loader
Dstv Habarileo  Mobile
Wakulima wahimizwa  kulima kahawa kitaalamu

Wakulima wahimizwa kulima kahawa kitaalamu

HALMASHAURI ya Wilaya ya Nyasa kwa kushirikiana na Bodi ya Kahawa Tanzania, imeadhimisha Siku ya Wakulima wa Kahawa yenye lengo la kutoa elimu kwa wakulima wa kahawa na kuhamasisha wakulima kulima zao hilo kitaalamu.

Maadhimisho hayo yalifanyika Agosti 14, mwaka huu katika shamba darasa la kahawa la Kikundi cha Pisi, katika Kijiji cha Kingerikiti, Kata ya Kingerikiti, wilayani Nyasa.

Mgeni rasmi alikuwa Mkuu wa Wilaya ya Nyasa, Laban Thomas aliyewakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbinga, Aziza Mangosongo.

Akifungua maadhimisho ya siku ya kahawa, Mangosongo aliwataka wakulima kuongeza ukubwa wa mashamba yao na kupanda mbegu aina ya compact ambayo ni mpya, inavumilia ukame na inatoa mavuno bora na kuongeza kipato kwa wakulima na halmashauri kwa ujumla.

Aliongeza kuwa kahawa ni zao la biashara la kimkakati la serikali ambalo linatakiwa uzalishaji wake uhamasishwe na wakulima wote waweze kuhamasika na kulima kwa kufuata kanuni bora za zao hilo kuanzia upandaji hadi uvunaji wake uweze kuongeza tija na uzalishaji wa kahawa bora.

Alitoa wito kwa wawekezaji katika kilimo cha kahawa katika Wilaya ya Nyasa kwa kuwa kuna eneo kubwa la uwekezaji kwa zao hilo.

Alisema katika Tarafa ya Mpepo, kuna hekta 2,169 ambazo hazijawahi kulimwa hivyo ni fursa kwa wawekezaji. Akitoa taarifa fupi ya lengo la siku ya kilimo cha kahawa, Kaimu Meneja wa Bodi ya Kahawa Mkoa wa Ruvuma, Rashid Rashid, alisema lengo wakulima kupata elimu juu ya uzalishaji bora wa zao hilo.

Alisema walifundishwa kwa vitendo tangu kuandaa shamba, kupanda, kutunza mpaka kuvuna na kisha watatoa elimu kwa wakulima wenzao ambao hawajawahi kushiriki.

Rashid alitaja mafanikio yaliyopatikana katika kilimo cha kahawa wilayani Nyasa kuwa ni pamoja na kuongezeka kwa wakulima wa kahawa, upandaji wa mbegu bora aina ya compact ambayo imeongeza uzalishaji na kwamba Chama cha Msingi Kingerikiti Amcos, kimeanza kukaanga na kuuza kahawa yake.

Wilaya ya Nyasa ni mzalishaji mkubwa wa kahawa na zao hilo huchangia asilimia 80 ya mapato ya ndani ya halmashauri. Alihamasisha wananchi wa Tarafa ya Mpepo kuongeza uzalishaji wa zao hilo.

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi