loader
Jiwe, Unga wa Ulezi, Majivu ukatili mpya ukeketaji watoto

Jiwe, Unga wa Ulezi, Majivu ukatili mpya ukeketaji watoto

AINA mpya ya ukeketaji imeibuka nchini ambao wahusika hufanya kwa kuwasugua maumbile ya siri  ya watoto wachanga kwa kutumia jiwe la kusugulia miguu, unga wa ulezi au majivu.

Ofisa Maendeleo ya Jamii wa Halmashauri ya  Wilaya ya Arusha, Angela Kiama  ameyasema hayo katika mahojiano maalum kuhusu ukeketaji kwa wanawake na watoto na kwamba walibaini  hayo baada ya kuanza kuwakagua watoto wanaopelekwa kliniki.

“Ukeketaji mpya ulioibuka hivi sasa wanachukua jiwe lile la kusugua miguu, wanawasugua maumbile yao mpaka yanaisha, ukimkagua mtoto unakuta eneo lake la sehemu za siri jekundu sana na wanaposuguliwa wanatoka damu na inaacha makovu.

“Ndio ukatili tunaopambana nao kwa sasa, maana kila siku mangariba wanabuni njia mpya, wapo ambao wanawakeketa wakiwa wachanga tumepambana na hilo, sasa wamebuni njia hiyo nyingine ya kuwasugua kwa jiwe, tunachoomba mtu akioneka mtoto anafanyiwa ukeketaji wa namna hii aripoti haya matukio hili tuweze kufikia lengo la serikali ifikapo 2022 la kutokomeza ukeketaji nchini,”alisema.

Mpango wa Taifa wa Utekelezaji wa kukomesha Ukatili dhidi ya Wanawake na Watoto (NPA-VAWC) 2017/2018-2021/2022) umeeleza kwa ufasaha kwamba ukeketaji ni mila inayoathiri wanawake na watoto. Tanzania imedhamiria kukomesha kabisa ukatili wa aina zote dhidi ya wanawake na watoto, ikiwemo ukeketaji, kama sehemu ya utekelezaji wa ajenda ya Maendeleo Endelevu ya 2030.

Ofisa Uhusiano wa UNFPA, Warren Bright akizungumza kwa njia ya simu katika mahojiano maalum  alisema kuelekea mwaka 2030 malengo ya Dunia, iwapo Mataifa yatasimama pamoja ipasavyo lengo namba tano katika usawa wa jinsia wadau wakishirikiana watatokomeza ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na mila kandamizi dhidi ya wanawake na wasichana .

Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa  inakadiriwa kuwa wasichana na wanawake wapatao milioni 200 wamepitia aina fulani ya ukeketaji katika nchi 30 hasa barani Afrika, Mashariki ya Kati na Asia.

Pia Takwimu za Kitaifa zinaonesha mikoa mitano iliyo na kiwango cha juu cha ukeketaji ni pamoja na Manyara (asilimia 57.7 ya wanawake wenye umri kati ya miaka 15 hadi 49 wamefanyiwa ukeketaji), Dodoma (asilimia 46.7), Arusha (asilimia 41), Mara (asilimia 32) na Singida (asilimia 30.9).

Takwimu pia zinaonesha kuwa wanawake na wasichana wenye umri wa miaka 15 hadi 49 ambao wanaishi katika maeneo ya vijijini wana uwezekano mara mbili ya wenzao wa mijini kufanya ukeketaji (asilimia 12.7 vijijini dhidi ya asilimia 5.3 mijini).

Ngariba aweka nyembe chini:

Maclina Robbi John (50) ni Ngariba aliyeweka wembe chini na kuamua kuokoka, anasema mbinu hizi mpya zimekuwa zikitumika katika koo mbali mbali.

“Kwa sasa wanakeketa watoto wadogo kwa kutumia Jiwe la kusugulia miguu, unga wa ulezi kwa kikurya tunaita ‘Ememera’ kuna koo nyingine wanaita ‘Inama Inuka’ kwamba Ngariba ameinama akinuka ameshatimiza lengo lake, ingawa baadhi ya koo bado wanakeketa kwa wembe.

“Kwa sasa wanakeketa kwa aina hizo watoto wa dogo kwa vile hawajitambui, wakishakuwa wakubwa kuanzia miaka 13 wengi wanakuwa wanajitambua hivyo wanakimbia na wengine wanakuwa wasumbufu, ndio maana wanafanyiwa angali wadogo,” anasema Robi

Aweka wembe chini

Nimeacha kukeketa baada ya kukamatwa na kufungwa miezi sita, kwa sasa nimeokoka baada ya kushawishiwa na Katekista Dominic Kastari niache na niokoke.

“Nimekeketa zaidi ya mabinti 10,000 waliopata madhara ni ambao wametoka damu nyingi, ni wengi pia, ila sina idadi.” anasema

Wazee wa Mila waficha waliofariki:

Wazee wa mila hawawezi kusema kwa Ngariba kuwa mtu amekufa kwa sababu ya kukeketwa, wanaficha ili kutoleta hofu kwenye jamii.

Atoa suluhisho la kutokomeza ukeketaji:

Ngariba Robi anasema ili kutokomeza mila hizo za ukeketaji, serikali iwekeze nguvu katika kuwawezesha kiuchumi.

“Unajua mfano mwezi huu wa 11 hadi Januari mwanzoni ni msimu wa ukeketaji, Ngariba anapata mamilioni ya hela, zawadi za ng’ombe na mbuzi, wanategemea zaidi kupata kipato kupitia ukeketaji,ila wakielimishwa kama nilivyoelimishwa mimi na kuwezeshwa kiuchumi wataacha.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) inasema wanawake na wasichana waathirika wa ukeketaji wanakabiliwa na hatari kubwa katika afya yao na uzima, hii ni pamoja na athari pindi tu baada ya kukeketwa ikiwemo: maambukizi, kuvuja damu nyingi au kiwewe pamoja na magonjwa ya muda mrefu ambayo huenda yakatokea maishani.

Pia wanawake ambao wamekeketwa wana uwezekano mkubwa wa kupata tishio la kupoteza maisha wakati wa kujifungua, kukabiliwa na magonjwa ya akili na maambukizi ya muda mrefu.

Pia huenda wakahisi uchungu wakati wa hedhi, wakienda haja ndogo au wakati wa kitendo cha kujamiana.

Manusura Wanena:

Robby Karumo, ni mmoja wa waathirika wa ukeketaji akiwa mkoani Mara anasema  “Mimi ni manusura wa ukeketaji, niña watoto wanne, wavulana wawili na wasichana wawili, kazi yangu kubwa ni kutoa mafunzo kuhusu madhara ya ukeketaji. Tunawaambia akina mama na wasichana kwamba ukeketaji una madhara kwa wasichana wetu na kwetu sisi, huenda sehemu ya mwili wangu ilichukuliwa lakini siwezi kamwe kutoa moyo wangu. Ndani ya moyo wangu ninawaza ni jinsi gani tunaweza kutomeza ukeketaji.”

Kwa upande wake manusura mwingine wa ukeketaji Nyanjige Wangesi kutoka Mara pia anasema “Iwe ni kwa kutangaza kwenye radio au televisheni au kuzungumzwa na watu wa jamii yangu, ujumbe ni kutokomeza ukeketaji, iwapo hatutatokomeza kitendo hicho basi vizazi vijavyo vitaendeleza ukeketaji. Ni lazima tuusitishe hapa.”

Ukeketaji ni ishara ya ukosefu wa usawa wa kijinsia

Zaidi ya wasichana na wanawake milioni 200 duniani ni amnusura wa ukeketaji ambao una madhara ikiwemo athari za kiafya. Kwa mujibu wa takwimu za Umoja wa Mataifa za mwaka 2020, takribani wasichana milioni 4 wako hatarini kukeketwa.

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Gutteras ananukuliwa akisema  “ukeketaji ni ishara tosha ya ukosefu wa usawa wa kijinsi uliyoota mizizi katika mifumo ya kijamii, kiuchumi na kisiasa. Aidha ni ukiukaji wa haki za binadamu na ukatili mkubwa dhidi ya wanawake. Kwa bahati nzuri kuenea kwa visa hivi kumepungua kwa aslimia 25.”

Amesema, hata kisa kimoja cha ukeketaji hakifai na kwamba, kuna umuhimu wa vijana kupaza sauti zao. Ni lazima tuimarishe sauti hizo na tuwasaidie kuchagiza kuleta mabadiliko na kwa ajili ya haki zao.”

Guterres amesema, “kwa pamoja tunaweza kuutokmeza ukeketaji kufikika mwaka 2030. Kwa kufanya hivyo kutakuwa na matokeo chanya ya muda mrefu kiafya, kielimu na kiuchumi kwa ajili ya wasichana na wanawake.”

 

 

foto
Mwandishi: Vicky Kimaro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi