loader
Dstv Habarileo  Mobile
Bil 29/- kuboresha miradi Geita

Bil 29/- kuboresha miradi Geita

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Rais Samia Suluhu Hassan ametoa Sh bilioni 28.6 kwa ajili ya ujenzi na uboreshaji miradi ya maendeleo mkoani Geita.

Majaliwa alisema Rais Samia anataka kuona kila Mtanzania anapata huduma mbalimbali za kijamii zikiwemo za afya, elimu, maji, nishati ya umeme na miundombinu katika makazi yao.

Alisema hayo alipozungumza na wananchi wa Kata ya Muganza katika Wilaya ya Chato mkoani Geita. Alisema kati ya fedha hizo Sh bilioni 16 zimepelekwa wilayani Chato. Majaliwa aliwataka viongozi wa Mkoa wa Geita kuhakikisha fedha hizo ambazo zimetolewa kwa ajili ya utekelezaji wa miradi ya maji, elimu, barabara na afya zinatumika kama ilivyokusudiwa.

Akizungumzia kuhusu changamoto ya upungufu wa watumishi wa sekta ya afya, Majaliwa alisema serikali inaendelea kuajiri ili kuhakikisha lengo lake la kufikisha huduma bora za afya kwa wananchi linafikiwa. Aliagiza uongozi RUWASA Wilaya ya Chato uhakikishe Sh bilioni 5.2 zilizotolewa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi wa maji zinatumika vizuri na wananchi wanapata huduma.

Majaliwa aliwaagiza viongozi hao kuhakikisha wanaanza kufanya utafiti ili waweze kutumia maji ya Ziwa Victoria kwa kuyasambaza kwa wananchi. Alisema haiwezekani watu wakakaa karibu na ziwa bila maji ya kutosha.

Awali, Mbunge wa Chato, Dk Medard Kalemani alishukuru Serikali ya Awamu ya Sita kwa ujenzi wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa katika wilaya hiyo kama ujenzi wa barabara, miradi ya ujenzi wa miundombinu ya elimu, vituo vya afya pamoja na miradi ya maji.

foto
Mwandishi: Na Mwandishi Maalumu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi