loader
Wataalamu wazungumzia tiba asili dhidi ya Covid-19

Wataalamu wazungumzia tiba asili dhidi ya Covid-19

WATAALAMU wa afya wameeleza umuhimu wa kufanya utafi ti zaidi na kuhalalisha tiba asili ikiwa ni suluhisho la ndani la kuimarisha zaidi mapambano dhidi ya janga la Covid-19. Akizungumza wakati wa majadiliano katika Mkutano wa nane wa Afya wa Tanzania (THS) unaoendelea mjini Dodoma, Mkurugenzi wa Taasisi ya Tiba Asili katika Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Dk Joseph Otieno alisema jukumu la tiba asili wakati wa Covid -19 limeonekana lakini kulikuwa na haja ya utafiti zaidi kufanywa.

Kwa mujibu wa Dk Otieno, utafiti zaidi unapaswa kufanywa matokeo yatumiwe katika kupambana na magonjwa yanayosababishwa na virusi siku zijazo hasa kutokana na kuwapo kwa dalili ya kuibuka magonjwa mengine.

“Mimea ina kemikali ambayo inaweza kuzuia mchakato wa virusi vya Covid-19 kupenya kwenye mwili wa binadamu, kwa hivyo tunahitaji kuhalalisha tiba ya asili za sasa lakini tufanye tafiti zaidi kwa muda mrefu,” alisema.

Mwakilishi Mkazi wa Shirika la EngenderHealth Tanzania, Prudence Masako alisema kuna haja ya juhudi za pamoja katika vita dhidi ya janga la Covid-19 na kuongeza kuwa kushirikisha sekta binafsi katika vita hiyo ni jambo muhimu. “Ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi (PPP), unaweza kutumika kama nyenzo ya kupambana na janga la Covid-19 kwa sababu hii inamaanisha kuweka rasilimali pamoja,” alisema.

Mganga Mkuu wa Serikali, Dk Aifelo Sichwale alisema serikali kwa sasa inaelimisha umma juu ya umuhimu wa chanjo, lakini pia inaendelea na utafiti wa matibabu ambao ndio suluhisho kuu la changamoto zinazoathiri sekta hiyo.

“Hata chanjo ya Covid-19 ni matokeo ya utafiti na kwa suala hili tunahitaji kuimarisha taasisi za utafiti ili kuhakikisha kuwa wanabeba na kutekeleza kazi hii kwa ufanisi,” alisema.

Dk Sichwale alisema kuna haja ya kuja na maazimio ambayo yanapaswa kuwasilishwa kwa wizara kwa hatua kwani mkutano huo umesaidia kutoa maoni lakini pia kupata suluhisho la changamoto katika sekta ya afya.

foto
Mwandishi: Na Anastazia Anyimike, Dodoma

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi