loader
‘Tanzania nitakulinda mpaka kufa’

‘Tanzania nitakulinda mpaka kufa’

NDUGU msomaji, kwa muda mrefu nimekuwa nikiandika kuhusu umajumui yaani makala kuhusu Bara la Afrika kwa ujumla. Kwa maoni yenu leo nimeamua kuandika kuhusu nchi yangu pendwa.

“Naapa naahidi mbele za Mungu, Tanzania nitakulinda mpaka kufa, Tanzania ni ngali mtoto mdogo, nimepewa jukumu la kukulinda wewe. Naapa naahidi mbele za Mungu, Tanzania nitakulinda mpaka kufa…”

Ni wazi kwamba kwa kila aliyebahatika kupita jeshini wimbo huu ukisikika lazima ‘vibe’ (kama wasemavyo vijana) liamke. Wimbo huu huimbwa kwa hisia na mapenzi halisia kwa waimbaji wenyewe.

Umesheheni kila kiashiria cha uzalendo na ukakamavu katika kutimiza majukumu ya kulilinda taifa letu.

Leo nimependa kukumbuka wimbo huu katika makala haya kwa kuwa nitagusa mambo kuhusu taifa letu pendwa la Tanzania.

Inawezekana kwa sasa neno la uzalendo lisisikike sana, lakini kwa taifa lolote kuendelea ulimwenguni, dhana ya uzalendo haiepukiki hata kidogo. Ni jambo linalopaswa kuhubiriwa usiku na mchana wakati wote pasipo kulionea aibu.

Kulinganisha na mataifa mengine ulimwenguni, Tanzania imebarikiwa sana. Ina madini ya kila aina tena mengine yanapatikana Tanzania tu, ina gesi asilia, ina milima na wanyama kwaajili ya vivutio.

Inasadikika kuwa na mabaki ya mtu wa kwanza kuishi duniani, inawezekana kuwa na mafuta, juzi kumegunduliwa masalia ya mjusi aliyesadikika kuishi miaka zaidi ya milioni 150 huko mkoani Lindi na mambo kadha wa kadha lakini bahati mbaya hadi leo, zaidi ya miaka 50 ya Uhuru vitu vyote hivi havijaweza kumnufaisha Mtanzania ipasavyo.

Sitaki kuamini kwamba ni kwa sababu ya kukosa uwezo ila naamini ni kwasababu ya kukosekana kwa utashi wa kisiasa baina ya wanasiasa.

Wakati fulani Rais wa Awamu ya Tano, Dk Joseph Magufuli alipata kunena kwenye moja ya hotuba yake maneno haya, nanukuu:

“Ni aibu, Tanzanite ndugu zangu zilikuwa zinasombwa tu. Na ndio maana nchi inayoongoza kuuza Tanzanite duniani siyo Tanzania, nchi ya pili inayoongoza kuuza Tanzanite duniani siyo Tanzania! Wakati madini ya Tanzanite yako Tanzania na ndio maana yaliitwa Tanzanite kutokana na neno Tanzania.

“Fedha zilizokusanywa za Tanzanite duniani Tanzania imepata asilimia tano, asilimia tisini na tano zimeliwa na wengine wa nje. Mnataka ndugu zangu niache kuzungumza hili? Sasa nilichaguliwa kuwa Rais wa nini? Kama nisipozungumza huo uozo hadharani?...

“Kwa hiyo nilitaka kuwaambia ndugu zangu vita ya uchumi ni ngumu zaidi kuliko vita ya kawaida… na ndio maana nawaomba wote tusimame kwa pamoja tuwe wamoja na tupiganie haki zetu..”

Inawezekana maneno haya yakakosa nguvu au maana kwa vile aliyeyasema kashatangulia mbele ya haki, lakini je, ni kweli kama nchi tumeshindwa kusimamia rasilimali zetu wenyewe?

Hatuoni umuhimu wa kuongeza masharti magumu ili wanaozihitaji wazipate kwa gharama kubwa? Hatuoni umuhimu wa kila Mtanzania kunufaika na hizi mali? Je, atanufaikaje kama hatutaweka misingi na mifumo ya kuruhusu faida hii kwa wananchi wote?

Kila nikiwaza haya huwa naikumbuka Libya ya Ghadaffi, kutoka kwenye nchi ya jangwa hadi nchi ya asali na manemane huku kila mahali kukijaa bustani nzuri za kuvutia. Naikumbuka ilivyokuwa na uwezo wa kuwahudumia Walibya wote pasipokuwa na hiana huku wote wakinufaika na keki ndogo ya nchi hiyo kutokana na rasilimali ya mafuta.

Bahati mbaya mabeberu wakamuondoa kabla hata ya kutenda makubwa zaidi kwa ajili ya watu wake. Sasa huwa kuna msemo kama iliwezekana kule sisi tunashindwaje?

Kwa nyakati tofauti viongozi wetu wa kisiasa hutenda kwa kushauriwa na wasaidizi wao ambao kwa namna moja au nyingine wanaweza kukosea mahali katika ushauri wao.

Kwa mfano hivi majuzi kumekuwa na matamko tofauti kuhusu suala zima la wamachinga. Inawezekana kwa maslahi ya watu wachache jambo hili lilipitishwa kabla hata ya kulifanyia tafiti katika suala zima la mapokeo kwa walengwa kwa baadhi ya maeneo.

Nafikiri hii nchi ni yetu sote, kuna umuhimu wa kila mmoja kuchangia pato la taifa na pia kufaidi matunda ya rasilimali zetu kwa usawa.

Bahati mbaya mara nyingi kuandika haya huwa na taswira mbili ya kwanza ni ya ulalamishi na ya pili ni ya kukosoa. Lakini nakipenda sana Chama changu Cha Mapinduzi (CCM) na kwamba kama nilivyoapa kuilinda nchi na chama 

changu ni vile vile.

Sitanyamaza nikiona kuna dalili za kukipa shida chama changu kipindi cha kampeni za 2025 japo nimeona zimeanza mapema sana kipindi hiki. Sijui ni kwa makusudi au ni kwa bahati mbaya lakini natamani kuona wananchi wote wakinufaika na matunda ya chama changu tawala.

Natamani kuona nguvu zaidi tena ya pamoja ikitumika kupigania rasilimali zetu kama Watanzania ili zitunufaishe wote? Bahati mbaya tuna baadhi ya wanasiasa wanaowaza matumbo yao tu na hivyo wakati mwingine wako tayari kujifanyia unafiki hadi wao wenyewe ili wapate wanachotaka.

Wanasiasa huongea maneno ya kuwafurahisha wateuzi wao ili wazidi kutetea nafasi zao walizopewa badala ya kuzitetea kwa kuchapa kazi inayoleta matokeo chanya kwa wananchi.

Tunahitaji uzalendo haswa katika kupigania rasilimali zetu, kuilinda nchi yetu dhidi ya watu wenye nia ovu. Vijana kuna umuhimu wa kuwakumbusha wazee wetu juu ya viapo vyao na sisi kuzidisha uzalendo na kuungana na serikali iliyopo kuwaletea Watanzania na kulinda nchi yetu mpaka kufa.

Mwandishi wa Makala haya anapatikana kwa namba +255712246001

flugeiyamu@gmail.com

 

https://apps.tsn.go.tz/public/uploads/3018d5dd0adec538a4e6574bed090a34.jpg

UCHUMI na maendeleo ni mambo yanayohitaji kujengewa miundombinu ...

foto
Mwandishi: Felix Lugeiyamu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi