loader
Zanzibar isipoteze utamaduni wa kurusha vishada (SPOTILEO)

Zanzibar isipoteze utamaduni wa kurusha vishada (SPOTILEO)

MAZAO mengi ya chakula, matunda na biashara kama karafuu kwa Zanzibar huwa na msimu kama ilivyo hali ya hewa. Hali hii pia huonekana kwa michezo ya watoto Zanzibar. 

Hapo zamani ilikuwa ni kawaida Visiwani kuona kwa kipindi maalumu watoto wanashabikia mchezo wa aina moja katika kila pembe na vichochoro. 

Lakini baada ya muda watoto hao hupendelea mchezo mwingine na ule waliokuwa nao kuwekwa pembeni na kurejewa baada ya wiki au miezi michache.

Hapo zamani miongoni mwa mchezo uliokuwa na msimu ni ule wa kurusha vishada ambao kwa kawaida ulianza siku chache kabla ya kuingia mwezi mtukufu wa Ramadhani na kwenda arijojo mwezi ulipomalizika.

Hali hii siku hizi imetoweka na vishada vya rangi mbalimbali na vingine vikiwa na rangi mchanganyiko ambavyo vilikuwa vikitanda anga ya Zanzibar wakati wa mwezi wa Ramadhani vimetoweka.

Hivi vishada vilikuwa vya aina na ukubwa tofauti, kama tunavyoona kwa mavazi. Hata nyuzi za kurushia huwa za aina mbalimbali.

Kila wakati msimu wa kurusha vishada ulipoingia mafundi cherehani walikuwa na wakati mgumu, kwani walilazimika kuwa macho kulinda vigurudumu vya uzi kwenye cherehani zao.

Hii ilitokana na baadhi ya watoto watundu kuvizia fundi anasinzia au kaondoka mara moja kwenye cherehani na hapo mtoto hufanya haraka kuchomoa kigurudumu cha uzi na kukimbia nacho.

Ninakumbuka wakati ninasoma chuoni na shule walimu siku zote walikuwa wakitueleza ubaya wa kuiba nyuzi kwa mafundi cherehani kwa kutuambia kufanya hivyo ni wizi na tungelikuwa tunapata dhambi kwa kufanya hivyo.
Wazee nao walikuwa na kazi pevu ya kuwakataza watoto wao wasiibe vigurudumu vya uzi kwa mafundi cherehani na badala yake waombe pesa za kununulia uzi wa kurushia vishada uliokuwa ukiuzwa madukani.
 
Eneo ambalo lilisifika kwa kuwa na watengezaji vishada mahiri ni mtaa wa Kundemba, mjini Unguja.
 
Hapo ilibidi mtu aagize kutengezewa kishada na kusubri kwa siku mbili mpaka tatu ndipo apate kishada chake, kama vile unapokwenda kushona nguo kwa fundi cherehani.

Baadhi ya wakati palizuka ugomvi kati ya mtoto (hata mzee) na mtengenzaji vishada. Hii iitokana na fundi kukawisha kukitengeneza kishada wakati fundi ameshalipwa ada yake ya kukitengeza kama tunavyoona siku hizi kwa watu wanaowapelekea mafundi kushona nguo zao, hasa pale inapokaribia wakati wa Siku Kuu.

Ninakumbuka baadhi ya mafundi walitoza ada zaidi ya kutengenza kishada kwa haraka (express).  Kama uliambiwa usubiri kwa siku tatu ilikubidi ulipe ada ya mara mbili ili upate kishada chako siku hiyo hiyo, kama tunavyoona siku hizi kwa washoni na wanaofua nguo.

Lakini sio Kundemba ya leo ambayo kwa bahati mbaya baadhi ya vijana wameiharibu sifa ya mtaa huu na saa kueleweka kama moja ya eneo lenye vijana wengi wanaotumia dawa za kulevya.

Katika miaka ya nyuma karibu kila kijana wa kiume wa eneo hili alijua kutengeneza kishada, lakini leo sio tu hawajui kukitengeneza, bali hata ustadi wake wa kukirusha.

Hapo zamani mji wa Unguja ulikuwa na maduka mengi yaliokuwa yakiuza karatasi nyepesi za kutengenzea vishada, lakini karatasi hizi zilizokuwa zikitoka India zimepotea kabisa na vijana wengi wa leo hawajawahi kuviona. 

Kwa hakika inasikitisha kuona utamaduni wa kutengeneza na kurusha vishada ambao uliwaepusha watoto na vijiwe vya kuwaingiza katika mambo maovu unaoekana kupotea.

Hii leo ukimweleza kijana kwamba katika miaka ya nyuma palikuwepo na mashindano ya kurusha vishada, kama inavyofanyika katika nchi nyingi za Bara la Asia hivi sasa, atakushangaa na kutoelewa unazungumzia kitu gani.

Ni vizuri kwa watu wanaohusika na michezo ya watoto na utamaduni wakaliangalia suala hili kwa undani na kutafuta njia za kurejesha utamaduni huu ambao unatoa burdani isiyouwa na madhara kwa watoto na kuwaepusha na vijiwe vyenye mwendo mbaya.

Siku hizi panapofanyika matamasha ya utamaduni wa Mzanzibari huoni sio tu kishada kurushwa , bali hata hakitajwi kwamba upo wakati vishada vilikuwa vinapamba anga ya Zanzibar.

Ninakumbuka nilipokua mdogo wafanyakazi wa Idara ya Umeme (siku hizi shirika) walikuwa na zoezi maalumu baada ya kila muda la kukwamua vishada viliokwama kwenye nguzo na waya za umeme.

Ni vyema utamaduni wa kurusha kishada ukatafutiwa njia za kuufufua na kuendelea kama ilivyokuwa zamani kuwa sehemu ya pambo la anga ya visiwa vya Unguja na Pemba.

Hilo likifanyika, labda ipo siku Zanzibar itashiriki katika mashindano ya kimataifa ya kugombea Kombe la Dunia la kurusha vishada vya aina mbali mbali ambayo kwa kawaida hufanyika Kabul, Afghanistan.

Kuviacha vishada kwenda arijojo ni kuruhusu sehemu ya utamaduni wa kuvutia wa watu wa Zanzibar kwenda arijojo pia.
 

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/75f8a48915fd3968f9b84a90a35bbe4f.jpg

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: Na Salim Said Salim

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi