loader
MWILI WA HAMZA WASUBIRI NDUGU

MWILI WA HAMZA WASUBIRI NDUGU

MWILI wa mtu aliyefanya mauaji ya askari polisi watatu na mlinzi wa kampuni binafsi, Hamza Mohamed, bado upo mikononi mwa Jeshi la Polisi ukisubiri ndugu kuuchukua.

Mkuu wa Jeshi la Polisi Nchini (IGP), Simon Sirro alisema wasipotokea, jeshi litakabidhi kwa Halmashauri.

Alisema hayo jana Dar es Salaam alipozungumza na waandishi wa habari baada ya hafla ya kuwaaga makamishina wa jeshi la polisi, Robert Boaz na Valentino Mlowola.

Hamza ambaye anatajwa kuwa mkazi wa eneo la Fire, Upanga, Dar es Salaam, anadaiwa kufanya mauaji hayo Jumatano iliyopita karibu na Daraja la Selander na Ubalozi wa Ufaransa kabla ya kuuawa kwa majibizano na polisi. Watu wengine sita walijeruhiwa katika tukio hilo.

“Mwili wa Hamza tunawakabidhi ndugu zake kwa sababu tayari tumeufanyia kazi kama ndugu zake hawajaja kuuchukua, waje wauchukue. Lakini siku zikifika muda hawajaja kuuchukua, halmashauri itakwenda kuuzika.

“Lakini niseme ndiyo hayo, hiyo familia inajisikiaje? Familia ya Hamza? Ungekuwa ndiye baba yake Hamza, Mama yake Hamza, mdogo wake Hamza, ungejisikiaje?” aliwaambia waandishi wa habari waliotaka kufahamu hatma ya mwili wa kijana huyo.

IGP Sirro, aliwataka wananchi, hususani wazazi kutowaficha watoto wao ambao ni wahalifu kwani kufanya hivyo kunaweza kuleta madhara kwa watoto hao wenyewe, familia na jamii kwa jumla.

Wakati huo huo: IGP Sirro ameonya watu wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kuandika taarifa za uongo na upotoshaji na kuwataka watumie nguvu hiyo katika kushirikiana kufichua wahalifu.

Alisema baadhi ya watu wanaotumia mitandao ya kijamii hawajui maana ya uvunjifu wa amani na hawajui nchi ikiingia kwenye matatizo hali inakuwaje.

“Nilikuwa naangalia kwenye mitandao baadhi yao hawajui maana ya uvunjifu wa amani, hawajui nchi ikiingia kwenye matatizo hali inakuwaje wangejua wasingeweza kuandika mambo ya uongo; mtu anatengeneza jambo kwenye mtandao sijui kwa faida ya nani! Amani ikipotea ukirudisha ni tabu, wale wanaokomalia mitandao zungumzeni jambo la ukweli,” alisema IGP Sirro.

Aidha, alisema jeshi hilo halipo kwa ajili ya kumuonea mtu, bali lipo kwa ajili ya kutenda haki na kuwashughulikia wahalifu.

“Sisi hatupo kwa ajili ya kumuonea mtu tupo kwa ajili ya kutenda haki, wewe kama unachukua bunduki unategemea nini, tena bunduki ya kijeshi unategemea nini wewe ukiwa na bunduki ukiniwahi sawa nikikuwahi safi, ujue askari na yeye ni binadamu na anapenda kuokoa maisha yake,” alisema.

Alisema kwa sasa makosa yanayosumbua kzaidi ni udhalilishaji, vitendo vya kubaka na i pamoja na dawa za kulevya.

Katika hafla hiyo, Kamishina Robert Boaz alitoa rai kwa askari wanaobakia kazini kuwa na weledi, upendo, uadilifu na nidhamu katika kuwatumikia wananchi.

Aliomba serikali kuwekeza katika teknolojia na vifaa kwani uwanda wa vitendo vya uhalifu unabadilika.

“Kazi ya polisi ni ngumu na ina changamoto nyingi, nashukuru nimefanya kazi na wenzangu kwa moyo mmoja na hadi naondoka jeshini, nashukuru nchi iko salama,” alisema Boaz.

Alisema changamoto za Jeshi la Polisi ni pamoja na masuala ya ugaidi, lakini kwa umoja ndani ya Jeshi la Polisi, ilidhibitiwa.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/4b02a8bcf97bbe15e61a4dd8470ccb4d.jpeg

WAFANYAKAZI wa Kituo cha Redio ...

foto
Mwandishi: Oscar Job

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi