loader
Dstv Habarileo  Mobile
FISTON  MAYELE Aihofia Simba  licha ya kuifunga

FISTON MAYELE Aihofia Simba licha ya kuifunga

FISTON Mayele mshambuliaji wa mpya wa klabu ya Yanga, ambaye siku za karibuni jina lake limekuwa maarufu baada ya bao aliloifunga Simba katika mchezo wa Ngao ya Jamii.

Mshambuliaji huyo aliyepata umaarufu mkubwa akiwa na timu ya nyumbani kwao Congo AS Vita, ambayo aliichezea kwa mafanikio na kumfanya ajulikane na kuzivutia timu nyingi, ikiwemo Yanga ambayo ndio anaitumikia hivi sasa.

Hivi sasa mashabiki wa Yanga wamemsahau Makambo ambaye ndiye walikuwa wakimuimba kila siku na kiti cha ufalme amekikalia Mayele ambaye mashabiki wa Simba hawapendi kusikia ukimtaja mbele yao kutokana na kile alichowafanya pale kwa Mkapa Septemba 25, 2021.

Gazeti hili limefanya mazungumzo na mshambuliaji huyo mwenye matarajio makubwa ya kurudisha ufalme wa Yanga akishirikiana na wachezaji wenzake naye hakusita kueleza mengi akiwa na kikosi hicho kinacho pambana kurudi kwenye ubora wake.

KUSAJILI YANGA

Mshambuliaji huyo anasema moja ya sababu kubwa iliyomfanya asaini Yanga ni uwepo wa rafiki zake wawili kwenye kikosi cha Yanga, ambao ni Tuisila Kisinda na Tomombe Mukoko, lakini pia alivutiwa na upinzani wa Simba na Yanga na alitamani siku moja kuwa upande mmoja kati timu hizo mbili.

Anasema ilipomfikia ofa ya Yanga hakujiuliza mara mbili sababu, kwanza mkataba wake ulibakiza muda mfupi kumalizika, lakini kingine kilichomfanya asijiulize ni baada ya kubaini hata mchezaji mwenzake mwandamizi wa AS Vita Djuma Shabani naye alishamalizana na Yanga.

“Dhamira yangu ilikuwa ni kubadilisha mazingira sababu nimecheza nyumbani tangu naanza soka la ushindani, lakini ushindani wa Simba na Yanga nilivutiwa nao sana ndio maana nilishangilia sana nilipofunga bao kwenye mechi ya Ngao ya Jamii sababu Simba najua Simba ni timu kubwa,” anasema.

KUSHINDANIA NAMBA

Mayele anasema ingawa ndoto zake za kujiunga na Yanga zimetimia, lakini moja ya kitu kinampa presha kubwa ni nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza sababu timu hiyo inawashambuliaji saba, na wote wana uwezo mkubwa katika ufungaji.

Anasema wakati anawasili nchini kuanza maandalizi aliona namna mashabiki wa Yanga wanavyomkubali Makambo, jambo ambalo lilimzidisha hofu na kuongeza presha, akihofu kwamba na yeye ataweza kuweka kumbukumbu kama aliyoiacha mwenzake kabla hajaondoka kwenye Guinea?

“Nafurahi kwa mechi chache nilizocheza naamini kuna kitu nimekionesha na mashabiki wameanza kunielewa matarajio yangu ni kufunga mabao mengi zaidi siyo kwenye mechi na Simba, bali kila timu ambayo tutacheza nayo iwe ya ndani au nje ya Tanzania,” anasema Mayele.

“Malengo yangu mwisho wa msimu nataka niwe mfungaji bora wa ligi najua haitokuwa rahisi kutokana na ushindani uliopo ndani ya timu na ligi kwa ujumla, lakini mimi na wenzangu tumejipanga kupambana ili kutimiza kile tulicho kikusudia, ambacho ni kubeba mataji yote ya ndani,” anasema Mayele.

LIGI YA TANZANIA

Mshambuliaji huyo anasema kwa namna alivyo shuhudia mechi kadhaa za Ligi Kuu Tanzania Bara amebaini kuwa ushindani upo ingawa siyo mkubwa sana kama ilivyo kwao Congo na hiyo inatokana na wachezaji wengi kuandaliwa vizuri.

Mayele anasema alichokiona yeye kwa siku chache ushindani wa ligi ya Tanzania ni wa timu chache ambazo ni Yanga, Simba, Azam na baadhi ya timu chache ambazo zina afadhali kiuchumi tofauti na kwao Congo, ambako timu nyingi zina uwezo wa kifedha na ndio maana ushindani ni mkubwa.

“Kule Congo ingawa TP Mazembe na AS Vita ndio zinaonekana kufanya vizuri na zinajulikana sana, lakini timu nyingi zipo vizuri na zinatoa ushindani wa hali ya juu ispokuwa kuyumba kiuchumi ndio kumesababisha baadhi ya timu kama FC Lupopo, Maniema FC, DC Motema Pembe kupotea kwenye ushindani,” anasema Mayele.

ANAIHOFIA SIMBA

Straika huyo anasema Simba ndio timu ambayo inampa hofu kwenye ligi ya Tanzania, hiyo ni kutokana na ubora wachezaji wake kukaa pamoja kwa muda mrefu na uzoefu waliokuwa nao baada ya kushiriki mara kwa mara kwenye mashindano ya kimataifa.

Anasema ingawa msimu huu anaiona kama imeshuka kiwango, lakini hiyo haipaswi kuwa sababu ya kufanya timu nyingine waidharau sababu inaundwa na wachezaji wazuri tena wenye faida ya kucheza mechi za kimataifa na timu kubwa Afrika.

AMAKUBALI FEI TOTO

Siyo kitu chakawaida kwa mchezaji wakigeni kukubali uwezo wa mchezaji wa taifa jingine wakati ndani ya timu hiyo wapo wachezaji kutoka taifa lake kwa Mayele hilo limekuwa tofauti baada ya kumtaja Feisal Salum ‘FeiToto kuwa anavutiwa na kipaji chake.

Anasema kwa muda mfupi tangu amjue amejifunza mambo mengi kutoka kwake na hadhani kama klabu ya Yanga itaendelea kummiliki endapo ataendelea kucheza kwa ubora wake mpaka mwisho wa mkataba wake.

“Feisal ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa mno cha mpira, nilianza kupata sifa zake kutoka kwa Kisinda, sidhani kama siku zijazo tutakuwa naye kutokana na uwezo na utulivu wake awapo ndani na nje ya uwanja,” anasema Mayele.

KUTOLEWA LIGI YA MABINGWA

Mayele ni miongoni mwa wachezaji watatu waYanga ambao hawakuichezea timu hiyo kwenye mechi mbili za Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na vibali vyao vya kimataifa (ITC) kutokamila.

Anasema hilo limemyima raha sababu alipanga kuanza kuuwasha moto kwenye mechi hizo, lakini hawezi kuendelea kulaumu sababu tayari imeshatokea.

“Rivers United hawakuwa wazuri ila walitukuta bado hatujakaa sawa na baadhi ya wachezaji hawakucheza sababu ya vibali vya kazi ukweli nilipania kufanya mambo makubwa, lakini haikuwa bahati tunajipanga kuhakikisha msimu ujao tunakuwepo,” anasema Mayele

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/af306911f64f3aca7fca04eccdd05714.jpg

TIMU ya Taifa ya Soka la Watu wenye ...

foto
Mwandishi: Mohamed Akida

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi