loader
Majaliwa aagiza mambo 12 kuwezesha wananchi

Majaliwa aagiza mambo 12 kuwezesha wananchi

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa ametoa maagizo 12 kwa viongozi wa wizara, mikoa, taasisi za umma na binafsi ikiwamo ya kuangalia namna ya kupunguza riba inayotozwa kwenye mitaji kwa lengo la kufanya gharama ndogo za upatikanaji wa huduma za fedha.

Ameyasema hayo jana jijini hapa wakati wa kufungua Kongamano la Tano la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi.

Majaliwa alisema Wizara ya Fedha na Mipango na taasisi za fedha zinatakiwa kuhakikisha huduma za fedha zinasogezwa maeneo ya pembezoni ya miji na vijijini.

Pia ameziagiza kuangalia namna ya kupunguza riba inayotozwa kwenye mitaji kwa lengo la kufanya gharama ndogo za upatikanaji wa huduma za fedha na kuchochea shughuli za kiuchumi.

Ameitaka mikoa kuanzisha vituo vya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ambavyo vitatoa huduma za mikopo, mafunzo, urasimishaji wa shughuli za kiuchumi, upatikanaji wa taarifa mbalimbali zikiwemo za masoko na kutoa ithibati ya bidhaa zinazozalishwa.

“Taasisi za umma na binafsi zinazosimamia mifuko na programu za uwezeshaji zinazotoa mitaji na ruzuku zihakikishe kuwa zinaweka watumishi kwenye vituo vya uwezeshaji wa wananchi kiuchumi ili uwepo wa vituo hivyo uwe na maana kwa wananchi wanaokwenda kupata huduma na ziimarishe huduma ili kuwezesha ustawi na kukua kwa uchumi wa wananchi hasa wanaoishi maeneo ya pembezoni kwa lengo la kupunguza umaskini na kuchochea shughuli za kiuchumi,” alisema Majaliwa.

Pia Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Sekretarieti za Mikoa ziendelee kuhamasisha uanzishwaji na uendelezaji wa vikundi vya kifedha vya kijamii kwa kuwa vina mchango mkubwa katika kujenga uchumi jumuishi.

“Mikoa pia isimamie uimarishwaji wa majukwaa ya wanawake kwenye mikoa kama ilivyoelekezwa na Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan, alipokutana na wanawake jijini Dodoma Juni 8, mwaka huu,” alisema.

Pia ameagiza wizara za kisekta za kiuchumi kuimarisha na kuboresha huduma muhimu ikiwemo barabara, reli, bandari, umeme, mawasiliano, miundombinu ya kilimo, ya ufugaji na uvuvi ili kukuza uchumi hasa maeneo ya pembezoni ya miji na vijijini kwa lengo la kukuza ajira na kipato kwa mtu mmoja mmoja na Taifa kwa ujumla.

Aidha, Majaliwa ameziagiza halmashauri zote nchini kuhakikishe afua za uwezeshaji wananchi zinatengewa bajeti na kuwajengea uwezo maofisa biashara ili waratibu kwa ufanisi masuala ya uwezeshaji katika halmashauri zao.

“Pia halmashauri zote nchini ziweke mazingira wezeshi kwa wafanyabiashara na wajasiriamali wadogo sana, wadogo na wa kati kukua na kustawi ili kufanya shughuli za kiuchumi kwa kuendelea kutenga maeneo maalumu kwa ajili ya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu ili waweze kujishughulisha na uzalishaji mali na biashara,” alisema.

Amesisitiza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia imedhamiria kutekeleza dhana ya uchumi jumuishi kwa vitendo kwa kuweka vipaumbele vitakavyowawezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za kiuchumi.

Alitaja baadhi ya vipaumbele kuwa ni pamoja na uimarishaji wa huduma za afya, hifadhi ya jamii, maji, umeme na utekelezaji wa mpango wa elimumsingi bila ada Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amezindua Kanzidata ya Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi yenye lengo la kuwaunganisha watoa huduma wa Kitanzania na wawekezaji pamoja na taasisi mbalimbali za uwezeshaji.

“Ni matarajio yangu kwamba kanzidata hii itaongeza ushiriki wa Watanzania kwa kuwa itawawezesha kujulikana, kufahamu fursa kwenye miradi mbalimbali na kutambua wadau ambao 

wanaweza kushirikiana na kuingia ubia ili kupata fursa mbalimbali kwenye miradi ya kimkakati na uwekezaji unaofanyika hapa nchini.

“Ninaomba nitumie fursa hii, kutoa shukrani za dhati kwa Mheshimiwa Rais Samia kwa dhamiri yake kubwa aliyoonesha katika kukuza uwezeshaji kwa wananchi hasa wanawake, vijana, wafanyabiashara, wajasiriamali na watu wenye ulemavu,” alisema Waziri Mkuu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), Geoffrey Mwambe amewaagiza wakuu wa mikoa wasimamie kikamilifu shughuli za uwezeshaji wananchi kiuchumi ziwe na tija ili kuhakikisha malengo ya Rais Samia yanafikiwa.

Alisema Kongamano la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi lilianzishwa mwaka 2015/2016 ili kuwakutanisha wadau mbalimbali wa uwezeshaji kwa lengo la kujadili na kupeana uzoefu katika kuwawezesha Watanzania.

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/86499e51b7310d1b9642db141a44aad4.jpeg

RAIS Samia Suluhu Hassan amehutubia taifa ...

foto
Mwandishi: Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi