loader
Dstv Habarileo  Mobile
Majaliwa ataja fursa kituo cha mabasi kinachojengwa Moshi

Majaliwa ataja fursa kituo cha mabasi kinachojengwa Moshi

WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameweka jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa kituo cha kisasa cha mabasi katika eneo la Ngangamfumuni, Halmashauri ya Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro.

Alisema mradi huo ni wa kimkakati kwani Mkoa wa Kilimanjaro upo mpakani hivyo uwepo wa kituo cha mabasi cha kisasa utatoa fursa kwa wakazi kufanya biashara kwa kuwa utapokea mabasi kutoka nchi za jirani.

Majaliwa alisema hayo juzi wakati akizungumza na wananchi wa Halmashauri ya Manispaa Moshi baada ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa kituo hicho akiwa katika ziara ya kikazi ya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa na serikali katika mkoa huo.

“Hiki ni kituo cha mabasi chenye hadhi ya kimataifa, mkoa huu unapokea watalii wengi kutoka katika maeneo mbalimbali, hivyo ujenzi wa hoteli katika kituo hiki utasaidia kuongeza fursa za biashara kwa wakazi wa hapa,” alisema.

Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi, Rashidi Gembe, alisema mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 28.86 unatekelezwa kwa awamu na kuwa awamu ya kwanza itahusisha ujenzi wa jengo la abiria lenye ukubwa wa meta 13,979 ikijumuisha sakafu ya chini ya ardhi na ghorofa mbili kwa gharama ya Sh bilioni 17.9.

“Awamu ya pili itahusisha ujenzi wa jengo la hoteli lenye ghorofa nne kwa gharama ya Sh bilioni 11.40. Mradi huo utakapokamilika unatarajiwa kuiongezea halmashauri wastani wa mapato ya Sh bilioni 2.72 kwa mwaka kutokana na makusanyo ya ushuru na kodi zitakazokusanywa,” alisema.

Baada ya kuweka jiwe la msingi katika kituo hicho, Majaliwa alikagua na kuweka jiwe la msingi katika mradi wa maji wa Tella Mande uliopo Moshi vijijini ikiwa ni sehemu ya mkakati wa Rais Samia Suluhu Hassan wa kufikisha huduma ya maji vijijini.

Akizungumza na wananchi hao, Majaliwa aliwataka wakazi hao wahakikishe wanaulinda ili uendelee kuwapa uhakika wa upatikanaji wa maji wakati wote pamoja na kuendelea kutunza vyanzo vyote vya maji.

Akizungumza na wakazi wa Himo, Waziri Mkuu alisema kuwa Rais Samia amedhamiria kuwekeza katika elimu ya mtoto wa kike ili waweze kutimiza ndoto zao.

“Vijana nawapa tahadhari, ukijulikana umempa mtoto wa kike mimba, sheria kali zitachukuliwa dhidi yako,” alisema

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi