loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kilimo kuongezwa tija 

Kilimo kuongezwa tija 

WAZIRI wa Kilimo, Profesa Adolf Mkenda amesema ni jambo la kawaida kupungua kwa mchango wa kilimo kwenye Pato la Taifa kadiri nchi inavyoendelea.

Hivi karibuni, Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Dk Albina Chuwa alisema takwimu za uchumi zinaonesha mchango wa shughuli za kilimo katika Pato la Taifa uliongezeka hadi asilimia 26.9 mwaka jana ikilinganishwa na asilimia 26.6 mwaka 2019.

Profesa Mkenda alilieleza HabariLEO kuwa, hata nchi zilizoendelea mchango wa sekta ya kilimo kwenye Pato la Taifa ni takribani asilimia nne.

Alisema jambo ambalo si la kawaida kwa Tanzania ni kwamba, wakati mchango wa kilimo kwenye Pato la Taifa ni mdogo, ilitarajiwa nguvu kazi iliyopo kwenye kilimo ipungue kwa kasi kuliko ilivyo sasa.

Kwa mujibu wa Profesa Mkenda, sekta ya kilimo inajumuisha mazao, mifugo, uvuvi na misitu na kwamba mchango wa mazao kwenye Pato la Taifa nchini ni asilimia 15 na ilitarajiwa nguvu kazi iliyopo kwenye uzalishaji wa mazao nayo iwe chini ya asilimia 15.

“Mchango wa kilimo kwa ujumla wake ni kama asilimia 26, lakini nguvu kazi ni asilimia 58 mpaka 60, maana yake ni kwamba tija kwenye sekta yetu ya kilimo ni ndogo sana,” alisema.

Alisema wizara anayoiongoza ina mkakati wenye kulenga kuinua tija kupitia kampeni inazofanya na kuongeza utafiti.

Profesa Mkenda alisema utafiti walioufanya kupitia Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (Tari) ulionesha namna ya kuongeza tija kwenye pamba kutoka kilo 200 au 300 kwenda kilo 1,000 kwa ekari na kwenye korosho badala ya mti mmoja kwa sasa kuzalisha kilo 10 za korosho, unatakiwa uzalishe kilo 30 kwenda juu.

“Kwa hiyo tunapozungumzia tija ni kwamba tunaweza tukaiona kwenye zao moja na jingine hadi jingine, lakini ukichukua Pato la Taifa na nguvu kazi, unaona nguvu kazi kubwa inachangia kiasi kidogo sana cha Pato la Taifa, kwa hiyo alichosema Dk Albina Chuwa ni sahihi ilitakiwa nguvu kazi kwenye kilimo iongezeke sana kiasi kwamba hatuhitaji nguvu kazi yote iende kwenye kilimo,” alisema Profesa Mkenda.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi wameishauri serikali kuja na mkakati wa kuwa na kilimo chenye tija ili asilimia 20 tu ya Watanzania wabaki kwenye sekta hiyo na waliobaki wafanye shughuli nyingine za kiuchumi.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Profesa Humphrey Moshi alisema idadi kubwa ya Watanzania kuendelea kubaki kwenye kilimo inamaana kilimo nchini bado hakina tija.

Ili kufanya kilimo cha Tanzania kiwe na tija, Profesa Moshi alisema ni vyema serikali ikawasaidia wananchi kujikita kwenye kilimo cha umwagiliaji hata kama vitendea kazi vitaendelea kuwa majembe, bado wanaweza kuongeza tija kwa asilimia 100.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Gabriel Mwang’onda alisema kilimo bado hakina tija kwa sababu kiasi cha mazao kinachovunwa kwa ekari ni kidogo ikilinganishwa na nchi zingine.

Pia alishauri kihimizwe kilimo cha umwagiliaji kinachoendana na matumizi ya zana bora za kilimo, mbegu bora na mbolea na kwa kufanya hivyo, kutakuwa na utegemezi kati ya kilimo na viwanda.

foto
Mwandishi: Na Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi