loader
Dstv Habarileo  Mobile
TBC yaongeza neema Ligi Kuu

TBC yaongeza neema Ligi Kuu

SHIRIKA la Utangazaji Tanzania (TBC) limeingia mkataba na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wa haki ya urushaji wa matangazo ya Ligi Kuu Tanzania Bara upande wa redio kwa miaka 10 wenye thamani ya Sh bilioni 3.5.

Mkataba huo umekuja miezi mitatu baada ya kampuni ya Azam Media kupata haki ya kurusha matangazo ya michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara kwa upande wa televisheni wenye thamani ya Sh bilioni 225.6 kwa miaka 10.

Akizungumza baada ya kusaini mkataba na TBC jana, Rais wa TFF, Wallace Karia alisema shirikisho hilo litakuwa linapokea Sh milioni 300 kila mwaka kutoka shirika hilo, fedha ambazo zitakuwa zikigawiwa sawa kwa klabu zote zinazoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara kuanzia msimu wa 2021/22.

“Nawapongeza TBC kwa kushinda tenda nina imani tutakuwa na ligi bora, kuendesha mpira ni gharama kubwa,TFF itahakikisha timu zote zinapata gawio sawa kwa ajili ya kuendesha timu na mwisho wa mwaka zitawasilisha matumizi ya fedha ambazo zimepata kwa mkaguzi wa mahesabu.”

“Tunajua kuendesha mpira kunahitaji fedha, viongozi wanatakiwa kuzitumia katika matumizi sahihi, kwa sasa ligi yetu iko kwenye nafasi nzuri, kwa Afrika tuko nafasi ya nane, hii ni jambo la kujivunia,” alisema Karia.

Karia alisema katika Ligi Kuu hakuna timu kubwa ndio maana zote zinashiriki na mgao wote utakuwa sawa na fedha hizo zitasaidia kupata huduma kama usafiri na malazi zinapokwenda kucheza ugenini.

“Udhamini huu utaleta ushindani mkubwa kwa soka la Tanzania, hii inaonesha kila timu inapata fedha za kujikimu katika mahitaji yao.”

Haya ni maendeleo makubwa katika soka la Tanzania ambalo linakua kwa kasi na kufuatiliwa na wachezaji kutoka mataifa makubwa kisoka kama Ghana, Jamuhuri ya Kidemokrasia Congo, Zambia na Ivory Coast ambao wamekuwa wakija kutafuta nafasi kucheza soka hapa nchini,” alisema Karia.

Naye Mratibu wa Masoko wa TBC, Gabriel Nderumaki alisema Shirika la Utangazaji ni chombo cha umma hivyo wana haki ya kufanya matangazo ya michezo kuwafikia watu wengi zaidi ndani na nje hivyo wamepata haki ya kurusha matangazo ya Ligi Kuu Tanzania Bara kuanzia msimu wa 2021/22.

“TBC ina mtandao mpana wa satelaiti kuwafikia watu wengi zaidi kuliko chombo chochote hapa nchini na inasikika hadi nje ya mipaka yetu hivyo kuifanya nchi yetu kujitangaza kimataifa kupitia mchezo wa soka.

“Pia TBC ina dhima ya kuhamasisha ari ya mashindano ya michezo mbalimbali katika michezo ya ndani na imekuwa ikitangaza Ligi Kuu, Kombe la Mapinduzi na michezo mbalimbali ya ndani, “ alisema Nderumaki.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/e7e8bbcbcc6cfcfc52f5728d1dcd0e07.jpg

BAADA ya Yanga kuondolewa kwenye michuano ya Ligi ...

foto
Mwandishi: Martin Mazugwa

Post your comments

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi