loader
Dstv Habarileo  Mobile
Samia apongezwa amani, umoja

Samia apongezwa amani, umoja

VIONGOZI wa dini wakiwemo Mashehe na Maaskofu wameunga mkono ujumbe wa Rais Samia Suluhu Hassan katika sherehe za Maulid ya Kuzaliwa Mtume Muhamad (S.A.W) unaohimiza amani, upendo na mshikamano kwa Taifa.

Katika ujumbe alioutoa kupitia ukurasa wake wa Twitter jana, Rais Samia aliwatakia Waislamu na Watanzania kwa ujumla heri ya Sikukuu ya Maulid na kuwataka washerehekee kwa amani, upendo na mshikamano kama walivyofundishwa na Mtume Muhamad (S.A,W).

Rais Samia alihimiza Watanzania kuwa, kuzaliwa kwa Mtume Muhamad (S.A.W) kulete ari na mwito mkubwa zaidi wa kuendelea kuijenga nchi yao na kuinua ustawi wa jamii nzima.

Shehe wa Mkoa wa Pwani, Hamis Mtupa alisema alimekea ujumbe wa Rais Samia kwa furaha kwa sababu Tanzania inapita kwenye changamoto za kisiasa, kiimani na kijamii hivyo ni muhimu Watanzania wawe na umoja na mshikamano.

“Ili Tanzania ibaki salama na amani, ujumbe huu unatakiwa kuhamasishwa usiku na mchana kwa raia wote wa Tanzania ili tuwe wamoja na mshikamano.” “Watu wa siasa wanatutegemea watu wa dini na watu wa dini tunawategemea watu wa siasa na tunategemeana wote kama Watanzania,” alisema Shehe Mtupa.

Askofu wa Kanisa la Anglikana Tanzania Jimbo la Shinyanga, Johnson Chinyong’ole alisema 

ujumbe wa Rais Samia unahitajika zaidi kwa sasa kuliko wakati mwingine wowote.

“Kama taifa, mambo haya matatu ndiyo yametuunganisha Watanzania, amani yetu, upendo wetu na mshikamano wetu na ndiyo maana nchi nyingine zinaongelea ukabila lakini sisi tunajenga utaifa kwa sababu ya mambo haya matatu.”

“Kwa hiyo aliyoyasema Mheshimiwa Rais sisi kama viongozi wa dini tumeyapokea. Ujumbe huu wa amani, upendo na mshikamano ni wa msingi hata kwenye vitabu vyetu vya dini kwa upande wa Ukristo na upande wa dini

nyingine kama vile Uislamu yamesisitizwa,” alisema Askofu Chinyong’ole.

Alisema miongoni mwa mambo makubwa yanayotajwa kwenye Biblia Takatifu wakati wa kuzaliwa kwa Yesu Kristu ni amani.

“Sisi tunaamini kwamba, tabia ya kwanza ya Mungu ni upendo na ndiyo maana anasema mpende jirani yako kama nafsi yako. Amani na upendo ndiyo vinatufanya tuwe na mshikamano iwe ndani ya kanisa au nje ya kanisa. Kinachotuunganisha Watanzania ni amani, upendo na mshikamano wetu licha ya itikadi tunazotofautiana kifalsafa lakini sote ni Watanzania tunajenga amani ya Tanzania, tupendane

sisi kwa sisi, tudumishe mshikamano,” alisisitiza Askofu Chinyong’ole.

Shehe wa Mkoa wa Singida, Issa Nassoro alisema amani, upendo na mshikamano ni dira ya Uislamu.

“Nitoe wito kwa Waislamu wote kwamba huo siyo wito wa Mheshimiwa Rais, bali ni wito wa Mwenyezi Mungu kupitia Mtume wake Muhamad (S.A.W), kwa hiyo tuishi na Waislamu na wasio Waislamu kwa amani na salama na hata wasio na dini,” alisema Shehe Nassoro.

Askofu Msaidizi wa Jimbo Katoliki la Bukoba, Methodius Kilaini alisema ameupokea ujumbe wa Rais Samia vizuri kwa sababu

Watanzania wanahitaji kushikamana na bila amani hakuna maendeleo.

“Ukishika haya matatu, amani, upendo na mshikamano maendeleo yanaingia vizuri, kwa hiyo tukiyashika na kuyaendeleza tutafika mbali. Viongozi wa dini tushikamane bila kujali imani na makabila yetu, bila kutazama tofauti zetu kwa sababu Tanzania ni yetu na kwa pamoja tutaiendeleza,” alisema Askofu Kilaini.

Shehe wa Mkoa wa Mwanza, Hassan Kabeke alisema ameupokea kwa umakini na furaha ujumbe wa Rais Samia kwa sababu mambo hayo matatu amani, upendo na mshikamano, ndiyo hasa alikuja nayo Mtume Muhamad (S.A.W).

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi