loader
Dstv Habarileo  Mobile
Simba, Yanga buku 10

Simba, Yanga buku 10

JOTO la miamba ya soka nchini Tanzania maarufu Kariakoo Derby limeanza kushika kasi kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutangaza viingilio ambavyo kiwango cha chini kitakuwa Sh.10,000.

Mtanange huo wa Simba na Yanga wa Ngao ya Jamii, utapigwa kuanzia saa 11:00 jioni ya Jumamosi hii, Septemba 25, 2021, katika dimba la Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Ni mchezo unaoashiria ufunguzi wa msimu wa mashindano wa mwaka 2021/22.

Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF ,Cliford Ndimbo, amesema, maandalizi ya mchezo huo yanakwenda vizuri ikiwemo viwango vitakavyotumika siku hiyo.

Ndimbo amesema, viingilio “havitahusisha VIP A ambayo haitakuwa na tiketi ni kwa mwaliko maalum. Kama kuna watu wanadhani wanaweza kualikwa wawasiliane na TFF.”

Amesema, VIP B itakuwa Sh. 30,000, VIP C na viti vya rangi ya machungwa Sh.20,000 na viti vya rangi ya blue na kijani Sh.10,000.

Timu hizo zinakwenda kukutana kila mmoja akiwa ametoka kufungwa michezo yao waliyocheza juzi Jumapili, tarehe 19 Septemba 2021.

Mabingwa watetezi wa ligi kuu 2020/21, Simba ilifungwa 1-0 na TP Mazembe, kwenye kilele cha tamasha la Simba Day, Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Kaimu Ofisa Habari wa Simba, Ezekiel Kamwaga, amesema, baada ya tamasha hilo, wachezaji walipewa mapumziko ya siku mbili na leo Jumanne, wameingia kambini.

“Simba iko tayari. Mara baada ya tamasha la Jumapili, tulipumzika siku mbili na leo timu imeingia kambini na iko salama. Haina majeruhi yoyote. Tumepata mechi za vipimo vya kutosha na hatuna presha kwenye hiyo mechi,” amesema Kamwaga

Watani zao Yanga walikubali kipigo cha 1-0 kutoka kwa Rivers United nchini Nigeria, kwenye mchezo wa marudiano wa Klabu Bingwa Afrika.

Kilikuwa kipicho cha pili kutoka kwa timu hiyo, kikitanguliwa na cha 1-0, Uwanja wa Mkapa na kuwatoa kwenye michuano hiyo.

Hassan Bumbuli, Ofisa Habari wa Yanga amesema, tayari kikosi cha timu hiyo kimerejea salama na kinaendelea na maandalizi “kwani ratiba ya huu mchezo tulikuwa tunaijua na wala hatuna presha.”

“Tunaingia katika mchezo huu dhidi ya Simba tukiwa na kikosi imara, kinaendelea kuimarika siku hadi siku na wale ambao mlikuwa mnawasikia sikia, nao watakuwepo. Sisi tupo imara sana,” amesema Bumbuli.

Bumbuli na Kamwaga wamewaomba mashabiki zao kujitokeza kwa wingi siku hiyo kushuhudia kandanda safi huku kila mmoja akijinasibu kuibuka mshindi katika mchezo huo.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi