loader
Dstv Habarileo  Mobile
Tuwalinde watoto na mimba za utotoni

Tuwalinde watoto na mimba za utotoni

TAARIFA za matukio ya mimba na ndoa za utotoni yanaongezeka nchini, hali inayosababisha watoto kuacha shule na kuharibu ndoto zao huku baadhi yao wakiozeshwa kwa makubaliano ya familia husika kimyakimya.

Licha ya sheria kuwa kali kuhusu wanaume wanaoshiriki mapenzi na watoto wenye umri chini ya miaka 18, kitendo kinachochukuliwa kama kunajisi mtoto, lakini bado matukio hayo yanaendelea.

Kuendelea huko kunatokana na familia mbili, yaani ya mtoto wa kike aliyepata mimba na ya upande wa mwanaume kukaa pamoja na kuyamaliza kimyakimya nje ya mkondo wa sharia. Hili linazidi kukuza tatizo.

Kwa mfano, taarifa zilizo tolewa na Ofisa Ustawi wa Jamii wa Mkoa wa Morogoro, Jesca Kamugela siku chache zilizopita, zinaonesha kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja, 2020/2021, watoto 1,277 walipata ujauzito mkoani humo.

Kwa kuwa wengi wao walikuwa wanafunzi, ni sawa na kusema wanaume zaidi 1,000 walitakuwa wawe jela wakitumikia kifungo cha miaka 30 katika huo ni mkoa mmoja pekee lakini pengine hakuna hata mmoja aliyeko jela!

Kwa mujibu wa Jesca kila halmashauri mkoani humu imekuwa ikitoa ripoti ya matukio hayo na mmomonyoko wa maadili umetajwa kuwa chanzo kikubwa cha mimba hizo.

Hakuna ubishi kwamba kumekuwepo na changamoto kwenye malezi kutokana na wazazi wengi kusahau jukumu la ulezi kutokana kujikita zaidi kwenye kutafuta.

Watoto wengi siku hizi, mijini na vijijini, wanalelewa na bibi na babu na wengine wanajilea huku wazazi wakiwa wamekwenda kutafuta maisha ikiwemo kulima mashambani.

Zipo pia habari za wazazi, hususani wa kiume kutekeleza familia na kusababisha hali ngumu katika familia inayochangia mabinti wadogo kurubuniwa kwa pesa kirahisi.

Wazazi wamekuwa pia wazito kufuatilia nyendo za watoto wao, kujua makundi wanayoshirikiana nayo ili kuingilia kati mapema kabla hawajingia kwenye makundi mabaya na vishawishi.

Kukosekana kwa mabweni au shule za kutwa kuwa mbali, imekuwa pia ikichangia tatizo la mimba za utotoni.

Katika muktadha wa kumomonyoka kwa maadili, matumizi ya simu za mkononi ambayo yamerahisisha mawasiliano yasiyofaa na hivyo mipango ya kuwadanganya wanafunzi kufanywa kwa simu inatajwa pia kuwa sababu.

Kwa mujibu wa takwimu za 2020 za Shirika la Afya Duniani (WHO), kila mwaka katika maeneo yanayoendelea, wasichana milioni 21 wenye umri kati ya miaka 15-19 hupata ujauzito.

Hayo yote yanatokea katika jamii yetu ambamo sisi tunaishi na tunashuhudia watoto kupata mimba za utotoni ambazo zina madhara lukuki ikiwa ni pamoja na kuharibu ndoto zao za maisha ukiachilia mbali madhara ya kiafya lakini bado jamii inaona hilo haliwahusu bali ni la mtoto na familia yake.

Mawazo hayo si sahihi. Linapokuja suala la mtoto yeyote aliye chini ya miaka 18 jamii nzima inapaswa kumlinda. Tuna wajibu wa kukemea na kuchukua hatua tuonapo kuna mienendo isiyoeleweka kwa watoto.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/603e891d17b5fecd47193ab7899921fc.png

TANESCO ni shirika la huduma lakini pia ni ...

foto
Mwandishi: Ikunda Erick

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi