loader
Polisi yatadharisha wizi mtandaoni, yaonya wasichana picha za utupu

Polisi yatadharisha wizi mtandaoni, yaonya wasichana picha za utupu

JESHI la Polisi linatoa tahadhari kwa wasichana au wanawake kujihadhari na wapenzi au marafiki zao wanaowadanganya wajipige picha za utupu kisha wawatumie ambao baadae wanazitumia kufanya utapeli kwa njia ya mtandao.

Kwa mujibu, Msemaji wa Jeshi la Polisi Nchini SACP David Misime, amesema matukio machache yametokea baada ya wapenzi au marafiki hao kupokea picha hizo walianza kuwataka wasichana waliokubali kuwatumia picha wawape fedha la sivyo watazisambaza kwenye mitandao ya kijamii.

“Baadhi ya wakina dada wamejikuta katika matatizo ikiwa ni pamoja na msongo wa mawazo, kushindwa kufanya shughuli zao za kujiletea maendeleo na wengine kushindwa kufuata masomo darasani na kupelekea kushuka kiwango.” alisema Misime

Aidha, Misime, aliwataka wananchi kuchukua tahadhari watu wachache wanaofanya utapeli kwa njia ya mtandao.

Alisema kuna kesi zimesharipotiwa katika vituo vya Polisi za watu kutapeliwa na watu wanaojifanya Mawakala wa kuagiza bidhaa mbalimbali kutoka nchi mbalimbali duniani.

“Watu hao wamekuwa wakiweka mawasiliano ya udanganyifu na kufanya baadhi kuamini ni mawasiliano sahihi na kwamba wanawasiliana na mawakala sahihi lakini matokeo yake wanajikuta wametapeliwa fedha zao.”alisema

Alisema baadhi ya wahalifu wa aina hiyo wameshakamatwa na wengine wanaendelea kufuatiliwa.

“Tunatoa Wito kwa wananchi kama wanao ulazima wa kutumia mawakala kuagiza bidhaa basi wahakikishe kwanza kama mawakala hao wapo na kwamba ni sahihi kwa kazi hiyo.

“Wanaweza kutumia taasisi mbalimbali kujiridhisha kwanza mfano ofisi za Interpol Makao Makuu ya Polisi Dodoma pia wanaweza kulipa baada ya kupokea bidhaa walizoagiza.

“Kupitia kwenu pia Jeshi la Polisi lingependa kutoa tahadhari kwa wananchi kwa utapeli mwingine ambao umetokea wa baadhi ya wahalifu kutumia majina ya viongozi wa Serikali na viongozi wakuu wastaafu kuwa wamefungua NGOs au mashirika ya kukopesha fedha.

Wahalifu hao wamekua wakifungua akaunti za mitandao ya kijamii kwa majina ya viongozi na kuwadanganya watu watume fedha kwa ajili ya usajili ili wapate mikopo jambo ambalo si kweli ni utapeli.

Kesi kama hizo zimetokea na Jeshi la Polisi limeshakamata baadhi ya wahalifu na linaendelea kufuatilia wengine kupitia kikosi chake cha doria mitandaoni.

“Wito kwa wananchi, wawe makini na wahalifu wa aina hiyo na kuhakikisha kila mara wanapata uthibitisho kupitia taasisi mbalimbali na pia kupitia viongozi wao wa serikali za mitaa ili kuepuka utapeli wa aina hiyo.

Aidha, kuna matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii kwa matapeli kuwapigia watu simu na kujitambulisha kuwa ni afısa kutoka Ikulu na kwamba kuna uteuzi unaendelea hivyo anatakiwa afike Ikulu asubuhi kwa maelekezo.

Mtu aliyepigiwa simu akivutika hutakiwa atume fedha ya tiketi ya ndege ili wao wamfanyie utaratibu wa kupata nafasi kwani ndege za kwenda Dodoma asubuhi zimejaa.

Wapo watu wameshapigiwa simu na matapeli kama hao na wakajiuliza maswali mengi na kuuliza baadhi ya watu mwisho wakabaini hakuna uteuzi unaofanyika kwa mtindo huo na akaepuka mtego wa matapeli.

Alisema Jeshi la Polisi linaendelea kutoa wito kwa wananchi kuwa makini na utapeli kama huo kwa kujiuliza maswali ya uhalali wa jumbe mbalimbali mitandaoni au wanazotumiwa na mawakala feki wa kuagiza bidhaa na akaunti zinazo onyesha ni za viongozi wa serikali.

Aidha kuanzia ngazi ya familia wapeane elimu juu ya matumizi salama na yenye kuleta tija ya mitandao ya kijamii na juu ya matapeli wanavyotumia mitandao kwa utapeli na kwamba usipokuwa makini utapoteza fedha zako au utadhalilika kama hutakuwa makini.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi