loader
Dstv Habarileo  Mobile
Waelimisha rika wawezeshwe masuala ya afya kazini

Waelimisha rika wawezeshwe masuala ya afya kazini

HIVI karibuni Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma iliendesha semina ya siku mbili kwa waelimisha rika katika Chuo cha Mafunzo ya Ufundi Dar es Salaam (DIT), lengo lilikuwa ni kuwajengea uwezo wa namna ya kushughulikia ugonjwa wa ukimwi na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukizwa mahala pa kazi.

Katika mada zilizotolewa na watoa mada kwenye semina hiyo ambao ni ofisa kutoka ofisi hiyo, Filbert Temba, Meneja Rasilimali Watu wa DIT, Lawrence Thobias na Daktari wa Chuo Godwin Ndaki, kati ya mambo muhimu waliyotilia mkazo ni pamoja na umuhimu wa waelimisha rika kutunza   siri za ugonjwa wa wafanyakazi.

Binafsi mbali na kuunga mkono jitihada hizo za Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma katika kuwajengea uwezo waelimisha rika, ninaona kuna wajibu bado wa suala hilo la elimu kutiliwa mkazo hasa eneo la utunzaji wa siri za wafanyakazi wanaojitambulisha kuugua magonjwa mbalimbali.

Ifahamike kuwa, waelimisha rika ndiyo watu wa kwanza katika kuratibu afya za wafanyakazi katika maeneo ya kazi, hii inatokana na kuwa kundi hilo linahusisha wakuu wa vitengo ambao hufanya kazi kwa karibu zaidi na kamati za kufuatilia afya za wafanyakazi.

Kutokana na ukaribu wao katika kuelimisha na kufuatilia afya za wafanyakazi, wanakuwa watu wa kwanza kufahamu ni mfanyakazi ugonjwa gani unamsumbua, hivyo wanao wajibu wa kutunza siri za mgonjwa husika.

Ni vema waelimisha rika mkatambua kuwa mmebeba dhamana kubwa ya wafanyakazi ambayo inaweza kusaidia ufanisi wa kazi kama mkizingatia miongozo ya kazi zenu na siyo vinginevyo.

Mnao wajibu wa kutotoa siri kama mfanyakazi akieleza kuwa ameathirika na ugonjwa wa ukimwi au ugonjwa wowote ambao anakuwa hayupo tayari kuuweka wazi.

Hii inatokana na ukweli kuwa, wapo wafanyakazi ambao licha ya kuwa ni haki yao kutoa taarifa za ugonjwa ili kusaidiwa, wanasita kutoa taarifa hizo kutokana na kuhisi kutangazwa, sasa kama wakihakikishwa kuwa taarifa zao zitakuwa siri wanaweza kujitokeza na kujieleza.

Mfano, katika ofisi ambayo ina wafanyakazi wagonjwa ambao ugonjwa wao unawataka kuwa wanaenda mara kwa mara hospitalini kuchukua dawa, kama wakifahamu kuwa taarifa za kuumwa kwao zinatangazwa hata kwa watu wasiopaswa kujua, wanaweza kuathirika zaidi.

Lakini pia kwa ofisi ambazo hazina waelimishaji rika wenye weledi wa kutosha, hilo nalo ni tatizo kwa ofisi husika na ninaiomba ofisi hiyo ya Rais kuzishughulikia ofisi zisizokuwa na waelimisha rika. Wanapaswa kuwepo na pia wawezeshwe kutoa elimu hiyo mara kwa mara.

Waelimisha rika waendelee kupewa elimu ya mara kwa mara ili kuongeza uwezo wao wa kutoa elimu lakini pia mapendekezo yao kufanyiwa kazi, mfano wakipendekeza ofisi iwe na utamaduni wa mazoezi ya mara kwa mara basi ushauri huo utekelezwe.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/a068d65766641be33f1129d1655f279d.jpeg

WIKI iliyopita umefanyika uzinduzi wa siku ...

foto
Mwandishi: Evance Ng’ingo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi