loader
Majaliwa awataka    mabalozi wakuze uchumi  

Majaliwa awataka   mabalozi wakuze uchumi  

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ameagiza mabalozi wa Tanzania nje ya nchi waimarishe biashara na nchi wanapokwenda kwani wana jukumu la kukuza uchumi wa nchi kupitia diplomasia ya uchumi.

Amewataka mabalozi hao watangulize maslahi ya taifa katika utekelezaji wa majukumu yao.

Waziri Mkuu alitoa maelekezo hayo jana ofisini kwake Mlimwa, jijini Dodoma wakati alipokutana na mabalozi saba wanaokwenda kuiwakilisha Tanzania katika nchi za Uturuki, Sweden, Rwanda, India, Ethiopia, Uswisi na Jamhuri ya Korea.

Mabalozi hao na nchi zao kwenye mabano ni Luteni Jenerali Yacoub Mohamed (Uturuki), Grace Olotu (Sweden), Meja Jenerali Richard Makanzo (Rwanda), Anisa Mbega (India), Innocent Shiyo (Ethiopia), Hoyce Temu (Uswisi) na Togolani Mavura (Jamhuri ya Korea).

 "Waheshimiwa mabalozi mna jukumu kubwa la kukuza uchumi wetu. Nendeni mkaimarishe biashara na nchi yetu. Muangalie sisi tumefanya nini na tumepungua wapi na je tunaweza kurekebisha vipi," alisema Majaliwa.

 Alisema ili Tanzania ipae zaidi kiuchumi, inapaswa kukuza sekta ya viwanda iweze kuuza  bidhaa zilizosindikwa.

"Mnalo jukumu la kuangalia ni namna gani tunaweza kuongeza uzalishaji na siyo wa mazao ghafi bali yaliyosindikwa. Tunataka tuuze kahawa iliyosindikwa hadi mwisho na kama ni korosho tuuze zilizobanguliwa,"alisema Majaliwa na kuongeza: 

"Tanzania tunataka tuimarishe uchumi wetu wa viwanda. Kuna watu wanadai viwanda vingi vilivyokuwapo zamani vimekufa lakini wanasahau kwamba teknolojia imebadilika sana. Kwa hiyo leteni watu kwenye uwekezaji wa viwanda, cha msingi wawe ni wale ambao wana historia nzuri kwenye nchi zao."

 

Alisema Tanzania imedhamiria kufufua mazao ya mkonge, michikichi na mbegu za mafuta na akawataka watafute wawekezaji makini watakaokuja kuwekeza kwenye mazao hayo.

 "Sambamba na hilo, muangalie uwezekano wa kupata masoko ya mazao yanayozalishwa nchini. Mnapaswa muwe ni kiungo baina ya nchi yetu na hizo nchi mnazoenda kutuwakilisha. Muangalie sisi tuna mazao au bidhaa gani na wao wanaweza kuagiza kiasi gani kutoka hapa nchini," alisema Majaliwa.  

Aidha, aliwataka waangalie ni namna gani wanaweza kuinua sekta nyingine kama vile utalii kwa kuitangaza Tanzania waendako ili kuvutia watalii wengi zaidi kuja nchini.

"Tanzania tuna fukwe nzuri sana kule Zanzibar na kuanzia Tanga hadi Mtwara. Himizeni wawekezaji wa kujenga hoteli kwenye hizi fukwe ili watalii wakija wakute wanazozihitaji," alisema Majaliwa.

 Kuhusu Wanadiaspora, Waziri Mkuu aliwataka mabalozi wawatambue walioko huko waendako, watambue biashara na kazi zao na wawashawishi wafungue matawi ya kampuni zao Tanzania.

"Pia angalieni fursa za masomo katika nchi mnazoenda ili Watanzania wapate fursa za mafunzo ya kitaalamu huko nje. Kumbukeni kuwa lugha yetu ya Kiswahili ina fursa nyingi za ajira kwa Watanzania, hivyo msiache kukitangaza katika nchi zenu," alisema Majaliwa.

Aliwataka mabalozi hao waende wakaripoti kwenye vituo vyao vya kazi kwani tayari wana maelekezo ya viongozi wakuu wa serikali.

"Mmeshapata maelekezo ya Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Mheshimiwa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na hayo ndiyo maelekezo muhimu. Nendeni vituoni, muda umeisha. Huu siyo muda wa kwenda kuaga mawaziri. Wako wengi sana. Naamini baada ya kuonana na viongozi wetu wakuu, sasa mko imara," alisema Majaliwa

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/65507a09f9476d807b0499140c2d6d3f.jpg

RAIS Samia Suluhu Hassan amehutubia taifa ...

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi