loader
Dstv Habarileo  Mobile
Asimulia Nyerere alivyoombewa dua Bagamoyo

Asimulia Nyerere alivyoombewa dua Bagamoyo

FAMILIA ya Shehe Mohamed Ramiya ambaye alikuwa akimfanyia dua Baba wa Taifa Mwalimu Julius Nyerere wakati wa kudai Uhuru, imeiomba Wizara ya Maliasili na Utalii kulifanya eneo hilo kuwa la makumbusho.

Shehe Ramiya anatajwa kuwa alikuwa ni mtu mwenye karama (Walii) ya kuwaombea watu waliokuwa na matatizo mbalimbali na kuyatatua na alikuwa na uwezo wa kufanya miujiza.

Akizungumza na waandishi wa habari, mtoto wa mwisho wa Ramiya, Ahmed Ramiya alisema kuwa ili kumuenzi mwalimu kwa mambo mbalimbali ni vema sehemu hiyo ikafanywa sehemu ya makumbusho kwenye eneo hilo Mtaa wa Ramiya Kata ya Dunda Tarafa ya Mwambao Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani.

Shehe Ramiya alifariki dunia akiwa na miaka (78) na kuacha wake wanne na watoto wanane. Mwanaye huyo wa mwisho alipewa jina lake na anafuata nyayo za baba yake. Ramiya alisema kuwa Mwalimu Nyerere alikuwa akifika nyumbani kwao na kufanyiwa dua mara kwa mara wakati wa harakati za kudai uhuru.

“Mwalimu Nyerere aliletwa hapa Bagamoyo na baadhi ya wazee wa Jiji la Dar es Salaam wakiongozwa na Tambaza lengo likiwa ni kumfanyia dua ili harakati za kudai Uhuru zifanikiwe bila ya kumwaga damu,” alisema Ramiya. Alisema kuwa wanaomba kwani kuna baadhi ya watalii kutoka nje ya nchi huwa wanafika hapo na kutembelea sehemu ambayo Mwalimu alifanyiwa maombi na baba yake ambapo nyumba hiyo ni msikiti ina karne mbili kwa sasa.

“Watalii huwa wanakuja hapa na kuangalia sehemu hiyo ambayo ni msikiti ambao umejengwa kwa mawe kwani baba alikuwa na wanafunzi ambao ni Wajerumani wawili hivyo watalii hufika na kuuliza mambo mbalimbali,” alisema Ramiya.

“Shehe Ramiya alimpa baraka na kumwambia nchi itapata Uhuru kwa usalama na damu haitamwagika na kweli mwaka 1961 nchi ilipata Uhuru wake bila ya kumwaga damu kama baadhi ya nchi,” alisema Ramiya.

Alieleza kuwa kutokana na kuthamini mchango wake Mwalimu alimpeleka Chuo Kikuu cha Mzumbe na kusomea masuala ya sheria na aliporudi alimteua kwenye tume ya maadili ya viongozi wa umma na kufanya kazi kwa muda. Hata hivyo, aliacha ili aendelee na shughuli zake za kiimani.

foto
Mwandishi: Na John Gagarini, Bagamoyo

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi