loader
Mila desturi zinavyochangia wanaume kupata magonjwa ya akili

Mila desturi zinavyochangia wanaume kupata magonjwa ya akili

 “NILIPATA tatizo baada ya kugundua kuwa nimefanyiwa usaliti na mwanamke ninayempenda sana, niliathirika hadi nikaamua kutumia vidonge ili nife lakini kwa bahati nilinusurika kufa.”

Hii ni kauli ya James Minja (jina la kwanza si halali), kijana wa miaka 32 mkazi wa Mkoa wa Mbeya. Anasema hata baada ya kunusurika kufa bado tabia yake ilibadilika na kuanza kunywa pombe sana.

“Nikawa najitenga na watu, napenda kukaa peke yangu na pia kazini nilikuwa siendi. Baada ya kuona nimebadilika dada yangu alinipeleka hospitali nikaanza matibabu na pia nikapata msaada wa kisaikolojia.

Anasema hakuwahi kuweka wazi tatizo lililokuwa likimsumbua haraka hadi alipozungumza na daktari.

“Ilikuwa ni siri yangu sikutaka watu wajue, lakini daktari aliponiuliza ikabidi nisimfiche baada ya kupata matibabu ya dawa na kisaikolojia sasa nimerudi kwenye hali yangu ya awali,” anaeleza.

James ni miongoni mwa wanaume wengi wanaopata tatizo la afya ya akili bila kushirikisha watu wa karibu.

Kwanini hakushirikisha ndugu zake?

Anajibu anasema: “Nilikuwa na aibu ya kuchekwa na pia nilikuwa nawaza kuonekana dhaifu kulingana na makuzi katika jamii zetu.

Dk Rayamod Mgeni, kutoka Idara ya Afya na Magonjwa ya Akili, Hospitali ya Rufaa ya Mbeya anayemhudumia James anakiri kuwa hali yake imeimarika.

Takwimu za Hospitali ya Taifa ya Muhimbili zinaonesha kuwa wanaume ndio wanaoongoza kupata magonjwa ya akili kuliko wanawake.

Kwa mwaka 2018/2019 takwimu zilionesha kuwa idadi ya wanaume waliougua walikuwa 18,535 huku idadi ya wanawake ikiwa 10,631. Takwimu hizo pia zinaeleza ongezeko la wagonjwa wa afya ya akili kwa asilimia 10.8.

Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Akili katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, Dk Fileuka Ngakongwa anasema wagonjwa waliotibiwa kwa mwaka 2019/2020 walikuwa 32,307 ikilinganishwa na wagonjwa 21,183 walitibiwa 2018/19.

“Kwa upande wa Muhimbili Mloganzila 2019/2020 wagonjwa waliotibiwa walikuwa ni 980 wakati mwaka 2018/2019 waliotibiwa walikuwa 753 huku ongezeko likiwa ni asimilia 23.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), watu zaidi ya milioni 300 wana matatizo ya afya ya akili huku hapa nchini watu milioni saba wakiwa na tatizo hilo wengi wao wakiwa ni wanaume.

Ripoti hiyo inamaanisha kuwa vijana asilimia 20 wana shida ya afya ya akili na katika nchi za kipato cha kati na chini karibu asilimia 15 wamefikiria kujiua. Kujiua ni chanzo cha vifo vya vijana wenye umri wa miaka 15 -19 duniani.

Katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Mbeya, Dk Mgeni anasema asilimia 60 ya wagonjwa wa akili anaowaona ni wanaume.

“Kwa wiki tuna kliniki siku tatu tunaona wagonjwa 40 na wagonjwa 160 kwa mwezi.”

Kutokana na takwimu hizo, HabariLEO ilifanya mahojiano na wataalamu wa afya ya akili, wazee wa mila, viongozi wa dini na wanasaikolojia kujua sababu ya wanaume kuongeza kupata magonjwa hayo.

JE, MILA NA DESTURI INAWEZA KUWA MAUMIVU KWA WANAUME?

“Mila na desturi zetu zinamwangalia mwanaume kama kiongozi mkuu wa familia, hivyo naamini anaweza kubeba majukumu yote bila kulalamika, kustahimili vitu vyote.

“Huwa utamaduni hauruhusu wanaume kuongea matatizo yanayowakumba hadharani, tunawafundisha kuwa na ukakamavu na ujasiri,” anasema Sonda Kabeshi Mzee wa Mila wa jamii ya Wasukumu mkoani Shinyanga.

“Hali hiyo tunaiita uanaume, wanaume wengi hawawezi kusema migogoro ya ndani ya familia endapo kama mke ni msumbufu au anakosa huduma anazotakiwa kupata ni aibu.”

Mshili wa Kabila la Wameru, mkoani Arusha, Stanley Kitomary anasema katika kabila hilo wanaume ni watu shupavu ambao wanaweza kustahimili kila changamoto na kuzitatua wenyewe bila kushirikisha watu wengine.

“Lakini yapo mambo wanashirikisha wazee wa ukoo pale anapokosa kabisa utatuzi wa changamoto, wengi ni wasiri katika kueleza matatizo yao na hii ni kulingana na utamaduni tuliokuta ya kuwa mwanaume imara zaidi.

   

 

“Kukabiliana na matatizo inaweza kuwa sababu, wanaume hawaoneshi hisia za wazi kisaikolojia ni hatari anaona bora akanywe pombe au kutumia dawa za kulevya anaona akielezea ni udhaifu.

“Hivyo hawapelekwi hospitali moja kwa moja hadi inaposhindikana wanakuja, hii inaathiri matibabu na pia unyanyapaa ni tatizo,” anaeleza Dk Mgeni.

Mtaalamu wa Saikolojia kutoka Chuo cha Kikatoliki cha Mwenge (MWECAU), Cristian Bwaya anakiri kuwa wanaume wanakumbwa na tatizo hilo kutokana na mfumo wa maisha katika jamii.

“Kitu kidhaifu kwa mwanamke huwa kina utatuzi mfano akikerwa atalia, akiwa na taarifa ya kusumbua moyo atasema wanawake wengi si watu wa kuweka vitu akiwa na vitu atazungumza.

“Akifiwa atalia na akiwa na wasiwasi na kitu atasema, hii kwa wanaume wanaona ni udhaifu ni kwasababu mwanaume amelelewa kuficha hisia zake,” anaeleza Bwaya.

Anasema hali hiyo ndiyo inayoathiri afya ya akili kwa wanaume wanaponzwa na tabia zao za kuvumilia vitu ambavyo ndani yao havivumiliki. “Tabia ya kutokuongea na kuogopa kudhalilika ndio inasababisha kupata shida.”

Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Afya ya Akili Tanzania, Isack Lema anasema sababu zingine ni mtoto wa kiume kusahaulika katika malezi na uwezeshaji ndani ya jamii.

“Zipo sababu nyingi kwanza tunaangalia magonjwa yanayopatikana kwa kiwango kikubwa kama magonjwa ya sonona, magonjwa ya hisia (bypola), magonjwa ya akili aina ya ‘skizofeni’ na magonjwa ya matumizi ya vilevi.

“Kwa magonjwa ya sonona wanaume wengi wanayo kwasababu hawaongei matatizo yao au kwenda katika njia ambazo si sahihi kama matumizi ya vilevi. “Kundi kubwa la wanaume linajiingiza katika matumizi ya vilevi kama pombe, bangi, vitu hivi huathiri mfumo wa akili na kuchochea magonjwa ya akili.”

Lema anayefanya kazi katika Hospitali ya Taifa Muhimbili anaeleza kuwa kampeni nyingi za uwezeshaji zinawaelekea vijana wa kike hivyo changamoto za maisha kama uchumi zinawaumiza vijana wa kiume.

SABABU ZA KIBAIOLOJIA

Mkuu wa Idara ya Magonjwa ya Akili, Dk Ngakongwa anasema sababu nyingine ni utofauti wa kibaiolojia kati ya mwanaume na mwanamke.

“Mfano ugonjwa wa skizofemia (kichaa) uwiano kati ya mwanaume na mwanamke ni mbili ya moja. Kibaiolojia wanaume wanaweza kupata mara mbili zaidi ya wanawake na pia wanaume wanawahi kupata kwa umri mdogo kulinganisha na wanawake lakini ukija kwenye sonona uwiano kwa wanaume ni mkubwa zaidi,” anabainisha.

HII NI NAMNA YA KUJISAIDIA

Mwanasaikolojia Bwaya anasema wanaume watambue wakishikilia vitu kwa sifa ya uanaume vinaweza kuwaponza.

Anawataka wanaume kujenga mifumo itakayowasaidia kutoa sumu kwenye mioyo yao wasiogope kudhalilika. “Kingine wanaume waoneshe hisia pale wanapojisikia vibaya mfano kulia.

Lema anasema kwa sasa wanaendelea kuhamasisha wanaume wazungumze kuhusu matatizo wanayopitia.

“Familia ziwe na utaratibu wa kuzungumza kati ya mzazi na mtoto au kati ya ndugu kwa ndugu waelezane matatizo yao na jinsi ya kuyatatua na wasitumie vilevi ni hatari zaidi.

“Waachane na mila na desturi zinazowaumiza na wajijengee njia za kukabili changamoto zinazowakabili,” anashauri.

 VIONGOZI WA DINI WAPENDEKEZA HAYA

Katibu Mkuu wa Baraza la Waislamu Tanzania (BAKWATA), Nuhu Mruma anasema wanaume wanaojitokeza kutafuta suluhu kwa viongozi wa dini ni wachache, wengi ni wanawake.

Anashauri: “Pale ambapo mwanaume kuna jambo limekushika ni bora kushirikisha watu unaowaamini kuliko kuchukua maamuzi ya kujiathiri au kuathiri wengine.”

Mchungaji mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Richard Ananja anaeleza kuwa mfumo unafanya wanaume kuvumilia kutoelezea matatizo yao.

“Wanaume wanatengenezwa kuvumilia na mila na desturi zetu lakini waliopata ukombozi wa fikra hawazingatii hilo, hatuwezi kutatua matatizo yetu wenyewe hivyo ni vizuri kuondoa mfumo wa kuona wanaume ni jasiri.

https://www.apps.tsn.go.tz/public/uploads/722ef458dbb39cdd3d598692af37a2d0.PNG

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: Aveline Kitomary

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi