loader
Dstv Habarileo  Mobile
Kudumisha Urafiki na Kukuza Ushirikiano kati ya China na Afrika katika Mazingira Mapya

Kudumisha Urafiki na Kukuza Ushirikiano kati ya China na Afrika katika Mazingira Mapya

Kama ishara ya matumaini kwamba Ulimwengu sasa uko tayari kurudi katika hali ya kawaida baada ya kuweko na vizuizi katika safari za kimataifa kutokana na gonjwa la UVIKO-19, Wakuu kadhaa wa Nchi na Serikali hatimaye waliweza kukusanyika katika Jiji la New York, Marekani kuanzia tarehe 20 hadi 28 Septemba 2021 kuhudhuria mkutano muhimu wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, maarufu kama UNGA. Jambo moja la kipekee katika mkutano wa mwaka huu lilikuwa kumshuhudia Rais Samia Suluhu Hassan wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania akiweka historia kwa kuwa Rais wa kwanza wa nchi yake kuhudhuria mkutano huo.

Vilevile, historia inaonesha yeye anakuwa mmoja wa Marais watano pekee wanawake kuwahi kuhutubia katika Mkutano huo mkubwa. Kwa kutambua namna nafasi hiyo ya juu ya uongozi aliyonayo inatoa mwanga wa matumaini na fursa ya kupigiwa mfano na wanawake na wasichana wadogo duniani kote wenye matamanio ya kuwa viongozi wakubwa, Rais Samia alitumia vizuri fursa hiyo ya kusikilizwa na Viongozi wa Dunia kugusia umuhimu wa Serikali kote duniani kuimarisha mifumo inayotoa fursa za usawa wa kijinsia.

Lakini la muhimu zaidi katika hotuba yake, aliuhakikishia ulimwengu kuhusu kutobadilika kwa msimamo wa kihistoria wa Tanzania wa kutambua na kuthamini mifumo na ushirikiano wa kimataifa katika kushughulikia changamoto mbalimbali zinazoibuka kila siku ulimwenguni.

Kwa hakika, Mkutano huo wa UNGA umekuwa na historia ya muda mrefu ya kutumika kama jukwaa la kuwasilisha, kujadili na kupitisha maamuzi makubwa ya kimataifa yanayolenga kudumisha maslahi ya nchi wanachama. Ukweli huo ulithibitishwa pale Rais Xi Jinping wa China alipogusia katika hotuba yake katika Mkutano huo wa 75 wa UNGA namna miaka 50 iliyopita, mwaka 1971 katika Mkutano wa 26 wa UNGA, nchi ya Jamhuri ya Watu wa China iliweza kurejesha haki zake zote kamili za kuwa mwakilishi pekee wa China katika Umoja wa Mataifa kwa kusaidiwa wa idadi kubwa ya nchi zinazoendelea kutoka bara la Afrika, Asia na Amerika Kusini.

Tukio hilo litakumbukwa vyema na nchi 54 za Kiafrika, ambazo ni asilimia 28 ya ncho zote wanachama wa Umoja wa Mataifa, kwani kwa kipindi hicho liliashiria ushindi mwingine wa nchi zinazoendelea d hidi ya mfumo wa kinyonyaji wa kimataifa mara baada ya nchi nyingi kupata uhuru dhidi ya ukoloni katika miaka ya 1960.

Kwa nchi ya Tanzania, tukio hilo litabakia katika historia yake na mahusiano na China kwani lilifanikiwa kwa kiasi kikubwa kufuatia mchango wa ushawishi na kampeni zilizofanywa na aliyekuwa Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Dkt. Salim Ahmed Salim, ambaye baadaye alikuja kuwa Waziri Mkuu na Makamu wa Rais kati ya Mwaka 1984 hadi 1990. Upo usemi usemao akufaaye kwa dhiki, ndiye rafiki wa kweli.

Kitendo kicho cha Afrika na Tanzania kuisaidia China kurejea katika Umoja wa Mataifa, pamoja na matukio mengine mengi ya baadaye ya ushirikiano baina ya pande hizo mbili katika Nyanja za kimataifa, kimechangia kwa kiasi kikubwa sana katika kuimarisha mahusiano kati ya Afrika na China.

Jambo hilo linadhihirishwa na namna china inavyokuwa mstari wa mbele kuisemea Afrika na nchi nyingine zinazoendelea ikiwemo kuzitaka nchi zilizoendelea kutoa nafasi kwa bara la Afrika kushirikishwa kikamilifu katika majukwaa ya maamuzi ya kimataifa kama vile Baraza la Kudumu la Umoja wa Mataifa na Kundi la Nchi 20 Matajiri Duniani (G20).

Miongo kadhaa baadaye, Nchi za Afrika na China zimepitia katika mabadiliko mbalimbali kisiasa, kiuchumi na kijamii. Kwa kuzingatia hilo, ni dhahiri kuwa ipo haja ya pande zote mbili kupitia upya namna na aina ya muhusiano yao kwa kuzingatia misingi imara iliyowekwa miaka ya nyuma.

Kwa sasa, mahusiano baina ya pande hizo mbili yanaendelea kukua chini ya Jukwaa la Ushirikiano kati ya China na Afrika (FOCAC) ambalo tangu kuanzishwa kwake mwaka 2000, limekuwa jukwaa muhimu la kuzikutanisha nchi za Kiafrika na China kujadiliana masuala muhimu ya uhusiano baina yao. Kama ishara ya mahusiano mazuri, mwezi Januari Mwaka huu, Mjumbe wa Baraza la Kuu la Utawala la China ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo, Wang Yi, alitembelea Tanzania ambapo, pamoja na mambo mengine, alitumia ziara hiyo kutoa tathmini ya utekelezaji wa maeneo makuu nane ya ushirikiano kati ya China na Afrika yaliyokubaliwa katika Mkutano Mkuu wa FOCAC wa Mwaka 2018. Alieleza kuwa hadi kufikia mwanzoni mwa mwaka 2021 utekelezaji wa maeneo hayo ulishafikia zaidi ya asilimia 70 katika maeneo ya kukuza ushirikiano wa viwanda, ujenzi wa miundombinu ya kikanda, uwezeshaji wa biashara, maendeleo ya kijani, mafunzo, huduma za afya, mahusiano baina ya watu pamoja na kudumisha ulinzi na usalama. Japo ya kuwa kidiplomasia ziara za viongozi wa ngazi za juu ni ishara kuwa nchi mbili zimeshibana na zina mahusiano mazuri katika nyanja mbalimbali, bado wachambuzi wataelezea umuhimu wa nchi husika kuwa na nia na mbinu endelevu za kudumisha na kukuza mahusiano yao katika mazingira mapya yanayojitokeza ili kuhakikisha matokeo chanya ya mahusiano hayo.

Kwa mfano, mbali na kubadilisha uongozi wa juu zaidi, mapema mwaka huu Tanzania ilizindua Mpango wa Tatu wa Maendeleo wa Miaka Mitano 2021/22 - 2025/26, ambao, pamoja na mambo mengine, umejikita katika kutekeleza miradi 17 ya kipaumbele – ikiwemo miradi miwili mikubwa ya kielelezo ya Bwawa la Umeme wa Maji la Julius Nyerere pamoja na Reli ya Kisasa (SGR). Vipaumbele vingine vya Mpango huo ni pamoja na kuchochea uchumi shindani na jumuishi ili kuhakikisha Tanzania inapanda kutoka nchi ya pato la kati la chini hadi kuwa nchi ya pato la kati la juu.

Kwa kuzingatia gharama kubwa za kutekeleza Mpango huo wa Maendeleo zinazokadiriwa kufikia shilingi 114.8 trilioni, ni dhahiri kuwa eneo bayana la ushirikano wa kifedha baina ya China na Tanzania linapaswa kupewa kipaumbele katika ajenda za ushirikiano, angalau kwa kipindi kati ya sasa na mwaka 2026.

Zaidi ya hapo, hivi karibuni Tanzania pia imeridhia na hatimaye kujiunga katika Mkataba wa Eneo Huru la Biashara Afrika (AfCFTA) ambalo linatoa fursa ya soko kubwa la pamoja lenye zaidi ya watu bilioni 1.2. Kujiunga huko kwa Tanzania ni ishara nyingine kuwa inathamini mahusiano ya kimataifa, hususani kujumuika na nchi nyingine wanachama wa Umoja wa Afrika (AU) kurekebisha mfumo usio haki wa kiuchumi na kibiashara wa kimataifa kupitia AfCFTA.

Ukubwa wa soko la AfCFTA ni fursa kubwa kwa nchi za Afrika na China pia. Hata hivyo, wapo wachambuzi wanaoona utekelezaji wa AfCFTA unaweza pia kutoa changamoto ya mahusiano ya kiuchumi na kibiashara kati ya Afrika na China.

Hii ni kuzingatia ukweli kwamba kimsingi Mkataba huo, pamoja na mambo mengine, unalenga kuibua na kukuza mahusiano mapya ya kibiashara baina ya nchi za Afrika ili hatimaye ziondokane na utaratibu wa kusafirisha malighafi nje na kuagiza bidhaa za viwandani kutoka kote duniani. China ni mbia mkubwa zaidi wa kibiashara wa Afrika.

Aidha, ni dhahiri kuwa uwiano wa kibiashara baina ya pande hizo mbili bado unainufaisha zaidi China. Kwa mfano, kwa sasa kuna takribani raia 20,000 wa China wanaoishi na kufanya biashara hapa nchini, huku thamani ya biashara baina ya nchi hizo ikifikia Dola za Kimarekani 3.9 bilioni.

Thamani ya bidhaa zinazopelekwa China kutoka Tanzania ni Dola za Kimarekani 238 milioni ikilinganishwa na thamani ya bidhaa zinazoingizwa nchini kutoka China zenye thamani ya Dola za Kimarekani 2.1 bilioni. Kwa kuzingatia ukweli kwamba Tanzania, kama ilivyo kwa nyingine nyingi za Afrika zilizo Kusini mwa Jangwa la Sahara, bado inategemea kwa kiasi kikubwa mauzo ya nje ya bidhaa za kilimo, mifugo na uvuvi.

Njia mojawapo ya haraka ya kufidia pengo hilo kubwa la kibiashara inaweza kuwa ni kwa China kuongeza katika orodha wa bidhaa nyingi zaidi zinazoruhusiwa kuingizwa nchini humo kutokea Tanzania. Kwa mfano, hadi sasa nyama na bidhaa za nyama kutoka Tanzania haziruhusiwi kuingizwa nchini China. Mwaka huu ni wa kihistoria kwa nchi ya China kwani si tu kuwa Chama chake tawala cha Kikomunisti (CPC) kinatimiza miaka 100 tangu kuanzishwa kwake, bali pia inatimiza miaka 50 tangu kurejea Umoja wa Mataifa kama Taifa huru.

Kwa miongo kadhaa sasa China imeudhihirishia ulimwenu kuwa ni nchi yenye mchango mkubwa katika maendeleo ya dunia na muumini mzuri wa mfumo na ushirikiano wa kimataifa. Hivyo, kwa kipindi hiki ambapo ulimwengu unakabiliwa na changamoto kubwa za aina mbalimbali, hususani kukosekana kwa uwiano wa kiuchumi duniani, basi ni wakati mzuri kwa Tanzania na nchi nyingine za Kiafrika kufanya kazi kwa karibu zaidi na China ili kutafsiri mahusiano mazuri ya kihistoria baina ya pande hizo mbili kuwa mahusiano yenye faida zaidi ya kiuchumi na kibiashara..

Hatua hiyo ni muhimu kwani itakuwa ni sehemu ya kuitikia wito wa kimataifa wa kijenga ulimwengu wa usawa wenye mustakabali mmoja. Kwa kuhitimisha, yapo mapendekezo kadhaa yanayoweza kuzingatiwa katika mchakato wa kudumisha mahusiano baina ya China na nchi za Afrika.

Hizi ni pamoja na China kuendelea kutumia nafasi yake ya ushawishi kimataifa kuisemea Afrika na kuhakikisha inashirikishwa katika nafasi za maamuzi katika masuala makubwa ya kimataifa, ikiwemo kwa mfano suala la upatikanaji wa dozi za kutosha za chanjo kwa nchi za Afrika – ikiwemo uwezekano wa kufungua kiwanda cha kutengeneza chanjo hizo barani Afrika; China kuongeza ufadhili kwa Afrika kupitia Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) na Benki ya Mitaji ya Afrika (Afrexim Bank) ili kusaidia ukuzaji wa viwanda, maendeleo ya miundombinu ya kikanda, kuongeza uzalishaji wa ajira miongoni mwa sekta binafsi pamoja na kutekeleza ajenda ya Mkataba wa AfCFTA; na kuongeza ushirikiano wa kidijitali ili kuiwezesha Afrika kunufaika na uzoefu na uwezo wa kiteknolojia ya China.

Mwisho, tunapotafakari masuala hayo machache hapo juu, nichukue fursa hii kuungana na wapenda amani wote duniani kuwatakia Wananchi wote wa China Heri ya Siku ya Uhuru, tarehe 1 Oktoba.

Mwandishi ni Waziri Mkuu Mstaafu wa Tanzania na Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi, Chama cha Kukuza Urafiki kati ya Tanzania na China.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/e0c36de3590671feca689cfea8e674d9.jpg

MAZAO mengi ya chakula, matunda na biashara kama ...

foto
Mwandishi: Mizengo Pinda

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi