loader
Dstv Habarileo  Mobile
Vijiji 94 vyarasimishwa Tabora

Vijiji 94 vyarasimishwa Tabora

SERIKALI imesema kwamba wakazi wa vijiji 94 kati ya 100 vya Mkoa wa Tabora ambavyo vilikuwa na migogoro ya ardhi, wataendelea kuishi katika maeneo hayo wakati utaratibu mwingine wa kuweka mipaka ukiendelea.

Kauli hiyo ilitolewa na Mwenyekiti wa kamati ya mawaziri wanane walioteuliwa na Rais Samia Suluhu Hassan kufuatilia na kutatua migogoro ya ardhi katika mikoa yote, William Lukuvi wakati akiwasilisha taarifa juu ya uamuzi uliofikiwa juu ya vijiji 100 vya Mkoa wa Tabora.

Lukuvi aliwaelekeza watendaji wote wa ngazi za mkoa na wilaya kusimamia uwekaji wa mipaka mipya ya maeneo yaliyokuwa na migogoro bila ya kuleta taharuki kwa wananchi wa maeneo husika.

Alisema kazi ya kuainisha mipaka itafanyika ili wananchi wasiendelee kuvamia maeneo ya hifadhi ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya sasa na kizazi kijacho. Mbunge wa Kaliua, Aloyce Kwezi alishukuru kwa kurasimisha baadhi ya vijiji vya Kaliua ambavyo vilikuwa katika migogoro ya ardhi na kuiomba serikali kutatua mgogoro uliozuka baada ya Hifadhi ya Msitu wa Isawima kupandishwa hadhi. Alisema baada ya Serikali kukabidhi usimamizi wa Isawima kwa Mamlaka ya Usimamizi wa Wanyamapori Tanzania (TAWA), kumekuwepo na mgogoro mkubwa na vijiji 11 ambavyo ndivyo vilitoa ardhi yao kwa ajili ya uanzishwaji wa hifadhi hiyo.

Kwezi alisema TAWA wameongeza mipaka na kuingia katika maeneo ya wananchi jambo ambalo limesababisha taharuki kubwa ya wakazi kukosa mashamba ya kulima wakati wa masika. Lukuvi aliutaka uongozi wa Mkoa wa Tabora kutumia wataalamu waliopo kushughulikia mgogoro wa mpaka baina ya wilaya ya Kaliua na Urambo.

Alisema tangazo lililoanzisha wilaya hizo lipo hivyo, ni vema wakarejea kwenye kumbukumbu hizo na kuondoa dosari ambazo zimesababisha mgogoro wa mpaka katika maeneo hayo. Lukuvi alisema baada ya usuluhisho huo ni vema serikali ngazi ya mkoa, ikaiandikia Tume ya Uchaguzi ya Tanzania (NEC) itumie ramani iliyosainiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na si waliyonayo kwa kuwa inasababisha mgogoro.

foto
Mwandishi: Na Lucas Raphael, Tabora

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi