njia ya uanagenzi kwa vijana 14,440.

Taarifa ya ofisi ya Waziri Mkuu ilieleza kuwa, Waziri Mkuu alisema serikali imetenga Sh bilioni tisa kwa ajili ya kugharamia mafunzo hayo kwa vijana.

“Vijana ambao hawakubahatika kupata nafasi ya kushiriki mafunzo kwa awamu hii wawe na subira kwani tunaendelea kuandaa fursa hizi kupitia vituo vingine na tutatangaza tena,” alisema Majaliwa.

Alizitaka mamlaka za serikali za mitaa ziwaunganishe vijana kwenye vikundi vya ushirika na kuwapatia mikopo na nyenzo za kufanyia kazi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Jenista Mhagama alisema mafunzo hayo yameandaliwa kimkakati.

foto
Mwandishi: Joachim Nyambo, Rungwe

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi