loader
Dstv Habarileo  Mobile
Bil 50/- kujenga bandari ya uvuvi Kilwa

Bil 50/- kujenga bandari ya uvuvi Kilwa

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Sita imetenga Sh bilioni 50 kwa ajili ya ujenzi wa bandari ya uvuvi wilayani Kilwa katika Mkoa wa Lindi.

Majaliwa alisema bandari hiyo itaongeza kasi ya uvuvi wa kisasa na biashara ya samaki ili kuongeza Pato la Taifa na kuboresha maisha ya wananchi.

Alisema hayo jana alipozungumza na watumishi, madiwani na wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa.

Majaliwa alisema mradi huo unatarajia kuchangia ukuaji wa maendeleo kwa wananchi wa Wilaya ya Kilwa na Watanzania kwa ujumla, hivyo akahimiza wananchi wachangamkie fursa hiyo kwa kujenga nyumba za kulala wageni na migahawa kwa kuwa watu wengi watahitaji makazi.

“Wataalamu walishapita katika maeneo yote ya pwani kuanzia pwani ya kutoka Tanga hadi Mtwara na kuridhia kwamba Kilwa ni mahali sahihi kwa ajili ya ujenzi wa bandari hiyo kwani eneo la uwanda wake ni zuri na lina kina kirefu ambacho hakihitaji kuongezwa na Mheshimiwa Rais ameridhia ijengwe,” alisema Majaliwa.

Wakazi wa Halmashauri ya Wilaya ya Kilwa waliishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa kuamua kujenga bandari hiyo kwa kuwa itaimarisha biashara ya samaki na kuongeza ajira.

Wakati huohuo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa zaidi ya Sh bilioni 16 kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji wa miundombinu ya elimu mkoani Lindi. 

Alisema hayo juzi alipozungumza na wananchi, madiwani na wananchi wa Halmashauri ya Mtama mkoani Lindi.

Majaliwa alitoa mwito kwa watumishi kwenye mkoa huo wahakikishe fedha hizo zinatumika katika kazi iliyokusudiwa na atayezitamani zitamuunguza. Alisema watumishi hao wana wajibu wa kuwatumikia Wana-Mtama na kwamba serikali inataka kuona mabadiliko ya kiutendaji katika maeneo yao. 

foto
Mwandishi: Mwandishi Maalumu, Kilwa

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi