loader
Dstv Habarileo  Mobile
Majaliwa ahimiza Watanzania haki, mshikamano

Majaliwa ahimiza Watanzania haki, mshikamano

SERIKALI imewataka Watanzania wadumishe amani, umoja na mshikamano kwa ustawi wa taifa kwa kuwa mambo hayo ni tunu kutoka kwa Mwenyezi Mungu aliyewakirimia.

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alitoa mwito huo alipomwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan kwenye Baraza la Maulidi kitaifa kusheherekea kuzaliwa Mtume Muhamad (S.A.W) katika Uwanja wa Kaitaba, Bukoba mkoani Kagera jana.

Alisema kudumisha amani ni jukumu la kila mwananchi kwani bila amani hawawezi kupata maendeleo, kufanya ibada, watoto kwenda shule au kufanya shughuli za maendeleo.

“Maadhimisho haya kwetu ni fursa muhimu kuyasoma na kuyatafsiri kivitendo maisha ya Mtume Muhamad (S.A.W) katika mfumo wetu wa maisha ya kila siku ili kuyafanya yawe bora zaidi hapa duniani.” “Tafakuri hiyo ituwezeshe kuisha maisha ya undugu, tupendane, tuheshimiane, lakini pia tushikamane miongoni mwetu Waislamu na Watanzania wote kwa ujumla wake,” alisema Majaliwa.

Alisema tangu Rais Samia aingie madarakani, ameliongoza taifa kwa kutoa haki bila kuzingatia tofauti za kidini, ukabila, maeneo ili kila mtu aishi kwa furaha, upendo na mshikamano.

Kuhusu kuharakishwa kesi za watu waliopo magerezani kama alivyoomba Shehe Mkuu Mufti Abubakar Zubeir, Waziri Mkuu alisema kama nia njema ya Rais Samia kesi zinaisha kwa kuzingatia taratibu na sheria jambo hilo litakwisha kwa utaratibu huo na kwa maelekezo ya Rais.

Chanjo Majaliwa alisema viongozi wa dini wamekuwa wakiiunga mkono serikali katika mapambano dhidi ya magonjwa mabaya ikiwamo malaria, ukimwi, kifua kikuu, Covid-19 na mengineyo.

Alisema wataalamu wamefanikiwa kupata chanjo ya Covid-19 na Rais Samia ameshazindua kampeni ya chanjo hiyo, hivyo Watanzania wamuunge mkono kwa kuchanja.

“Chanjo hii ni salama na inatolewa bure, tujitokeze kwa wingi kupata chanjo na kuhamasisha wengine. Taifa haliwezi kuwa salama kama afya zetu zitakuwa mashakani, kuchanja ni muhimu, kunasaidia kupunguza makali ya ugonjwa na kuongeza virutubisho ndani ya mwili,” alisema Majaliwa.

Alisema nchi zilizoweka zuio kwa Watanzania kutokana na kutochanja zimeanza kufungua milango ikiwamo Uingereza, pamoja na Maka ambako watu hawakwenda kuhiji kwa miaka miwili kutokana na janga hilo.

Pia alitoa mwito kwa Watanzania kushirikiana na serikali kufanikisha maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru Desemba 9 mwaka huu, lakini pia kushiriki katika sensa ya watu na makazi Agosti mwakani.

Awali, Mufti Zubeir alitoa ombi kwa serikali kuhusu Msikiti wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania Msikiti Mkuu wa Mfalme Muhamed wa Sita uliopo Dar es Salaam uanze kutumika kwa kuswali na Mfalme atakapopata nafasi aje aufungue kwa sababu unavyoendelea kukaa unaweza kuharibika.

Majaliwa alimhakikishia Mufti kuwa atapata jibu katika kipindi kifupi kijacho.

foto
Mwandishi: Matern Kayera

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi