loader
Simba yaileta TP Mazembe

Simba yaileta TP Mazembe

MABINGWA wa soka Tanzania Bara, Simba watacheza na TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) katika kilele cha Tamasha la Simba Day.

Simba Day ni maalumu kwa klabu hiyo kutangaza kikosi chake kwa ajili ya msimu mpya, ambapo kwa mwaka huu itafanyika Septemba 19 kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Akizungumza na HabariLEO jana, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez alithibitisha TP Mazembe ambao ni mabingwa mara tano wa Ligi ya Mabingwa Afrika ndiyo watacheza na Simba siku hiyo.

“Nina furaha kuwatangazia Wanasimba na Watanzania wote kwa ujumla kwamba tutacheza na TP Mazembe siku ya Simba Day Septemba 19 mwaka huu.”

“Tayari tumekamilisha taratibu zote za kuwaalika na sasa ni rasmi wao ndiyo watakuwa wageni wetu,” alisema Barbara.

Alisema TP Mazembe ni moja ya timu zenye heshima kubwa Afrika na ni heshima kubwa kwa Simba kupata fursa ya kucheza nayo.

Barbara alisema lilikuwa lengo la uongozi na benchi la ufundi kuhakikisha Simba inapata timu nzuri ya kucheza nayo Simba Day.

Alisema kwa Afrika, Mazembe inachukuliwa kama mojawapo ya klabu bora na jina lake linahusishwa na mafanikio katika mchezo huo.

Alisema taarifa zaidi kuhusu ujio wa TP Mazembe zitaendelea kutolewa na klabu kuelekea katika Simba Day.

Mara ya mwisho kwa timu hizo kukutana ilikuwa Februari 2, mwaka huu kwenye mashindano maalumu ya Simba ‘Simba Super Cup’ ambapo mechi iliisha kwa suluhu katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Kikosi cha Simba kwa sasa kipo jijini Arusha kwa ajili ya maandalizi ya msimu mpya baada ya kumaliza kambi ya wiki mbili nchini Morocco.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/d80545ba44941694a1146313ffcc4c6c.png

ZIMEBAKI pointi mbili, Mbeya City iwafikie Simba SC ...

foto
Mwandishi: Abdallah Mashaka

Post your comments