loader
Dstv Habarileo  Mobile
Jaji Siyani ajitoa kesi ya Mbowe

Jaji Siyani ajitoa kesi ya Mbowe

JAJI Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mustapha Siyani amejitoa kusikiliza kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka ya kupanga njama za ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe na wenzake watatu.  

Ametangaza kujitoa leo muda mfupi baada ya kutupilia mbali mapingamizi mawili yaliyowekwa na upande wa utetezi kwenye kesi ndogo ndani ya kesi kubwa.

Mapingamizi hayo yalihusu maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili katika kesi hiyo Adam Kasekwa, yasitumike mahakamani hapo kama sehemu ya ushahidi wa jamhuri na maelezo hayo yalitolewa baada ya Kasekwa kuteswa.

Katika uamuzi wake, Jaji Kiongozi Siyani amesema, kulikuwa na sababu ya msingi ya kutolewa nje ya saa nne kwa mujibu wa sheria na kuhusu kuteswa upande wa utetezi haujathibitisha hilo.

Siyani aliyekuwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma, alianza kusikiliza kesi hiyo Septemba 10, 2021, baada ya aliyekuwa akiisikiliza Jaji Elinaza Luvanda kujitoa.

Jaji Luvanda alitangaza kujitoa Septemba 6, 2021, baada ya washtakiwa wakiongozwa na Mbowe, kuomba ajitoe kwani hawana imani nae kwa kile walichodai kuwa hatawatendea  haki, ombi ambalo alikubaliana nalo.

Kwa upande wa Siyani, amejitoa ikiwa ni takribani siku wiki mbili zimepita tangu Rais Samia Suluhu,  alipomteua kuwa Jaji Kiongozi, Oktoba 8, 2021.

Siyani aliteuliwa kuchukua nafasi ya Eliezer Feleshi ambaye yeye aliteuliwa kuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Akitangaza kujitoa, Jaji Kiongozi Siyani amesema, kesi hiyo ikiwa itakwenda mfululizo itawachukuwa takribani miezi minne na kwa kuwa yeye kwa sasa ana majukumu, “nimeona nijitoe aje Jaji mwingine haraka iwezekanavyo.”

Baada ya kueleza hayo, Jaji Kiongozi Siyani ameahirisha kesi hiyo hadi Msajili wa Mahakama Kuu atakapompangia jaji mwingine na watuhumiwa wamerejeshwa rumande.

foto
Mwandishi: Mwandishi Wetu

Post your comments

Tangazo

CRDB

Habari Nyingine

Categories

habari zaidi zinazoendana na hii

mpya # zaidi