loader
Dstv Habarileo  Mobile
Mwalimu Mkuu mbaroni kipigo cha mwalimu darasani

Mwalimu Mkuu mbaroni kipigo cha mwalimu darasani

JESHI la Polisi mkoani Morogoro linamshikilia Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Mkuyuni, Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Mussa Hasira (46) kwa tuhuma za kumpiga mwalimu mwezake darasani hadi kumng’oa jino.

Hasira anadaiwa kumpiga Witness Clemence Makoti (31) kwa kutumia fimbo, ngumi na makofi.

Kamanda wa Polisi Mkoa Morogoro, Fortunatus Muslimu alisema jana kuwa, tukio hilo lilitokea Oktoba 15, mwaka huu shuleni hapo.

Alisema baada ya tukio hilo, Witness alitoa taarifa katika Kituo cha Polisi Mkuyuni na alipewa RB na akatibiwa katika Kituo cha Afya Mkuyuni na hali yake inaendelea vizuri.

Alisema chanzo cha tukio hilo hakijafahamika na kwamba Hasira amekamatwa.

Jana, Witness alisema kwa njia ya simu kuwa, Mwalimu Mkuu, Hasira alimpiga Ijumaa mchana wakati akiwa darasani na wanafunzi watatu wa kike akisahihisha kazi zao na kujibu baadhi ya maswali waliyokuwa wakimuuliza.

Alidai kwa kawaida inapofika muda wa mapumziko asubuhi huwa anakwenda kumnyonyesha mwanawe lakini siku hiyo kabla ya kuondoka wanafunzi watatu wa kike walimfuata darasani na madaftari wakihitaji kusahihishiwa na kuelekezwa kuhusu kazi zao.

Witness alidai mara nyingi wanafunzi wa madarasa tofauti humfuata kumuuliza maswali na pia kusahihishiwa kazi zao.

Alidai siku ya tukio wakati akiwa na wanafunzi hao aliingia mwalimu mwezake wa kike na kumuuliza anafanya nini na wanafunzi hao, alimjibu kuwa alikuwa akizungumza nao wakimuuliza maswali na kusahihisha kazi zao.

Alidai mwalimu mwezake pia alimuulizia kama angeweza kupata kofia sawa na aliyoivaa yeye siku hiyo.

Mwalimu huyo alidai pia hujushughulisha na ujasiriamali wa kutengeneza chokoleti na kushona kofia na kuziuza kwa wateja.

Alidai muda mfupi baada ya mwalimu mwenzake kuondoka darasani humo, aliingia Mwalimu Mkuu na akamuuliza alikuwa akifanya nini na wanafunzi hao.

Alidai kabla ya kujibu Mwalimu Mkuu huyo alimshika na kuanza kumpiga mbele ya wanafunzi ambao walikimbia kwenda nje ya darasa.

Witness alidai wanafunzi walimjulisha mwalimu aliyekuwa kwenye varanda la jengo akisahihisha madaftari, akaingia ndani kuamulia lakini wakati huo alikuwa amepigwa sehemu mbalimbali za mwili.

Mwalimu huyo alidai hafahamu kwa nini alipigwa na alitoa taarifa kwa Mratibu Elimu Kata (MEK) na Ofisa Elimu wa Halmashauri ya Wilaya Morogoro.

Ofisa Tarafa ya Mkuyuni, Eleonora Kileva alithibitidha kutokea kwa tukio hilo na kwamba walitoa taarifa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri na kwa Mkuu wa Wilaya.

foto
Mwandishi: John Nditi, Morogoro

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi