loader
Dulla Mbabe,   Kiduku kimeumana

Dulla Mbabe,  Kiduku kimeumana

MABONDIA wa ngumi za kulipwa, Abdallah Pazi ‘Dulla Mbabe’ na Twaha Kiduku wanapanda ulingoni leo kuzichapa, huku kila mmoja akimtambia mwenzake kuwa kitaeleweka. 

Pambano hilo la kuwania gari aina ya Toyota Crown litapigwa Ubungo, Dar es Salaam. 

Hii ni mara ya tatu mabondia hao kukutana katika ulingo. Mara mbili walizochuana huko nyuma, Kiduku aliondoka kidedea katika pambano moja na jingine walitoka sare.

Pambano hilo litakuwa la raundi 10 katika uzito wa Super Middle kilo 75 na awamu hii huenda pakawaka moto, kwani Kiduku anayetokea Morogoro amepania kuendeleza kichapo kwa mpinzani wake na Dulla Mbabe akisema hatokubali kushindwa tena lazima afe mtu.

“Namshukuru Mwenyezi Mungu nimejiandaa vizuri jambo la muhimu niamke nikiwa na afya njema,” alisema Kiduku.

Kwa upande wake Dulla alisema: “Tukutane kesho (leo) kitaeleweka, naomba Mungu niwe na afya njema kama leo (jana).”

Hii itakuwa ni mara ya kwanza kuwa na pambano kubwa kama hilo kisha mshindi anaondoka na gari.

Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Omary Kumbilamoto amewapongeza waandaaji wa pambano hilo kwa kile ambacho wanakifanya katika kuendeleza mchezo huo na kusema serikali itawaunga mkono katika mapambano mengine yajayo.

Aliwataka mapromota kuwa na hofu ya Mungu kwa kuhakikisha atakayeshinda anapata haki yake.

Alisema atahudhuria pambano hilo kuunga mikono mchezo huo akiamini ni ajira na inabadilisha maisha ya watu.

Mratibu wa pambano hilo, Seleman Semunyu alihimiza wadau na mashabiki wa ngumi kujitokeza na kuwaunga mkono mabondia hao akisema maandalizi yamekamilika.

“Maandalizi ya pambano yamekamilika, Kiduku na Dulla Mbabe watapanda kwenye ulingo saa 6:00 usiku, tunaomba mashabiki wajitokeze kwa wingi,” alisema.

Mabondia wengine watakaopanda ulingoni kuwasindikiza mabondia hao ni Cosmas Cheka dhidi ya Ismail Galiatano, Selemani Kidunda dhidi ya Paulo Kameta, George Bonabucha dhidi ya Sunday Kiwale, Seba Temba dhidi ya Albano Clement, Grace Mwakamela dhidi ya Felista Mwakatika, Jamal Kunoga dhidi ya Christopher Steven na Saidy Said dhidi ya Jay Jay Ngotiko.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/f784e4901e4571f679b654c5d0e044ad.jpeg

KLABU ya Simba imegomea kuvaa nembo ...

foto
Mwandishi: Grace Mkojera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi