loader
Dstv Habarileo  Mobile
Hongera serikali kwa hoja za Muungano

Hongera serikali kwa hoja za Muungano

KUTATULIWA Kwa hoja 11 Za Muungano kunatoa taswira ya Serikali za Jamhuri ya Muungano na ile ya Mapinduzi ya Zanzibar namna zilivyodhamiria kumaliza kero za Muungano.

Kero za Muungano zimekuwa zikishughulikiwa na kupunguzwa na serikali tangu Awamu ya Kwanza chini ya Mwalimu Julius Nyerere, Awamu ya Pili iliyoongozwa na Ali Hassan Mwinyi, Awamu ya Tatu ya Benjamin Mkapa, Awamu ya Nne iliyoongozwa na Jakaya Kikwete na Awamu ya Tano chini ya John Magufuli.

Katika vipindi hivyo, serikali imeendelea kushughulikia hoja za Muungano hadi kufikia hoja 11 katika Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu iliyojitahidi zaidi kuzishughulikia.

Ninasema serikali sasa imedhamiria kushughulikia kikamilifu zaidi hoja za Muungano kwa kuwa ndani ya muda mfupi, imefanikiwa kumaliza kabisa hoja tisa za Muungano na kubakiza hoja mbili.

Kati ya hoja 11, tisa zimetengenezewa hati za makubaliano ya pande mbili huku hoja mbili hazikusainiwa kwa sababu zipo katika ngazi ya utendaji zaidi.

Hoja zilizosainiwa ni pamoja na Bahari Kuu, Uingizaji wa maziwa kutoka Zanzibar, Ajira kwa watumishi wa Zanzibar katika taasisi za Muungano na Mgawanyo wa misaada inayotoka nje. 

Hoja nyingine ni Mkataba wa mkopo wa fedha za mradi wa ukarabati wa Hospitali Kuu ya Mnazi Mmoja na Mkataba wa mkopo wa Barabara ya Chakechake hadi Wete Pemba.

Nyingine ni Mkataba wa mkopo wa ujenzi wa Bandari ya Mpigaduri, Usimamizi wa ukokotoaji na huduma za simu na Mapato yanayokusanywa na uhamiaji kwa upande wa Zanzibar.

Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya mawaziri, makatibu wakuu na wataalamu kutoka pande zote za Muungano kukutana Zanzibar na kujadili mambo 18 kati ya 25 yaliyoorodheshwa tangu mwaka 2006 ambapo tayari kero saba zilikuwa zimetatuliwa.

Izingatiwe kuwa, mafanikio haya yanaonekana  miezi mitano pekee tangu serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani Machi 19, 2021.

Hii inadhihirisha kuwapo kwa dhamira ya kweli, uzalendo na kutanguliza kwa maslahi ya nchi.

Hiyo ni zawadi kwa waasisi wa taifa hili Abeid Aman Karume na Mwalimu Julius Nyerere waliokuwa mstari wa mbele kuwaunganisha Watanzania kwa kuhakikisha kero za Muungano zinaondolewa na Muungano unadumu.

Kwa msingi huu, wadau wote wa muungano wahakikishe wanauimarisha kwa kuendelea kuzifanyia kazi hoja zinazokinzana zilizopo ili kuuimarisha Muungano wa Tanzania na kuufanya uendelee kustawisha maslahi ya pande zote.

Ndio maana, ninaipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu kwa nia yake ya dhati ya kumaliza kero za Muungano na kudumisha Muungano adhimu wa Tanzania. 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/21d67f09fcc4abeba4071ca8cf77c0c9.jpeg

WIKI iliyopita umefanyika uzinduzi wa siku ...

foto
Mwandishi: Selemani Nzaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi